Mikoa ya Manyara na Arusha ndiyo inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha ukeketaji kwa 43%

Mikoa ya Manyara na Arusha ndiyo inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha ukeketaji kwa 43%

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
KUH; MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA KUPINGA UKEKETAJI DHIDI YA MWANAMKE NA MTOTO WA KIKE TAREHE 6 FEBRUARI, 2025



Dar es Salaam, 02 Februari, 2025

Ndugu wanahabari
, tarehe 6 Februari, 2025 kila mwaka ni Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kupinga ukeketaji dhidi ya mwanamke na mtoto wa kike. Kwa mujibu wa Taarifa za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS-MIS) ya mwaka 2022/23, kiwango cha ukeketaji kwa wanawake na wasichana wenye umri wa miaka 15-49 kimeshuka hadi 8% kutoka 10% kwa takwimu za mwaka 2015/16. Aidha, Mikoa ya Manyara na Arusha ndiyo inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha ukeketaji kwa 43% ikifuatiwa na Mara 28%, Singida 20%, Tanga 19% na Dodoma 18%. Mikoa mingine iliyobainika kufanya ukeketaji ni pamoja na Iringa kwa 12%, Morogoro 10%, Njombe 7% na Pwani 5%.

Ndugu wanahabari, uchambuzi wa kina wa takwimu pia umeonesha kuwa, kiwango cha ukeketaji kimepanda na kushuka katika baadhi ya Mikoa. Nitumie nafasi hii kuipongeza Mikoa na Wadau wote wa masuala ya Ukeketaji hususani kwenye Mikoa ambayo ukeketaji umepungua kwa jitihada kubwa waliyoionesha. Mikoa ambayo ukekeketaji umeshuka kati ya mwaka 2015/16 hadi 2022/23 ni pamoja na Mkoa wa Manyara ambapo, kiwango cha ukeketaji kimepungua kutoka 58% hadi 43%, Mkoa wa Dodoma kutoka 41% hadi 18%. Aidha, Mikoa ya Mara kutoka 32% hadi 28%, na Singida kutoka 31% hadi 20%.

Kwa upande mwingine, nitumie fursa hii kuwaomba Wadau wanaopambana katika eneo hili kwa uratibu wa Serikali kuendeleza juhudi za kukabiliana na ukeketaji kwa Mikoa ambayo kiwango kimeongezeka ikiwa ni pamoja na Arusha ambapo, ukeketaji umeongezeka kutoka 41% hadi 43%, Tanga kutoka 14% hadi 19%, Iringa kutoka 8% hadi 12% na Morogoro kutoka 9% hadi 10%.

Aidha, utafiti pia ulibainisha kuwa 55% ya wanawake waliokeketwa walifanyiwa vitendo hivyo na Wakunga wa jadi wakati wa kuzaliwa na 26% na Mangariba, 17% hawakujua nani aliwafanyia ukeketaji na 1% walikeketwa na Wataalam wa afya.

Ndugu wanahabari katika kutambua jitihada za Serikali yetu katika kukabiliana na ukeketaji, Umoja wa Afrika ulitoa fursa kwa Serikali yetu kuandaa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Kutokomeza Ukeketaji tarehe 9 hadi 11 Oktoba 2023 Jijini Dar es Salaam kwa kushirikisha nchi 25 zinazofanya ukeketaji kutoka Umoja wa Afrika, baadhi ya Nchi za Ulaya pamoja na Nchi za Amerika ikiwemo Marekani.

Hivyo, Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeendelea kutekeleza Maazimio ya mkutano huo yakiwemo; (i) Vijana kuungana na kuwa vinara katika kutokomeza ukeketaji (ii) Adhabu kali inatolewa kwa wanaofanya ukeketaji (iii) Wadau wa Maendeleo kusaidia kutokomeza ukeketaji (iv) Kuimarisha ushirikiano kutokomeza ukeketaji (v) Kuwe na jukwaa salama na huru la kujadili mapambano dhidi ya ukeketaji bila hofu na (vi) Matumizi ya vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, vipeperushi ili kupaza sauti kuhusu kutokomeza ukeketaji.

Ndugu wanahabari, Kaulimbiu ya maadhimisho mwaka huu ni; “Imarisha Ushirikiano; Kutokomeza Ukeketaji” ambayo, inahimiza Wanawake, Watoto wa Kike na Kiume, Jamii na Wadau wote kushirikiana ili kuwa na nguvu ya pamoja katika kutokomeza ukeketaji ambao si tu ni kinyume cha Sheria lakini pia ni kinyume cha haki za binadamu. Aidha, kaulimbiu hii inatambua kwamba umoja ni nguvu na katika umoja huo, tunaweza kutokomeza kabisa vitendo vya ukeketaji. Nitumie fursa hii kutoa rai kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wadau wote waliopo katika Mikoa inayoendeleza ukeketaji kuhakikisha maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika kwa ufanisi ikiwa pamoja na ;

Kuanzisha Madawati ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto katika Shule za Msingi na Sekondari ili kutumia jukwaa hilo kuelimishana kuhusu ukeketaji na kupokea taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vikiwemo ukeketaji, na

Kutumia vyombo vya habari hususan Redio za Kijamii na mitandao ya kijamii na wadau wao wote ili kuelimisha Wanawake, Watoto, Wazazi/Walezi, Ngariba, Wazee wa Mila, Viongozi wa Dini na Kijamii kwa ujumla kuukataa ukeketaji kwa kaulimbiu ya “Imarisha Ushirikiano; Kutokomeza Ukeketaji”


Dkt. Dorothy Gwajima (Mb)

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,

WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM
 
Back
Top Bottom