2007-01-30 11:00:10
Na Hellen Mwango na Rosemary Mirondo
Watu wanaodaiwa kuwa ni familia ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri anayekabiliwa na kesi ya mauaji, jana waliendelea kuwaletea fujo waandishi wa habari wanaofuatilia mwenendo wa kesi hiyo.
Watu hao wengi wao wakiwa ni wanawake, walifanya hivyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya pili kwa watu hao kuwafanyia vurugu waandishi wa habari mahakamani hapo wakiwa kazini.
Katika tukio la kwanza, mwanamke mmoja alidiriki kuziba kwa kutumia kitambaa cheusi kamera ya mpiga picha wa ITV ili asichukue picha za mshtakiwa Ditopile anayedaiwa kumuua dereva wa daladala.
Na katika tukio la jana, watu kama hao, pia waliwatolea lugha chafu ya matusi huku wakitandaza pande za khanga kuwazuia waandishi wa habari wasipige picha za matukio mbalimbali hasa la mshtakiwa Ditopile mahakamani hapo.
Hali kadhalika, watu hao wakiongozwa na mwanamke mmoja alisikika akijitaja kwa jina la Jamila Jumbe na kujinadi kuwa ni `dada` wa damu wa mshtakiwa na kwamba siyo wa manati wala wa kuunga unga.
Aidha, mbali ya kutoa kashfa na kejeli kwa waandishi wa habari, pia walidai kwamba, wamechoshwa na tabia ya waandishi hao kuendelea kumsakama ndugu yao Ditopile kila anapofikishwa mahakamani hapo kwa kumpiga picha huku wakitambua kwamba anasumbuliwa na kisukari na shinikizo la damu.
Na hata baada ya Ditopile kuingizwa katika chumba cha Mahakama, mwanamke huyo aliyedai kuwa ni dada yake wa damu wa mshtakiwa akiwa pamoja na mwanaume mmoja, waliziba kwa upande wa khanga mpiga picha ili asipige picha yoyote inayohusiana na tukio hilo hadi alipoingia Hakimu Mkuu Mkazi, Bw. Michael Luguru anayesikiliza kesi hiyo.
Baada ya Mahakama kuanza shughuli zake, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Bw. Charles Kenyella, akisaidiana na Mrakibu Msaidizi Bi. Naima Mwanga na Inspekta Msaidizi Bw. Boniface Edwin, alidai kuwa, upelelezi kwa upande wa polisi umekamilika na jalada limewasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kwa hatua.
ACP Kenyella aliongeza kuwa, kwa sasa upande wa mashtaka wanasubiri maelekezo zaidi na ushauri kutoka kwa DPP.
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Cuthbert Tenga na Samwel Mapande, ulidai kuwa, umesikia hatua hiyo ya upepelezi wa kesi hiyo kukamilika. Waliiomba mahakama wasipumzike ili kesi hiyo ifikie tamati.
ACP Kenyella alidai kuwa, anaamini kwamba, DPP atalishughulikia shauri hilo.
Katika kesi ya msingi, Ditopile anadaiwa kuwa, Novemba 4, mwaka jana, saa 1:00 usiku, kati ya Barabara ya Bagamoyo na Kawe, jijini Dar es Salaam, alimuua dereva wa daladala, Hassan Mbonde kwa kumpiga risasi.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 12, mwaka huu itakapotajwa tena na mshtakiwa alirudishwa rumande.