Mizania ya siasa, uchumi kwa mlalahoi
Bakari Mohamed
MARA zote mfumo wa uhai wa maisha ya binadamu huongozwa na utashi wa siasa-uchumi.
Hata pale mwanzo binadamu alipoumbwa na kuachwa uwandani kwa mujibu wa kanuni za kimaumbile, aliwajibika kujitafutia riziki yake kwa jasho lake!
Hii ilikuwa, imekuwa na itaendelea kuwa ndiyo njia ya mwenendo wa binadamu hata pale atakapomaliza siku zake za kuishi kwa mujibu wa kanuni zinazotawala maisha ya binadamu.
Kwa kuwa binadamu ni kiumbe wa kijamii na anawajibika kuishi kijamii kama wanajamii wengine wanavyoishi, basi ni wajibu kwa binadamu huyo kufuata sheria, taratibu na kanuni za kimaumbile kwa jinsi ya mwenendo murua wa maisha ya kijamii na ya kibinadamu.
Hata hivyo, kwa sehemu kubwa mwenendo murua wa maisha ya kijamii kwa sehemu kubwa ya wanajamii wa dunia, Tanzania ikiwemo, umeharibiwa na ufisadi (uharibifu) wa mizania ya siasa-uchumi.
Makala hii kwa jinsi ya kifalsafa na kisayansi (uchunguzi na mantiki) yatajaribu kuonyesha jinsi mizania ya siasa-uchumi kwa mlalahoi ilivyovurugika na kuwafanya watu maskini (walalahoi) kuishi maisha ya msoto na yenye dhiki na taabu nyingi za maisha ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Kwa sehemu kubwa, mlalahoi amegeuka mtumwa wa nafsi yake na anatumika kinyume na utashi wake wa uhuru, haki na usawa. Mlalahoi hana jinsi ya kujinasua na kwa jinsi hiyo analazimika kukubali maumivu ya mbinyo wa maisha ya shida na taabu nyingi hata kama kwa shingo upande!
Japokuwa binadamu ameumbwa kwa taabu bado anahitaji maisha ya staha na yenye kuzingatia utashi wake kama mtu. maisha bora kwa kuzingatia chakula bora na cha kutosha, malazi bora na yenye faragha, afya bora na endelevu, huduma bora na endelevu za kijamii, mavazi yenye heshima na sitara kwa rika zote, na siasa inayoendeshwa kwa uhuru, haki na usawa baina ya makundi yote ya kijamii.
Kwa ujumla, maisha ya kiumbe wa kijamii (binadamu) yanahitaji ustaarabu wa utu na heshima inayozingatia utu wake. Huu ndio mwenendo wa ustaarabu juu ya kufikia saada ya maisha ya staha na raha kwa mujibu wa kanuni za kimaumbile.
Mlalahoi, kama anavyotafsiriwa kwa maana ya neno, ni mtu mwenye maisha duni kutokana na kuwa na kipato kidogo. Mlalahoi ni mtu mwenye fursa chache na au zisizoweza kutumiwa kabisa katika kumuongozea tija na saada kwenye mzingo wa maisha yake kama kiumbe wa kijamii.
Kwa ujumla, walalahoi ni wale wote wanaoishi kwa taabu na dhiki za maisha zinazotokana na mbinyo wa ufinyu wa fursa za kiuchumi hali inayosababishwa na mizani ya siasa-uchumi kuzidi upande mmoja.
Hususan, siasa isiyozingatia maslahi ya walalahoi kutumia fursa za kiuchumi kwa maslahi binafsi ya watu wachache kwenye mfumo wa siasa-uchumi.
Inawezekana wasomaji wakadhani ulalahoi ni hali ya kukosa kazi na au hali ya kujishughulisha na kazi (zisizo rasmi) na zenye kipato kidogo na au kisichokidhi haja kiuchumi. La hasha, ulalahoi ni hali ya jumla ambayo mtu (yeyote na wa kada yoyote ile) anaposhindwa kukidhi mahitaji yake muhimu ya kila siku kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi.
Kwa jinsi hiyo, hata wafanyakazi (wa sekta ya umma na au binafsi) wanaolipwa ujira (mishahara) usiyokidhi maisha yao ni walalahoi! Hawa ndio wale wanaominywa na kusubiri mwisho wa mwezi ilhali wamezongwa na madeni huku na huko.
