Sijui kwako ndoa ina maana gani lakini kwangu Mimi ndoa ilinipotezea Muda wangu, iliniacha na Maumivu na kilema cha Maisha yangu.
Sikuwahi kuwaza chochote kuhusu ndoa wala kuitamani, lakini siku moja nilikua natoka sokoni Mabibo naelekea nyumbani Magomeni Usalama, niliposhuka kwenye daladala kwa bahati mbaya niliteleza na kuanguka wakati navuka barabara. Mfuko wenye vitu nilivyonunua sokoni uliangukia pembeni.
Nilihisi aibu sana siku ile na kibaya zaidi mvua ilikua imenyesha majira ya asubuhi, lilijaa tope lililoniharibia Baibui langu. Eneo nililoangukia palikua na kijiwe cha Bodaboda. Kama uwajuavyo walianza kushangilia anguko langu kitu kilichozidi kunipa hasira lakini sikuwa na la kufanya zaidi ya kujiokotanisha pale.
βPole sana Dadaβ niliisikia sauti hii nikiwa nasimama, aliyenipa pole alinipatia na mfuko wangu akiwa ameokotanisha vitu vyangu. Alikua kijana mzuri mtanashati sana, nilijikuta nikiwa na kigugumizi kumjibu
βUnaelekea wapi?β
βNyuma ya sheli, usijaliβ nilisema nikiwa najipangusa tope kutoka kwenye Baibui langu jeusi, akanipa mkono wake
βNaitwa Salehe Mwinyimkuuβ Alijitambulisha kwangu, nilimtazama kwa sekunde kadhaa kisha nilimjibu
βNaitwa Saidaβ
βNimefurahi kukufahamu, wacha nikusogezeβ alisema, kwa msaada alionipa isingelikuwa hisani kukataa alichokiomba. Taratibu tuliikanyaga ardhi kuelekea karibu na nyumbani kwetu. Kwa muda mchache nilihisi kumjua kidogo, niligundua ni mpole, mwemye hekima na busara tele licha ya kuniambia ana Miaka 27 tu.
βMimi nina Miaka 23β nilijitanbulisha kwake huku nikianza kunogewa na mazungumzo yake. Tuliongea mengi hadi kubadilishana namba za simu kitu ambacho sikuwahi kukifanya kwa Mtu nisiyemjua.
Tulizidi kuwasiliana kwa zaidi ya mwezi mzima huku tukiwa marafiki wa kawaida tu lakini baadaye Salehe alinitongoza.
Nisiwe mwongo wala mnafiki hata kabla ya kunitongoza nilianza kumpenda hivyo kunitongoza alikua anatimiza wajibu wake kama Mwanaume kwani nisingeliweza kumwambia Nampenda isitoshe Mimi nilikua Bikra kwa wakati ule.
Tulianza mahusiano ya Kimapenzi lakini nilimwambia Salehe kuwa Mimi nimelelewa kwenye familia ya Dini sana, Baba yangu ni msaidizi wa Shekh Mkuu wa Msikiti wa Magomeni hivyo kama ananipenda kweli basi awaone wazazi wangu kwanza. Sijui tuseme alikua na kiu sana au alikua anahitaji Mke sana maana alilifanya hilo siku tatu tu baada ya kumwambia
Baba yangu alifurahi sana, Mama pia alifurahi zaidi akaniambia
βMwanangu ndoa ni Nusu ya Dini, sisi Wazazi wako tunakutakia kila lililo jema, Mungu akuongozeβ Daima Mama yangu alikua Mtu wa karibu sana kwangu, alisimama na Mimi kwenye kila jambo hata ambalo Baba yangu alipingana na Mimi.
Salehe hakutaka kuchelewesha alilipa Mahali siku iliyofuata.
βWewe Kijana ni Mtu wa wapi?β Baba alimuuliza Salehe wakiwa katika mazungumzo ya kawaida, kama Mzazi ni lazima ahakikishe usalama wa Binti yake
βKwetu Rukwa lakini nipo Hapa Dar Likizoβ alisema Salehe
βOoh! Unajishughulisha na nini?β
βNimeajiliwa, Mwalimu wa Shule ya Msingi Rukwa Mjiniβ
βUtamtunza Binti yangu?β
Kwanza Salehe alicheka kidogo kisha akamwambia Baba
βNisipomtunza Mke wangu nitamtunza Nani, wanasema Mbuzi unayemlisha ndiye utakaye mkamua maziwaβ Basi Baba na Salehe wakaishia kuangua vicheko, ilileta raha sana.
