Kesho, zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura linafikia tamati.
Leo, nikiwa na muda wa kutosha nyumbani, niliona ni vema kuzunguka vituo vya kujiandikisha vilivyopo katika eneo langu la Buza ili nijionee hali halisi. Swali lililonisukuma kufanya hivyo ni moja:
Je, haki yangu ya kupiga kura itahakikishwa au nimepoteza muda wangu tu kujiandikisha?
Nikiwa mkazi wa Buza, kuna takriban vituo vitano vya kujiandikisha katika eneo hili. Nilipita kwenye vituo vitatu; kituo cha polisi cha Abiola, kituo cha polisi cha Buza, na ofisi za kata Buza kanisani. Katika kila kituo nilichotembelea, nilijiandikisha bila shida yoyote.
Hata hivyo, nilijiandikisha kwa majina tofauti katika kila kituo na kila sehemu walinikubali bila kuuliza maswali ya kina. Swali lililonijia kichwani ni hili: Hawa watu wanajuaje kama nimejiandikisha mara nyingi kwa kutumia majina tofauti?
Katika zoezi hilo la kujiandikisha, maelezo pekee niliyoulizwa ni jina langu na umri wangu – basi! Hivi kweli mfumo huu unazingatia nini? Nilipoona hali hii, nikajaribu kudanganya kwa makusudi, nikitaja majina na umri tofauti katika kila kituo, na bado nilikubaliwa bila kipingamizi.
Hii inadhihirisha jinsi mfumo wa uandikishaji ulivyo na mianya ya udanganyifu. Nilichokiona kikanitia shaka sana.
Wana-JF, Je, Tumewekewa Kiini Macho?
Sasa, najiuliza, je, huu mfumo wa uandikishaji upo ili kutimiza tu utaratibu wa kisheria au kweli unalenga kuhakikisha haki ya kila mwananchi?
Inavyoonekana, uandikishaji haujawekwa kwa umakini wa kutosha ili kuzuia udanganyifu na kuhakikisha uwazi.
Inawezekana kwamba hata wale wasio na nia ya kupiga kura wanaweza kudanganya bila kugundulika.
Nimezungumza na watu kadhaa wakati wa safari yangu ya leo. Mtazamo wa wengi ni kwamba, mara tu unapojisajili, tayari umepiga kura.
Kwao, kitendo cha kujiandikisha ni sawa na kupiga kura. Baadhi hata wanaamini kuwa ukijiandikisha na ukashindwa kwenda siku ya kupiga kura, kura yako imekwishahesabiwa.
Hii ni ishara ya kukata tamaa na kukosa Imani kama kweli kura yao Ina nguvu ya kufanya uamuzi wa kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Maoni Kuhusu Mawakala wa Uandikishaji
Katika vituo nilivyopita, mawakala wa uandikishaji walionekana kuwa pale tu kwaajili ya kutimiza jukumu walilopewa.
Hakukuwa na jitihada za kuhakikisha wale wanaojiandikisha wanatoa taarifa sahihi au kufuata utaratibu wa uandikishaji.
Wanaonekana kutekeleza kazi yao bila kujali kama taarifa zinazokusanywa ni sahihi au la.
Kesho, zoezi hili linafikia ukomo. Hili linanipa wasiwasi mkubwa kuhusu jinsi uchaguzi ujao utakavyokuwa.
Kama mfumo wa uandikishaji una udhaifu wa namna hii, je, tuko tayari kweli kwa mchakato wa uchaguzi ambao ni wa haki na wa wazi? Na je, tuna uhakika kiasi gani kwamba mianya haitapelea kupata kiongozi ambaye hatukumchagua Kwa kura zetu?
Ni vyema tukajiuliza: Je, haki yetu ya kupiga kura itahakikishwa au tutaishia kuwa wahanga wa mfumo unaoonekana kuwa dhaifu na unaoweza kuruhusu udanganyifu kwa urahisi?
Ni dhahiri kuwa kupitia mianya hii ya udanganyifu Kuna uwezekano mkubwa ukafanyika uchaguzi usio sawa na wa haki kwani watu wanaweza kupiga kura zaidi ya mara Moja Kwa majina tofauti na kumpa ushindi
wanayemtaka.