Habari zaidi!
Walimu waanza kulipwa
Mlacha na Waandishi Wetu Mikoani
Daily News; Tuesday,November 18, 2008 @21:15
Wizara ya Fedha na Uchumi imepeleka zaidi ya Sh bilioni 10 kwa halmashauri 132 nchini ili kulipa malimbikizo hayo ya madeni. Katika taarifa yake Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, alisema serikali inaamini kuwa ni walimu wachache tu ndio waliojitokeza kushiriki katika mgomo huo batili na aliahidi kuwa serikali itafanya kila iwezalo kutatua matatizo yanayowakabili walimu.
Serikali inapenda kuwahakikishia walimu wote nchini kuwa inathamini na kutambua kazi yao nyeti na muhimu kwa uhai wa taifa letu, alisema Luhanjo. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili mkoani Dar es Salaam, ulibaini kuwa walimu wengi walitii amri ya mahakama kwa kuhudhuria madarasani na kufundisha kama kawaida na ni baadhi ya walimu tu ambao walisaini na kuondoka bila kufundisha.
Mkoani Mbeya, halmashauri nane za mkoa huo hatimaye jana zilianza kutekeleza agizo la serikali kwa kuanza kulipa madai ya walimu. Akizungumza jana, Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Juma Kaponda, alisema halmashauri za wilaya tayari zimepokea fedha zilizotumwa kwa ajili ya malipo ya madai ya walimu, na mkoa huo umepokea Sh.636,507,723 kwa ajili ya kuwalipa walimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashasuri ya Wilaya ya Chunya, Maurice Sapanjo alithibitisha wilaya hiyo kupokea Sh milioni 39,997,523 fedha zitakazotumika kuwalipa walimu 148. Ofisa Elimu wa Jiji la Mbeya, Aulelia Lwenza alisema Halmashauri ya Jiji la Mbeya imepokea Sh milioni 56.3 ambazo zitatumika kuwalipa walimu 442, wakati Wilaya ya Kyela imepokea Sh milioni 162.9 kwa ajili ya kuwalipa walimu 262.
Wakati Serikali ikiwa imeanza kulipa madeni hayo ya walimu, zaidi ya walimu 300 wa Mkoa wa Mbeya huenda wakajikuta mikononi mwa sheria baada ya kudaiwa kughushi nyaraka zilizokuwa zinathibitisha madai ya zaidi ya Sh milioni 400.
Habari kutoka Tabora zinasema kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Tabora jana ilianza kuwalipa walimu madai yao ambayo wamekuwa wakiidai Serikali kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Hassan Mwanziku amesema kwamba tayari kazi ya kusaini hundi za malipo hayo imeshakamilika. Mwanziku ameeleza kuwa malipo hayo yanatokana na serikali kutuma pesa katika manispaa hiyo jumla ya Sh milioni 106 kwa ajili ya malipo ya walimu hao.
Amesema kwamba jumla ya walimu 519 katika Manispaa ya Tabora walitarajia kulipwa pesa zao jana na kutoa wito kwa walimu kuacha mgomo. Baadhi ya walimu hao wameishukuru serikali kwa kuwalipa mapunjo yao ya muda mrefu ambayo wengi walikuwa wameyasahau.
Akiwataka walimu kurejea kazini kutokana na amri ya mahakama Rais wa Chama hicho, Gratian Mukoba, aliwataka walimu kurejea katika vituo vyao vya kazi na kuendelea na kazi wakati CWT inatafuta suluhu zaidi ya mgogoro wao na serikali.
Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, kufuatia zuio la mgomo huo, lililotolewa juzi usiku na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Ernest Mwipopo. Tunatoa tamko hili huku tukifahamu kabisa kwamba bado walimu hawajalipwa madai yao ya likizo, matibabu masomo na uhamisho na wengi bado hawajapata madaraja stahiki, lakini tunaomba waendelee kufundisha kwa kuwa tunaheshimu sheria, alisema Mukoba.
Alisema kwa mujibu wa Mahakama Kuu Divisheni ya kazi, ilitangaza zuio la walimu kuendelea na mgomo, ili kesi ya msingi iliyofunguliwa na serikali inayohusu uhalali wa hatua zilizofuatwa na CWT kutangaza mgomo isikilizwe, jambo ambalo inabidi watii hadi hatua hiyo ikamilike kwani hawawezi kukata tena rufaa.
Alisema pamoja na uamuzi huo wa kusitisha mgomo, wanaamini kuwa mahakama hiyo haitatumia muda mrefu kusikiliza shauri la msingi bali itatumia kasi kama ilivyofanya pindi serikali ilipowasilisha ombi la kuzuia mgomo huo. Aidha alisema kitendo cha serikali kukimbilia mahakamani si suluhisho la kudumu katika kutatua mgogoro huo bali ingeshughulikia kikamilifu matatizo yote yaliyoorodheshwa katika notisi ya mgomo ya siku 60.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nestory Ngulla, alisema shirikisho hilo linaunga mkono mgomo wa CWT, kwa kuwa madai yao ni ya muda mrefu na serikali ilikuwa na muda wa kutosha kuyatekeleza.
Pia alikishutumu Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kulihusisha suala la mgomo wa walimu na siasa na kutoa tamko lao katika kipindi cha mgomo wakati tatizo hilo la madai ya walimu lilikuwapo muda mrefu na chama hicho kilikuwa kimya. Matamko yaliyojitokeza hivi karibuni kutoka CCM yanajaribu kutishia uhuru wa wafanyakazi katika kudai haki zao kwa mujibu wa sheria, jambo hili hatulikubali na tunalipinga kwa nguvu zote na kukemea, alisema Ngulla.
Aliiomba serikali kutambua kuwa suluhu ya mgogoro huo wa walimu ni kutekeleza madai yao ya muda mrefu na kuchukua hatua za kisheria na kiutawala kwa wale wote waliosababisha kucheleweshwa kwa malipo na si kutumia dola au siasa. Wakati huohuo, Polisi mkoani Dodoma, inawashikilia baadhi ya viongozi wa CWT Mkoa wa Dodoma kwa kosa la kushinikiza mgomo na kashfa dhidi ya viongozi wa serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dodoma, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Omary Mganga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja viongozi hao kuwa ni Fratern Kwahson (46) ambaye ni Katibu wa CWT Mkoa wa Dodoma, Romana Aloyce (50) Katibu wa Manispaa ya Dodoma na Lucas Luhombo, Mwenyekiti wa Manispaa ya Dodoma.
Mganga alisema watu hao walipita katika shule tisa za Manispaa ya Dodoma kwa lengo la kushinikiza mgomo kwa walimu na kwamba watu hao watafikishwa mahakamani muda wowote upelelezi utakapokamilika. Alitaja shule walizopita kuwa ni Shule ya Msingi Amani ambako walikuta wanafunzi wakiwa katika mtihani wa kumaliza mwaka na kuwashawishi walimu wagome, kitendo kilichopelekea wanafunzi hao kufanya mtihani mmoja tu.
Shule nyingine walizopita ni Changombe, Chamwino, Chinangali, Kiwanja cha Ndege, Mlezi Uhuru na Kaloleni. Maganga aliongeza kuwa katika uchunguzi wao waligundua katika simu za watuhumiwa hao kulikuwa na ujumbe wa simu unaomkashifu Rais na vyombo vya serikali. Wakati akitoa tamko, Rais wa CWT Mukoba, aliiomba serikali iwaachie walimu hao kwa kuwa walikuwa wakitekeleza mgomo ulio halali kabla ya amri ya mahakama kutolewa.