Middleborn
New Member
- Sep 11, 2021
- 1
- 1
Mimba za utotoni kikwazo kwa mabinti wengi vijijini
Habari wanajamvi,
Naomba kuwasilisha kwenu andiko hili kuhusiana na changamoto ya mimba za utotoni.
UTANGULIZI
Tunapozungumzia mimba za utotoni tunamaanisha ni ile hali ya kuwa na ujauzito kwa binti yeyote ambae hajatimiza umri wa miaka 18. Waathirika wengi wa tatizo hili ni mabinti walio katika rika la balehe ambao ni miaka 15 hadi 24.
Takwimu zinaonyesha kuwa tatizo hili limekuwa likiongezeka kila mwaka nchini licha ya kuwepo kwa sheria zinazotoa adhabu kali kwa wahusika kama vile kifungo cha miaka 30 jela au Maisha. Bado watu wamekuwa sio waoga kabisa. Nchini Tanzania, mwaka 2018, kati ya wasichana 10 wa kundi balehe, wasichana 4 walipata ujauzito. Kisiwa cha Ukerewe tatizo ni kubwa zaidi na inaelezwa ni miongoni mwa wilaya 3 za mkoa wa Mwanza zinazoongoza ikifuatiwa na Kwimba na Sengerema.
Katika andiko hili, nitaangazia mambo kadha wa kadha yanayosababisha na kuchochea ongezeko la mimba za utotoni, nini kinapaswa kifanyike. Haya yote yanatokana na uzoefu binafsi niliopata katika Maisha kutokana na kuishi katika mazingira husika.
SABABU ZINAZOSABABISHA MIMBA ZA UTOTONI
Ukosefu wa malezi ya wazazi:
Hili ni tatizo kubwa sana katika jamii zetu ingawa halitajwi kwa uzito unaostahili. Miaka ya nyuma sana kabla maendeleo ya sayansi na teknolojia hayajashika kasi, wazazi ndio walikuwa msingi wa malezi bora kwa watoto na jukumu hili lilifanywa na jamii yote. Mtoto alikuwa mali ya jamii. Mtu yeyote anaekuzidi umri alikuwa na uwezo wa kumkemea mtoto anapokuta anafanya jambo lililo kinyume na ustaarabu wa jamii. Mimi binafsi nikiwa kidato cha pili niliwahi kuadhibiwa barabarani na mzee mmoja jirani yetu baada ya kunikuta mjini nimevaa heleni. Wazazi wengi wameacha hili na kujipa jukumu la malezi wao wenyewe ilihali wakitambua uhalisia hata huo muda wa malezi hawana kutokana na kubanwa na majukumu mengi ya kikazi na biashara.
Hadi mtoto awe mtu mzima, alitakiwa kupita katika mikono ya wazazi bora, kupata mafundisho ya dini (shule za watoto za jumapili, jumamosi kwa wakristo na madrasa kwa waislamu), elimu dunia shuleni, elimu jamii kwa watoto wenzake (kikundi rika) na inaposhindikana kabisa ndio analazimika kuipata elimu hiyo kwa mujibu wa sheria ikiwemo magereza. Hapa mwisho ndio ule usemi wa wahenga kwamba asiefunzwa na ***** hufunzwa na ulimwengu.
Wazazi wengi wa karne hii wameelemewa na pilika za dunia. Sehemu kubwa ya malezi wameachiwa mabinti wa kazi za nyumbani na walimu. Ajira na biashara nyingi hazizingatii muda wa kupumzika. Changamoto ya foleni na usafiri mijini na umbali kwa kijijini vinachangia ongezeko la mimba za utotoni.
Ukosefu wa mahitaji ya msingi:
Hali ya kiuchumi kwa kaya nyingi hasa maeneo ya vijijini ni duni sana.Wengi wanaishi katika lindi la umasikini wa kutupwa kiasi cha kupelekea mabinti wengi kukosa mahitaji ya msingi kama taulo za kike, sabuni, mafuta na mavazi. Hii inachangia wengi wao kurubunika kiurahisi kwa wanaume wakwale wenye vijipesa vya mboga.
