MKASA WA KWANZA - Sehemu ya 8.
Inaendelea.............
Yaani ndiyo nilikuwa nimeingia kulala tu hata usingizi haujaanza kunikolea,swichi ya taa mle chumbani kwangu ilikuwa mlangoni kabisa hivyo ukiwa unaingia ndani kama kuna giza unawasha swichi ndiyo unaendelea na mambo mengine,kitanda kilikuwa mbali na swichi ya kuwasha taa,hivyo nilishituka na kutazama mlangoni nikiwaza labda nilikuwa sijafunga mlango dada yangu atakuwa kaingia lakini cha ajabu sikuona mtu,ikanibidi niamke nikatazame mlango kama nimeufunga!.Mlango nikakuta nimeufunga,bado sikuelewa maana niliona taa kujiwasha yenyewe ni kitu kisichowezekana,ikabidi nizime tena ile taa nikarudi kulala.Mara ghafla tena baada ya muda kidogo kupita ile swichi nikasikia inawashwa!,bado sijajua ujasiri kipindi kile ulikuwa unatoka wapi maana nilipoamka nilitamka kwa sauti "Niacheni nilale,nimechoka msinisumbie".
Kumbe ile kauli yangu ya kijasiri ndiyo ilikuwa kama nimekoleza pilipili kichaa kwenye macho!,niliamka vizuri kama kawaida nikaenda tena kuizima ile taa nikaingia kulala,ile taa ikawashwa tena na safari hii nilipo enda pale kwenye soketi kuizima haikuzimika!.Akilini niliwaza nikajisemea naweza kuwa nawaza mambo mabaya kumbe ilikuwa ni masuala ya umeme tu!.Basi nikaingia kulala hivyo hivyo na taa ikiwa inawaka sikutaka mambo mengi japo nilichelewa kupata usingizi maana toka zamani kupata usingizi na taa ikiwa inawaka kidogo ni mtihani!,nilipopitiwa na usingizi nilishituka nimesukumwa kutoka kitandani,kabla ya kufika chini kulikuwa kuna meza ambayo nilikuwa nikiweka vitu vyangu,nikajikuta nimeishika ndipo ikapunguza kasi ya kujipiga chini kama gunia la viazi,nilipata maumivu ya kidole kidogo cha mkono wa kulia maana lilikuwa ni tendo la ghafla ambalo sikulitarajia,kidole changu kidogo cha mwisho cha mkono wangu wa kulia mpaka leo hii ninapoandika huwa kimepinda na hakisikii maumivu,chimbuko la hayo yote ni hilo tukio!.
Basi ilibidi niamke nikafungua mlango nikaenda kumgongea dada yangu mkubwa nikamwelezea kila kitu,kiukweli alishangaa sana,ikabidi yeye amgongee mlango mama mdogo aliyekuwa akilala na dada yangu niliyemfuatia,ikabidi niingie nilale kule,mle chumbani alipokuwa akilala mama mdogo na yule dada yangu,kulikuwa na kitanda cha kawaida na kitanda cha double,hivyo mimi nikapanda kitanda cha juu cha double kulala.Asubuhi kulipo kucha mama mdogo alitoa wazo ya kwamba kuna rafiki yake anafahamiana na mtaalamu mmoja wa tiba za asili,hivyo angempigia simu huyo rafiki yake amlete yule mtaalamu pale nyumbani!,lakini alisistiza ya kwamba tusije kuwaambia mama na baba.
Kweli!,baadae yule rafiki ya mama mdogo alifika na huyo mtaalamu,mtaalamu baada ya kuingia mle ndani na kuanza vitu vyake akaanza kutueleza mtiririko wa matukio mpaka hapo tulipofika,mtaalamu alituambia ya kwamba "Yule Ashura alikuwa ni mshirikina na alipoondoka kuna vitu aliviacha na vipo humo chumbani alimokuwa akilala, kwa macho ya kawaida si rahisi kuviona".
Pia akasema "Huyo mwanamke alikuwa na nguvu zisizo za kawaida mpaka yeye mwenyewe atakaporudi kuja kuvichukua ndipo hayo mauzauza yataisha lakini vinginevyo huu mziki mtaendelea kuucheza bila kupenda!"
Hapo ndipo nikakumbuka ile kauli ya dada Ashura siku anaondoka kwamba "Nitarudi",yule mtaalamu alituambia lazima dada Ashura arudi maana vitu vyake alikuwa kaviacha ndani,haijarishi atarudi kwa staili gani lakini lazima arudi!.Yule mtaalamu alisema "mimi siwezi kuvitoa hivyo vitu vyake na nikilazimisha nitafia hapa!".
Jamaa hakuchukua muda sana akawa ameondoka,kwahiyo mama mdogo alibaki sana na maswali,siku hiyo tukakubaliana kwamba mimi niwe nalala na wao mle chumbani maana bado mdogo!,basi ndiyo ikawa hivyo.Nakumbuka siku kadhaa zikiwa zimepita na baadhi ya matukio kupungua,siku moja nikiwa nimeingia bafuni kuoga nikiwa nimejipaka sabuni kuanza kujisugua,ile nimefungulia maji ya bomba la juu(Shower)nikiwa naoga vizuri tu,sasa ile nimemaliza nageuka nyuma ya mlango nichukue taulo nijifute maji ili niondoke mle bafuni,mara ghafla nikakutana na dada Ashura ana kwa ana,nilipiga kelele na kuanguka mle bafuni,sikujua kilichoendelea tena mpaka niliposhituka nikiwa hospitalini.Kuna hospitali moja ilikuwa inaitwa WENAN HOSPITAL,hili jina sijui kama lipo sahihi lakini ndiyo hospitali ambayo nilipelekwa kipindi kile na sijui kama bado ipo maana ilikuwa ni hospitali kubwa tu pale Tarime kipindi hicho.
Sasa hili tukio lilikuwa baya sana maana lilinilaza kitandani miezi 4 nikashindwa kwenda shule,Kwahiyo sikuweza kuelewa na sikukumbuka tena ni nini kilitokea mpaka mimi kuwa pale hospitalini,ilibidi baba yangu atoke Dar es salaam alipokuwa kahamishiwa kikazo,mama yangu naye alikuja kipindi hicho.Hali ilizidi kuwa mbaya sana pale hospitalini, ilibidi nirudishwe nyumbani kwanza,hapo hospitali nilikaa si chini ya wiki mbili,hivyo nikarudishwa nyumbani.Mpaka hapo nilikuwa sikumbuki ni nini kilichonitokea maana nilikuwa naulizwa ni nini kimenipata nashindwa kusema,nilikuwa sikumbuki chochote kile,kuna rafiki yake na mama alikuja pale nyumbani akamshauri mama akamwambia "Huyu mtoto kama kaanguka bafuni basi msipofanya namna mnampoteza".
Kweli,mama hakulaza damu,akawasiliana na shangazi yetu alikuwa akiishi Mwanza ambapo yule ndugu yangu alikuwa akikaa kwake,alipowasiliana na shangazi shida yake kubwa ni kumleta Mmmganga kutoka huko Mwanza.Kwa namna ambavyo hali haikuwa nzuri ilibidi iwe haraka,baada ya siku mbili yule mganga akawa kafika kutoka Mwanza,baba akaenda kumpokea stendi ya Tarime mjini.Yule Mganga alipofika hapo nyumbani baada ya kuniona alianza kucheka sana, hakuna aliyefahamu alikuwa akicheka kitu gani!.
Itaendelea.................