Ndugu wa Salehe walifika tena waliazimia kuwa ndoa ipite kabla likizo ya Salehe haijaisha ili tuondoke wote kuelekea Rukwa, sikuwahi kufikiria kuwa siku moja nitaolewa na kwenda mbali kama Rukwa. Kidogo nilipata huzuni, nilimzoea Mama yangu
βUsijali, hata Mimi niliwaacha Wazazi wangu Morogoro nikaja kuishi na Baba yako Saida. Umri ukifika hakuna la kukuzuia kuanzisha Familia yakoβ Mama yangu hakuacha kunitia Moyo. Baba aliachia tabasamu maana tulikuwa wote sebleni
βNgoja niwaache muongee maongezi yenu ya kikeβ alisema Baba akaelekea zake Msikitini, zilipita siku kadhaa hadi siku ya ndoa ilipowadia. Ndoa ilipita salama, Siku ya pili tulianza safari ya kuelekea Rukwa Mimi na Mume wangu Salehe.
Bado nilikua Bikra wala hakunigusa usiku wa kwanza wa ndoa yetu hotelini kabla ya Kuanza safari, kwakua nami nikikua mgeni wala sikudai chochote kile. Tulifika Rukwa Usiku sana tena nikiwa ninasinzia, tulichukua Taxi hadi nyumbani kwa Salehe
βKaribu nyumbani Mke wangu, jisikie uko nyumbani kabisa na hapa ndipo tutakapoishiβ alisema tukiwa tunashuka kwenye taxi, tulisimama mbele ya nyumba moja iliyo giza sana, sikushangaa sababu mwenye nyumba hakuwepo kwa muda mrefu. Nilijiegemeza kwenye bega la Salehe nikamwambia
βMume wangu, ulipo nipo na nitaendelea kuwepo siku zoteβ lile Taxi liliondoka, kazi ya kuhamishia mabegi ndani ilianza. Salehe alikua ametangulia nami nilibakia nyuma nikikokota begi. Sijui ni mawazo yangu au nilisikia kitu halisi kabisa, nilisikia sauti za Watoto wakiomba Msaada
βSubhannahβΌβ nilishtuka, sikuisikia tena ile sauti maana mwanzo ilitokea ndani ya ile nyumba ambayo tulikua tukielekea. Mapigo ya moyo yalinienda mbio, niliposikiliza vizuri wala sikuzisikia tena nikajua ni fikra zangu tu. Basi niliendeelea kuvuta begi hadi ndani, taa zikawashwa
Palikua kimya sana, uzuri sikua na njaa wala hamu ya kula zaidi ya Kulala kutokana na Uchovu wa safari. Nilisimama kusuburia Salehe anioneshe chumba chetu, akaufunga mlango kisha akaniongoza hadi chumbani, nilipofika nilijitupa Kitandani na kujilaza kama pono bila kujali kuwa kitandani palikua vumbi tupu.
Nililala Usingizi wa nusu kifo hadi mapambazuko, sauti ya jogoo kuwika niliisikia ikiniamsha na kuniambia ni muda muafaka wa kuanza majukumu ya nyumbani. Macho yalijawa na Ukungu usio kifani, nilijinyoosha kama Kinda la ndege halafu nikajikuta nikipigwa na Butwaa zito sana ambalo kiukweli nilishangazwa mno na nilichokiona
βNipo wapi hapa?β Nilijiuliza swali hili, niliipapasa akili yangu inikumbushe jambo lakini haikua tayari kufanya hivyo, Salehe hakuwepo Kitandani. Moyo ulinienda hali Jojo, nilinyanyuka taratibu kutoka kitandani.