Katika maeneo ya visiwani, wasichana wengi walio katika kundi balehe huanza kujihusisha na ngono katika umri mdogo kutokana na mazingira wanayoishi kuwa na wafanyabiashara wengi wanaojihusisha na shughuli za uvuvi na mazao yatokanayo na uvuvi.
Tabia, mila na desturi:
Wengi wa vijana wa kiume, watu wazima na hata wazee wamejijengea tabia tu kwamba mabinti ni watamu kuliko wanawake. Zipo pia baadhi ya tabia katika jamii kuozesha mabinti wakiwa na umri mdogo kwa lengo la kujipatia mali. Hii huchangia ongezeko la mimba za utotoni na hata vifo vitokanavyo na uzazi.
Sheria ya ndoa:
Kumekuwepo na mjadala wa muda mrefu kuhusiana na sheria hii lakini muafaka haujapatikana hadi sasa. Sheria hii ya 1971 inatambua ndoa kwa binti wa miaka 14+ (kwa ruhusa ya mzazi) kinyume na sheria ya mtoto ambayo inatambua mtu yeyote chini ya miaka 18 ni mtoto.
Ukosefu wa usawa wa Kijinsia katika elimu:
Katika jamii zetu nyingi bado ile imani ya kuwa “kumsomesha mtoto wa kike ni kupoteza muda na pesa”. Tunaweza kushangazwa na jambo hili lakini ukweli kwamba nimetembea maeneo mengi ya wilaya ya Chemba, Kwimba, Ukerewe na Kahama ambako nimeshuhudia mabinti wengi wakikatishwa masomo na kuolewa.
Ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi na haki:
Binafsi niliwahi kushuhudia wafanyakazi wa taasisi moja wakiwekwa ndani kwa amri ya Mkuu wa Wilaya kwa kutembelea shule ya Upili ambako walidaiwa kukutwa wakifundisha elimu ya afya ya uzazi.
Bahati mbaya hata majumbani wazazi wengi hawapo tayari kuzungumza na mabinti kuhusu suala hili. Makanisani na misikitini pia haifundishwi. Wahudumu wa afya waliopo hawatoshi kuwafikia watoto hawa ambao wengi hupatikana jioni.
Hii inawafanya kundi balehe kuingia katika hali ya utu uzima wakiwa hawajui lolote kuhusiana na mapenzi wanayofata na hatimae kukutana na mimba zisizotarajiwa.
Ukatili wa Kijinsia:
Nilibahatika kuwepo Zanzibar kwa majuma kadhaa, sikushuhudia lakini niliambiwa tatizo la ukatili wa Kijinsia ni kubwa sana kiasi cha wazazi kuhofia hata kuwaagiza watoto wao madukani. Kwenye visiwa kama Ukerewe, wanaume huchukulia faida ya upungufu wa vituo vya polisi kufanya ukatili wa Kijinsia wakijua watamalizana na wazazi na watendaji wa vijiji au ikishindikana watakimbia na kwenda kuanzisha makazi sehemu nyingine.
Mabinti wanabakwa, wanafanyishwa biashara ya ngono na kuolewa katika umri mdogo hivyo kupelekea ongezeko la mimba za utotoni.
Biashara itokanayo na shughuli za uvuvi:
Kushamiri kwa biashara hii kumeendana na kuifanya kuwa kichocheo cha mabinti wengi kuanza ngono mapema kutokana na ukweli kwamba makundi yanayojihusisha na biashara hii hususani wavuvi, wachuuzi wa samaki na dagaa, mabondo, wafanyabiashara za maduka, magenge, migahawa na biashara nyinginezo wamekuwa watu wa “matumizi ya nguvu”. Wengi huamini samaki hawaishi ziwani/baharini. Hii imewavutia wanawake makahaba na wafanya biashara ya ngono kukimbilia huko kwa lengo la kujipatia kipato. Matokeo yake hata mabinti wadogo wamejiingiza kwenye ngono kwa lengo la kupata starehe, Pombe na kipato.
- NINI KIFANYIKE KUONDOA TATIZO LA MIMBA ZA UTOTONI
Wazazi warejee katika misingi waliyolelewa na wazazi wao. Tengeni muda wa kutosha kuzungumza na watoto wenu masuala mbalimbali ya mila na desturi, wafundisheni elimu ya afya ya uzazi na zaidi muwape muda wa kuwaeleza shida zao. Msipowasikiliza watasikilizwa na wanaume na kutatuliwa shida zao huko. Msisubiri kuuliza “mimba ya nani?”.