Maisha ya mlalahoi yamegubikwa na tamaa ya kupata kwa bahati nasibu (sadfa) japokuwa ni nadra kufanikiwa. Mlalahoi mara zote haishi kuitesa saikolojia (akili) yake kwa kufikiria mawazo mzunguko yanayomsababishia msongo wa mawazo hatimaye kumtia magonjwa kama shinikizo la juu la damu, tumbo kujaa hewa, na hata vidonda vya tumbo kutokana na fikra mzunguko zisizokuwa na suluhisho!
Mlalahoi anataabika na njaa ya kutaka kushiba kwenye mfumo ambao kwa jinsi yake ataendelea kuota ndoto za maisha bora ilhali siku za uhai wake zikipungua kwa kasi kwa kuzongwa na madeni yasiyolipika!
Mlalahoi hata kama ataonekana na afya (siha) njema ya kiwiliwili. Ieleweke kuwa akili (saikolojia) yake inaumwa maradhi makubwa na yasiyokuwa na tiba (hata kwa kikombe cha Babu wa Loliondo).
Maradhi ya akili ya mlalahoi ni kule kuota ndoto ya maisha bora hata kwa kudanganywa kujengewa "ghorofa angani" kama alivyokuwa akiota Abunuwas (kwenye Hekaya za Abunuwas). Mlalahoi ni mtu aliyekata tamaa ya maisha na hivyo haonekani kujitoa kwenye mzingo wa fikra mzunguko hadi pale atakapopata fikra ya ukombozi na kuipindua akili yake.
Kwa kuwa sehemu muhimu ya maamuzi yanayoweza kumponya mlalahoi juu ya maradhi ya fikra mzunguko na au mawazo mgando yanayomtweza nguvu hata kujiona ni dhalili asiye na jinsi, ni fikra-huru; na kwa kuwa mlalahoi hana budi kuleta mapinduzi ya fikra ili kuondokana na unyonge wake.
Kuna kila sababu kwa mlalahoi kuchukua nafasi yake ya kutumia fursa zinazomzunguka katika kupambana na mazingira yasiyo rafiki kwa mustakabali wa maisha yake na ya jamii yake sawia. Mlalahoi lazima apambane na fikra hasi ili azibadilishe na kuwa fikra chanya katika kujenga mizania sawa ya siasa-uchumi.
Tuchukue kundi kubwa la walalahoi, kama mfano wa kwanza, wakulima maskini wa vijijini. Hili ni kundi kubwa linalokadiriwa kufikia asilimia zaidi ya 75 kwa mujibu wa takwimu zinazokubalika Tanzania.
Wakulima walalahoi wa Tanzania wametelekezwa na wamejitelekeza kwa muda mrefu na wamebaki kuimba nyimbo zilezile za "TANU yajenga nchi" ilhali wachache wamekwisha imomonyoa (kwa pupa na ulafi) keki (tamu) ya taifa!
Wakulima vijijini wamebaki na jembe lilelile la mkono (kiserema) la tangu enzi za ujima! Wakulima wamesahaulika na wamejisahau, hakuna wa kuwatetea japokuwa wanaalikwa kuhudhuria karamu ya "Kilimo Kwanza" ilhali wenye tai shingoni ndiyo waalikwa!
Ana nini mkulima zama hizi? Ni suala linaloweza kuwakera wapanga sera, hata hivyo, ukweli utabaki kuwa wakulima walalahoi (wadogo) ndio waliyotelekezwa na nguvu ya serikali imeelekezwa kwa wakulima wakubwa na wa kati wenye nafasi za mtaji (na elimu ya ujasiriamali) ambao kwa sehemu fulani ndiyo wanaokopesheka na taasisi za fedha na au ndiyo wanaowanyonya wakulima wadogo kwa kuchuuza mazao yao yakiwa shambani kwa kisingizio cha kuwatafutia masoko ya uhakika.Mkulima mlalahoi amebaki shambani ilhali mazao yake yakichuuzwa kwa bei ya ubwete na walanguzi!
Kundi la pili, kama mfano, ni la wafanyakazi wa kada za chini. Kwa ujumla, wafanyakazi wa kada za chini na wale wanaoitwa wafanyakazi vibarua kwenye sekta za umma na binafsi wamekuwa wakisota msoto mbaya mbele ya waajiri wao.
Maisha ya wafanyakazi hawa hutegemea kipato cha mwisho wa mwezi. Hata hivyo, sio mwisho wa mwezi ule unaoweza kumfanya mfanyakazi aweze kumudu maisha ya siku angalau ishirini na tano za mwezi kwa kujikimu kwa mahitaji yake muhimu kama vile chakula, kodi ya pango la nyumba, matibabu, elimu ya watoto wake, na hatimaye kujiwekea akiba.