Nitakueleza kwanini nilipigwa na Butwaa la ajabu, kwanza harufu ya Udi wenye harufu mbaya ilizagaa kote ndani, pili nilisikia sauti ya Mtu akitwanga na kwa hakika alikua akitwangia ndani halafu sauti ya Mtoto Mchanga anayelia nilizidi kuisikia. Taratibu nilitaka kujuwa nipo wapi haswa maana tayari nilianza kupata hofu fulani
Nilipiga hatua za taratibu hadi mlango wa kutokea chumbani, ile sauti ilitoweka na palikua kimya sana. Moyo wangu haukutulia kabisa licha ya ukimya wa ghafla niliousikia, jua lilikua tayari limeshatoka
Nyumba ilikua safi sana. Ilikua na korido ndefu yenye vyumba kadhaa japo kwa wakati huo sikuhesabu kutokana na hali niliyokua nikiihisi. Basi Mimi Saida nilijiuliza
βAh ni mawazo gani haya Jamani, Ewee Allah niepushie Mbaliβ nilisema kisha nilirudi Chumbani kutafuta simu yangu nimpigie Salehe aniambie alipo si unajua maisha ya Ugeni yanavyoanza. Nilikumbuka mara ya mwisho simu niliiweka kwenye mkoba wangu
Sikuwa na shaka sana kuhusu simu yangu, niliikuta lakini kwa bahati mbaya ilikua imeisha chaji. Niliketi kitandani nikiwaza mambo kadhaa lakini niliona ni bora niweke simu chaji niwasiliane na Salehe
Nilipomaliza kuweka chaji na kuhakikisha simu yangu inaingia chaji nilipata nafasi ya kukiangalia kwa uzuri chumba, kilipangwa vizuri sana hadi nilijikuta nikitabasamu, nilijuwa ni Mume wangu Salehe alikua ameamka mapema na kuweka mazingira sawa. Nilijiona ni mwenye Bahati sana kuitwa Mke wa Salehe, nilikua na nguo zangu zilezile nilizokuja nazo hivyo wazo la kubadilisha nguo lilinijia lakini kabla ya kufanya hivyo nilisikia Mlango wa nje ukigongwa.
Sikujua naanzia wapi kuitikia wito huo, nilisogea hadi mlango wa chumba na kusikiliza vizuri. Mgongaji wa mlango alikua ni Mwanamke na sauti yake ilikua karibu sana hivyo kwa haraka niliamini anagonga mlango wa Nyumba ya Salehe. Hakuna aliyeitikia ile hodi hadi pale nilipoamuwa kumkaribisha nikiwa ndani tena kwa sauti ambayo aliisikia vizuri, nilijiangalia kama nilikua nipo sawa kutoka ndani kisha nilianza safari mara moja kutembea kwenye korido kuuelekea Mlangoni.
Niliufungua mlango wa kwanza kwa kutekenya kitasa tu kisha nikauelekea mlango wa Uwani ambao ndio mgongaji alikua hapo, nilipoufungua nilikutana na Mama Mmoja aliyebeba tenga la mboga mboga kichwani, alikua ameshakata tamaa alikua akiondoka nikamwita
βMamaaaβΌβ alipogeuka alirudi hadi Mlangoni
Shikamoo Mamaβ nilimsalimia kwa adabu, ndivyo nilivyofundishwa kwetu kwa wazazi wangu, yule Mama alitabasamu kisha akaniuliza
βHauchukui Mboga leo?β Nilitabasamu maana aliuliza kana kwamba alishawahi kuniuzia mboga ila nilielewa Lugha ya Kibiashara huwa hivyo mara zote
βMimi ni mgeni hapa Mama, labda kesho nikiwa nimeyafahamu vizuri mazingira naweza kuchukua. Usiache kupitishaβ nilisema kisha yule Mama aliondoka huku akiitikia
βNapita kila siku Mtaa huu, Wahiiii mboga mbogaβ alienda mbele zaidi kisha alitokomea machoni pangu. Kuzungumza na yule Mama ni kama kulinisahaulisha kuhusu Salehe lakini alipoondoka nilijiuliza
βSalehe ameenda wapi mbona hajaniaga?β Niliufunga mlango kisha nilirudi ndani, Nyumba ilikua kubwa ya Kisasa lakini ilikua kimya sana sikusikia hata sauti ya ndege kuruka. Uwani
palikua na sehemu ya kukaa nikaona ni bora nikae hapo kwanza nipate upepo, nilijikuta nikipitiwa na Usingizi wa ghafla tu.