Unaweza kuwa bize kutafuta pesa ambazo hazina faida yeyote iwapo wanao watakosa malezi sahihi. Kula vizuri, kuvaa vizuri na kuwapeleka sehemu nzuri za starehe sio mahitaji pekee ya watoto.
Kukuza kipato cha kaya:
Hadi sasa, kwa sehemu kubwa, wazazi na walezi wasio na kipato kikubwa wamekuwa wakishauriwa kujiunga na vikundi vya akiba na mikopo. Hii ni njia sahihi ya kujiongezea kipato kwa kaya masikini. Pia, TASAF isogeze huduma zake kwa walengwa ili kuwanusuru wanakaya masikini. Maeneo mengi ya vijijini bado kuna utajiri mkubwa wa ardhi yenye rutuba. Serikali inaweza kupeleka wataalamu na maafisa ugani wengi zaidi ili kufundisha kilimo biashara kitakachowafanya kuondokana na kilimo cha mazoea.
Kuondoa mila, desturi na tabia potofu/zilizopitwa na wakati:
Hivi ni vitu vimedumu kwa miaka na miaka katika jamii na vikionekana kama ufahari. Inahitajika mikakati madhubuti na shirikishi itakayowezesha jamii zetu kubadilika na kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati.
Kurekebisha sheria kinzani (Sheria ya ndoa vs Sheria ya Mtoto):
Kama kuna uwezekano, serikali ilione hili kuwa ni tatizo katika jamii ili kuifanya ione umuhimu wa kubadili sheria kinzani na kutambua mtu yeyote chini ya miaka 18 ni mtoto. Kuendelea kuwa na sheria inayotambua ndoa za mabinti chini ya miaka 18 kwa kisingizio cha ruhusa ya wazazi inaacha mwaya mkubwa kuendelea kuwa na ongezeko la mimba za utotoni.
Kuongeza usawa wa Kijinsia:
Jamii na wazazi wapewe elimu zaidi juu ya faida za kusomesha watoto wa kike sawa na wa kiume. Serikali iongeze nafasi za wanawake katika vyombo vya utoaji maamuzi na elimu itolewe kwa usawa kwa watoto wa jinsia zote.
Kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa kundi balehe:
Yawezekana tukakubali kuendelea kujidanganya kwamba kuwafundisha watoto wetu wa kike walioko mashuleni elimu ya afya ya uzazi ni kuwakumbusha kufanya ngono mapema. Serikali itafute namna bora ya kuondoa changamoto hii.
Wazazi wapewe elimu hii kwa kuwa hata wao wengi hawafahamu ni kitu gani hasa wanapaswa kuongea na mabinti zao. Walimu pia kwenye masomo yao mfano Biology inaweza kuwa na mada ya afya ya uzazi. Vituo vya kutolea huduma za afya vitoe huduma rafiki kwa vijana ili kuwavutia na kuwafanya kuwa huru.
Kuzuia ukatili wa Kijinsia:
Serikali na wadau washirikiane kwa karibu kuondoa tatizo hili ikiwemo kuzuia mianya ya rushwa na kuweka karibu na makazi ya watu vituo vya pamoja vya kuwahudumia waathirika wa ukatili wa Kijinsia kama vile Ustawi wa Jamii, vituo vya afya, Polisi na mahakama.
Kuwashirikisha wanaume:
Wanaume ndio wahusika wakuu wa mimba za utotoni. Harakati, afua nyingi na mikakati imekuwa ikielekezwa kwa wanawake na kusahau kundi hili. Ni wakati sasa tuwashirikishe kwa karibu ili kuondoa tatizo. Kuwepo na mijadala ya Kijinsia itakayowezesha kupatikana kwa makubaliano ya pamoja katika jamii. Kupitia mijadala hii, jamii zinaweza kujiwekea sheria ndogo ndogo zitakazowabana watakaohusika na mimba za utotoni.
- HITIMISHO
Upvote
1