Wakati mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unafanyika mjini Beijing, wataalamu na wachambuzi wa mambo ya ushirikiano wamekuwa wakifanya mapitio ya baadhi ya miradi inayotekelezwa na China barani Afrika, na matokeo yake kwa uchumi wa nchi hizo. Kinachoonekana ni kuwa uwekezaji huo, mbali na kuongeza nafasi za ajira, na kuboresha maisha ya wenyeji, pia umekuwa ukiendana na mahitaji ya sasa ya dunia, yaani kupunguza utoaji wa hewa ya kaboni.
Kwa muda wa zaidi ya miongo miwili tangu baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lianzishwe, moja kati ya maeneo makuu yaliyopewa msukumo kwenye ushirikiano ni uwekezaji wa moja kwa moja (FDI). Mwaka 2003, yaani miaka mitatu tu baada ya kuanzishwa kwa FOCAC, uwekezaji wa moja kwa moja wa China barani Afrika ulikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 75, na takwimu zilizotolewa hivi karibuni zinaonesha kuwa mwaka 2022 uwekezaji huo ulifikia dola za kimarekani bilioni 5.
Kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, katika kipindi hicho hicho, China imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika, na hasa nchi za Afrika kusini mwa sahara, ambapo takriban asilimia 20 ya mauzo ya nje kwa nchi hizo yanaenda China, na karibu asilimia 16 ya bidhaa zinazotumiwa barani Afrika zinatoka China, na hadi kufikia mwaka 2023 thamani ya biashara kati ya pande hizo mbili ilifikia dola za kimarekani bilioni 282.
Kinachofurahisha zaidi kuhusu uwekezaji wa moja kwa moja wa China barani Afrika katika kipindi cha FOCAC, sio tu ongezeko kubwa la tarakimu, bali ni ongezeko la pande zote lenye manufaa kwa wenyeji. Mwanzoni wakati uwekezaji wa China unatiririka kwa kasi zaidi kwenda barani Afrika, kulikuwa na kelele kutoka nchi za magharibi kuwa baadhi ya makampuni ya China yaliyowekeza barani Afrika yalikuwa yanapora ajira za wenyeji, lakini miradi mingi inayotekelezwa sasa na China barani Afrika kwa sehemu kubwa inatumia nguvu kazi ya wenyeji, na kuwa moja ya vyanzo muhimu vya ajira kwa wenyeji. Mfano wa hivi karibuni ni ule wa ujenzi wa reli ya SGR ya Kenya ambapo zaidi ya asilimia 80 ya watu walioshiriki kwenye ujenzi huo ni wenyeji.
Jambo lingine la kutia moyo ni kuwa uwekezaji wa China pia umekuwa ukibadilika, zamani uwekezaji ulijikita zaidi katika ujenzi wa viwanda vinavyotumia nguvu kazi nyingi, lakini sasa kumekuwa na viwanda vinavyochanganya teknolojia za kisasa na nguvu kazi, kwa mfano viwanda vya vifaa vya kielektroniki kama simu, kompyuta, majokofu, feni nk. Kwenye viwanda hivi wataalam wa China wanashirikiana na wenyeji ambao licha ya kupata ajira pia wanapata ujuzi wa matumizi ya teknolojia za kisasa.
Ikumbukwe pia kuwa mwanzoni suala la uchafuzi wa mazingira lilitumiwa sana na vyombo vya habari vya nchi za magharibi, lakini uwekezaji ambao umekuwa ukifanyika zaidi katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukizisaidia nchi nyingi za Afrika kuendana na wakati kwenye suala la kukabiliana na ongezeko la joto duniani. Kwa mfano, miradi ya kuzalisha umeme kama ile ya Bui nchini Ghana na Karuma nchini Uganda, imetajwa kuwa ni miradi ya uzalishaji wa umeme kwa maji ambayo haichafui hewa. Hii ni tofauti na miradi kama hiyo iliyokuwepo kwenye nchi hizo kwa muda mrefu ambayo inatumia mafuta ya dizeli ambayo yanachafua hewa.