Ndoto za hapa na pale zilinifuata usingizini na kunipa hekaheka hadi nikashtuka. Niliposhtuka nilikutana na sura mbili, moja ilikua ya Salehe na nyingine ni ya Mzee mmoja mweusi aliyevalia Baraghashia nyeupe na kanzu nyeupe. Macho yao yalikua kwangu
βEeeh imekuaje umelala hapo Mke wangu?β aliniuliza Salehe, nilijitabasamisha kidogo kama Mtu anayezuga ili asinione kuwa mvivu
βHewa ya hapa inavutia, kaupepo nikajikuta nasinzia tuβ
βSawa, huyu ni Baba yangu anaitwa Mzee MwinyiMkuu. Ni Baba yangu Mzaziβ alisema Salehe, nilimsalimia yule Mzee kwa heshima sana hata naye alifurahia na kuona ni namna gani nina heshima.
βMarhaba Mkwe wangu mzuri, hakika Mwanangu hakukoseaββ akasema kwa Utani tukajikuta tukicheka kidogo
βSamahani, najua umenitafuta ila nilienda kumpokea Baba maana aliniambia nikirudi tu atakuja kwa ajili ya kukusalimia wewe Mke wanguβ alijielezea Salehe, ni kweli Mzee MwinyiMkuu alikuja na begi dogo la Mgongoni lililochakaa sana.
Aaaah! Nimefurahi sana kumuona Baba yako Salehe, karibu Baba.β Nilisema kisha nilisimama na kulishika begi la Mzee MwinyiMkuu ambalo lilikua sakafuni, kabla sijaliinua yule Mzee alinishika mkono kwa nguvu sana hadi nilishtuka, nikamtazama Usoni alikua amenikazia sura yake
βHili begi halishikwi na kila Mtu, Salehe unajua pa kulipelekaβ alisema Mzee MwinyiMkuu, nilihemwa maana sikutegemea lakini hata kama ningelichukua ningelipeleka wapi wakati na Mimi ni Mgeni pale. Nilishusha pumzi, kilinishuka nikarudi kukaa, Salehe akaniambia
βMzoee Baba yangu ana utani sana Saida, wacha nikaweke begi lake nakujaβ Mara moja alipomaliza kusema alinyanyuka Salehe na kuelekea ndani, yule Mzee hakuacha kunitazama kwa jicho kali kama vile kuna kitu nimeharibu hadi nilianza kumwogopa, ikanilazimu kumwomba Msamaha
βSamahani Baba sikujuaβ
βSiku nyingine uwe unauliza, umeelewa?β
βNdiyo Babaβ Nilipomjibu alinikata jicho fulani la husda kisha akatoa mguno fulani wa kicheko cha dhihaka halafu akanyanyuka na kuiburuza kanzu yake akaingia zake ndani,nilishusha pumzi zote kama Mgonjwa wa Pumu. Niliusikia moyo wangu namna ulivyoamka nakuanza kudunda tena, hata koo ilianza kupitisha mate kwa kasi. Yaani sijui nikueleze vipi unielewe namna nilivyokua nimeshikwa na woga kupitiliza, sura ya yule Mzee niliyona imekaa kikatili sana
Wakati naendelea kujiuliza mara Mume wanu Salehe alirudi kutoka ndani, akaketi mahali alipokua ameketi Baba yake
βBaba yako ni Mkali sana Salehe hadi nimeogopa. Nimefanya kipi kibaya, kumsaidia Begi ni vibaya eti?β Nilimuuliza Mume wangu, yeye akanishika bega akaniambia
βUtamzoea, si unajuwa wazee wa zamani. Pengine hakutaka wewe ushike begi kwasababu zilizo kaa kitamaduni tu za Kizamani au kabila letu lakini ni mcheshi utamzoea kwa muda atakaokaa hapa.
βIna maana atakuwa anaishi hapa na Sisi?β
βNdiyo, ila muda mchache tu atakua ameondoka. Vipi umeshakula?β Basi kuzungumza na Salehe kulinifanya nisahau kilichotokea, tuliongea sana hadi Mchana tuliposikia adhana. Salehe akawa wa kwanza kunikumbusha kufanya Ibada, nilitabasamu nikashusha pumzi kidogo huku dimpozi zangu zikionekana