Kipato cha mfanyakazi malalahoi ni kiduchu ambacho kwa jinsi yoyote hakiwezi kukidhi mahitaji muhimu ya mwezi mzima.
Hapa ndipo mfanyakazi mlalahoi, atake asitake, anapowajibika kuingia kwenye msongo wa kukopa madeni hata kama yenye riba kubwa.
Pamoja na kukopa kwenye taasisi za fedha kama mabenki, wengi wa wafanyakazi walalahoi wa umma na wa binafsi wanakopa kwenye maduka mbalimbali yanayouza bidhaa za mahitaji ya kila siku.
Kwa ujumla, na ukweli usiopingika ni kwamba sehemu kubwa ya wafanyakazi walalahoi wana madeni kwenye maduka hata ya mitaani wanakoishi.
Kwa wale waliobahatika kufanyakazi za kada za juu na kada za kati kwenye taasisi za umma na au za binafsi wanapata walau kiasi cha kumudu maisha ya kifamilia kwa sehemu fulani ya maisha.
Hata hivyo, kwa jinsi ya maisha ya kijamii yalivyosukwa na jinsi wananchi wa Tanzania wanavyoishi kijamaa kuna kila sababu ya kudhani kwamba wale wote wenye nafasi ya mishahara mizuri kiasi wana kila sababu ya kuishi maisha ya kujitolea na au kujikamua ili kusaidia jamii zao katika kugawana umaskini na ulalahoi.
Wengi wa watu wenye mapenzi mema na ya kijamaa (kiukoo na au kifamilia) wanafanyakazi ya ziada katika kusaidia watu wa jamii zao kwa jinsi wanavyoweza.
Pamoja na ukweli huu, kuna hali ya ubinafsi iliyojengeka baina ya watu na jamii zao hali inayofanya sehemu kubwa ya maisha ya wananchi walalahoi kuwa kwenye mashaka makubwa kwa vile wanaonekana kama ni waliyokosa matumizi mazuri ya fursa.
Sehemu ya watu wenye bahati ya kuwa kwenye mduara wa ndani wa maisha bora na yenye raha wanadhani kwamba huo ni ujanja wao na wanasahau kwamba walalahoi wamefanywa hivyo na mfumo usiyozingatia mizania ya uhuru, haki na usawa juu ya siasa-uchumi.
Siasa-uchumi isiyozingatia uwiano wa matumizi ya uhuru, haki na usawa juu ya fursa na rasilimali katika kujenga jamii ya watu waliyo sawa na huru ndiyo iliyofanya kuwepo kwa kundi kubwa la walalahoi na kundi dogo la matajiri wanyonyaji wanaonyonya jasho la walalahoi wengi wa mijini na vijijini.
Haya yalishuhudiwa na mwanafalsafa wa sayansi ya uchumi-jamii, Vilfredo Pareto alipofanya utafiti na kuthibitisha kwamba asilimia 20 ya watu wanamiliki utajiri mkubwa wa asilimia 80 ilhali sehemu kubwa ya watu wanamiliki sehemu ndogo ya utajiri.
Kwa jinsi hii, kama alivyobainisha Vilfredo Pareto (na kuthibitishwa na Lorenzo), ni ukweli kwamba watu wengi wanapogawana sehemu ndogo ya utajiri kuna kila sababu ya kila mmoja miongoni mwa wengi kupata kiduchu, jambo linalosababisha ongezeko la umaskini na watu maskini.
Pengo la kipato (tofauti) baina ya matajiri wachache na maskini wengi ni kubwa sana na hata haliwezi kupunguzwa kwa kuwa matajiri wanatumia nafasi yao katika kuzitumia fursa zote katika kuchuma zaidi na kulimbikiza mali kwa kutumia gharama za walalahoi.
Walalahoi wamekuwa wakinyonywa ilhali matajiri wakitumia nafasi yao katika kuhakikisha kuwa hakuna mtu na au kikundi cha watu wanaoweza kuzuia mfumo wa unyonyaji na uporaji na au kuhodhi utajiri.
Wafanyakazi walalahoi wamekuwa wakipuuzwa madai yao na au hata kuzibwa midomo kwa mbinyo wa sheria na kanuni zinazolinda maslahi ya matajiri badala ya kuwalinda walalahoi.
Vyama vya wafanyakazi vimekuwa vikikosa nguvu kwa utumizi wa rungu la sheria kandamizi hali inayochochea kukata tamaa kwa sehemu kubwa ya jamii ya wafanyakazi katika kudai maslahi bora na yanayokidhi hali halisi ya maisha ya siasa-uchumi kwa kuzingatia mahitaji ya muda.
