Serikali yatoa tamko sakata la Ditopile
Nduguze kuchukuliwa hatua za kisheria
Nasra Abdallah, Safina Tibanyendela na Amana Nyembo
HATIMAYE serikali imetoa tamko kuhusu vurugu zilizofanywa katikati ya wiki iliyopita na ndugu na jamaa wa Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, ndani na nje ya jengo la Mahakama Kuu, jijini Dar es Salaam. Mbali ya hilo, serikali pia imeeleza kuguswa na matukio ya jana na juzi, ya mahabusu walio katika magereza mbalimbali nchini, kugoma kushuka katika makarandinga wakipinga kuchelewa kusikilizwa kwa kesi zao.
Tamko hilo la serikali lilitolewa na Waziri wa Usalama wa Raia, Harith Bakari Mwapachu, ambaye aliwataka ndugu na jamaa hao wa Ditopile-Mzuzuri na watu wengine walioshiriki katika vurugu zilizotokea Mahakama Kuu siku Ditopile alipoachiwa kwa dhamana, kukaa chonjo. Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Mwapachu alisema wizara yake haiwezi kukaa kimya na kuliacha suala hilo, ambalo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria, lipite hivihivi.
Alisema ofisi yake bado inalifuatilia suala hilo kwa karibu na hatua zaidi zinatarajiwa kuchukuliwa pale Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, atakaporejea kutoka Afrika Kusini. Kuhusu waandishi waliopigwa na kuharibiwa vifaa vyao vya kazi, Mwapachu alisema uongozi wa polisi unasubiri taarifa ya mahakama kabla kuchukua hatua kwa wote watakaobainika kukiuka sheria, kanuni na taratibu. Alisema hivi sasa, uchunguzi unafanyika kwa nia ya kubaini kilichotokea na kuwatambua wote waliohusika ili sheria ichukue mkondo wake.
Mwapachu ametoa kauli hiyo wakati mgomo ulioanzishwa na mahabusu wanaosikiliza kesi zao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutokana na mwenendo wa kesi ya Ditopile, ukisambaa mikoani. Kuhusu mgomo huo, alisema tayari ameshaliagiza Jeshi la Polisi na taasisi nyingine kwenda katika mahabusu zote zilizoathirika na kuzungumza na mahabusu waliogoma.
Waziri Mwapachu alisema amewataka polisi watakaoifanya kazi hiyo, kuhakikisha wanapitia kila jalada la kesi ya mahabusu mwenye matatizo kwa lengo la kubainisha imechukua muda gani. Mwapachu alitaka kupewa taarifa kuhusu agizo hilo mwishoni mwa mwezi huu. Aidha, alisema katika taarifa hiyo, polisi hao wanapaswa kuongeza maelezo kuhusu mahusiano kati ya mahabusu, wafungwa na askari magereza.
"Nimeagiza ripoti hii iandaliwe kwa ushirikiano kati ya wanasheria, majaji, mahakama na polisi," alisema Mwapachu ambaye ameongeza kuwa, lengo litakuwa ni kuhakikisha kesi ndogo ndogo zote zinashughulikiwa haraka kwa nia ya kupunguza msongamano katika mahabusu na magereza. Kuhusu Ditopile kupata dhamana haraka wakati mahabusu wengine wanasota kwa miaka mingi, Mwapachu alisema hiyo inatokana na uwezo wa Ditopile kuweka mawakili wazuri kumtetea.
"Watu wenye uwezo wa kufuatilia mambo yao, kesi zao huenda haraka kutokana na kuweka mawakili wazuri kitaaluma, ambao wana uwezo mkubwa wa kufuatilia kesi hizo," alisema na kukiri kutokuwepo kwa usawa kati ya watu wenye uwezo na wasio na uwezo, akibainisha kuwa hilo ni jambo la kawaida popote duniani.
Alisema suala la Ditopile kutoka haraka si la serikali wala mahakama, kwani ametolewa kwa mujibu wa sheria zilizopo. Wakati huo huo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Sivangilwa Mwangezi, amedai kuwa mgomo wa mahabusu hao hauwezi kuathiri utendaji kazi wa mahakama hiyo.