Kwa jinsi hii, wafanyakazi na wakulima walalahoi wamekalia kuti kavu juu ya mnazi mrefu uliyoparama! Maisha ya kiuchumi ya walalahoi yamewekwa rehani na mfumo mbovu wa siasa-uchumi ambao kwa jinsi yake umepoteza uhalali wa kuwatumikia watu kwa uwiano wa uhuru, haki na usawa.
Hakuna mtu anayetamani kusimamia ukombozi wa walalahoi kwa dhati ya nafsi yake miongoni mwa waliyepewa nafasi ya kuongoza mapambano ya kujenga jamii ya watu waliyo sawa na huru. Kila mmoja na lwake, ubinafsi kayaya umekuwa ndio mwenendo wa kuongoza watu.
Walalahoi wameachwa wahangaike huku na huko katika kutafuta riziki kidogo inayopatikana kwa shida na taabu nyingi ilhali viongozi wenye mamlaka na dhamana ya kuwatumikia wananchi hao wakifanya starehe na kuponda raha na anasa kwa matumizi yasiyoelezeka na hata wengine kudiriki kusema kwamba, "hawajui sababu za umaskini wa wananchi wa Tanzania."
Sikutegemea kama Tanzania, kwa miaka hamsini ya uhuru, ingefikia upeo huu wa uongozi kushindwa kujua sababu za watu wake kuwa maskini! Je, hii ni laana? Au, kwa mtazamo wa kifalsafa tuseme, "aliyeshiba" hamjui mwenye njaa!
Sidhani kama ni muafaka na ni sahihi kwa uongozi makini na unaozingatia uhuru, haki na uadilifu kutumia fursa zote za kuwaondolea shida na taabu watu wake kwa kebehi! Kama walalahoi wa Tanzania wamefikia hatua ya kufanyiwa kebehi ya hali ya juu kwa jinsi hii, sidhani kama kuna dhamira ya dhati na makusudi ya kudadavua tatizo la umaskini linalowakabili wananchi wengi wa Tanzania.
Kwa kuwa hakuna asiyetambua matatizo mengi yanayowakabili wananchi wa Tanzania – mijini na vijijini na kwa kuwa hata viongozi kwa jinsi wanavyoongoza wamesahau wajibu wao wa kuleta hali bora kwa wananchi waliyo wengi maskini.
Ni haki ya kila mwananchi kutumia fursa hiyo katika kuleta mapinduzi ya fikra na kuondokana na unyonge unaotokana na umaskini wa kipato.
Ni wakati wa kutambua wajibu wa kutumia rasilimali pekee ya mnyonge – umoja! Kwa pamoja, walalahoi wanaweza kutumia fursa zilizopo kwa gharama nafuu katika kuleta mapinduzi ya fikra, kama alivyowahi kusema nguli wa reggae, Bob Marley, "jiondoeni (wenyewe) kutoka kwenye utumwa wa kiakili; hakuna (awezaye) kuwaondoa isipokuwa (nyinyi) wenyewe!"
Walalahoi wengi wana akili angavu na wana utambuzi makini na hakuna awezaye kuwazuia wasilete mapinduzi ya fikra na kuchukua uongozi wa kuleta hali bora na mizania ya uhuru, haki na usawa kwenye siasa-uchumi.
Ni wajibu kwa viongozi wa kijamii kuchukua nafasi zao katika kuonyesha njia ili kwa njia hiyo walalahoi wapate msaada katika maisha yao kwa mujibu wa mgawanyo wa haki na wa usawa wa fursa kwa matumizi makini na endelevu ya rasilimali zilizopo.
Kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anatumia nafasi yake kwa manufaa ya taifa la Tanzania. Kila mmoja akatae ubinafsi kayaya na apige vita ufisadi wa kimfumo na wa ndani ya mfumo katika kuhakikisha jamii inaongozwa kwa misingi ya uhuru, haki na usawa bila ya ubaguzi na upendeleo wa jinsi yoyote.
Tanzania inaweza kufikia malengo ya maendeleo ya karne (Millenium Development Goals – MDGs) kama kila mmoja atatamani kumsaidia mwenzake kwa uhuru, haki na usawa. Mapenzi ya utaifa (uzalendo) na undugu baina ya wananchi ndiyo njia pekee ya kuifanya Tanzania kupata mizania ya haki juu ya siasa-uchumi.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: +255 713 593347
Barua pepe:
maligwa1968@yahoo.com