Alidai kuwa, kazi kubwa ya mahakama ni kusikiliza mashauri yanayoletwa mbele yake iwapo mahabusu watakuwepo mahakamani. Kwa kuwa mahabusu hao wamegoma, alisema kuwa mahakama haitakuwa na cha kufanya mpaka pale watakapoamua kurejea ili kesi zao ziendelee. "Kama wao hawashuki, sisi tunaendelea kusikiliza kesi za washitakiwa ambao wako nje kwa dhamana… mimi si kazi yangu kufuatilia mgomo kwa sababu hiyo ni kazi ya ofisa wa makosa ya jinai kanda ya Dar es Salaam na kama wataamua waende gerezani wakawaombe ili waje kuendelea kusikiliza kesi zao," alisema.
Mgomo huo, ulioanzishwa juzi na mahabusu katika Mahakama ya Kisutu, jana ulisambaa katika mahakama zingine Dar es Salaam na Arusha. Jana, mgomo huo ulianzia katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala majira ya saa 3:10 asubuhi baada ya gari la kubeba mahabusu lilipowasili kutoka gereza la Keko. Mahabusu waligoma kuteremka wakidai haki itendeke kupitia nyimbo walizokuwa wanaimba na vikaratasi walivyoviandika na kuvipenyeza kwa waandishi wa habari.
Katika vikaratasi hivyo, mahabusu hao walitaka viongozi kadhaa wa juu wa Jeshi la Polisi kujiuzulu wakiwatuhumu kwa uzembe, upendeleo na rushwa, na kwamba utendaji wao umedhihirisha kuwa hawaiwezi kasi mpya. Karandinga hilo lililokuwa na namba za usajili STH 3058 liliondoka kuelekea Mahakama ya Kisutu na liliwasili saa 3:30, lakini mahabusu hao walishikilia msimamo wao na kumtaka Waziri wa Sheria na Katiba, Mary Nagu, kutoa tamko.
"Hatushuki humu ndani labda mtuue humuhumu, waendesha mashtaka wanachelewesha kesi zetu, ndio chanzo kikubwa cha sisi kuendelea kujazana huku magerezani wakati kuna magonjwa mengi… mahakimu wanaendesha kesi kwa kuwasikiliza waendesha mashitaka tu, sisi hatusikilizwi," walidai. Alimtaka Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) naye awaeleze upelelezi wa kesi unachukua muda gani wakati wengine wamekaa mahabusu zaidi ya miaka kumi.
Ilipofika saa 3:47 asubuhi mahabusu walirudishwa Keko na karandinga la pili kutoka Gereza la Segerea lenye namba za usajili STJ 903 liliwasili Mahakama ya Kisutu saa 4:23 asubuhi likiwa limeongozana na gari moja la polisi lenye namba za usajili T 220 AMV na FFU lenye namba PT 0892. Mahabusu hao wapatao 150, nao walishikilia msimamo wa kutoshuka katika gari hilo wakiomba upelelezi wa kesi zao uharakishwe.
Baada ya mahabusu hao kugoma kuteremka, gari hilo liliondoka mahakamani hapo kuwarudisha Segerea majira ya saa 4:36 asubuhi huku wakiimba wimbo maarufu wa "Parapanda italia." Naye mkuu wa waendesha mashtaka mahakamani hapo, Germanus Mhume, alisema hawawezi kutumia nguvu kuwalazimisha mahabusu hao wateremke kwenye gari. Alisema wataendelea kusubiri mpaka siku watakayoamua kushuka kusikiliza kesi zao.
Kutoka Arusha, Ramadhani Siwayombe na David Frank wanaripoti kuwa, sakata la mahabusu kugoma baada ya kuachiwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, limechukua sura mpya mara baada ya mahabusu jijini Arusha jana nao kuamua kugoma kushuka katika karandinga kwa madai ya upelelezi wa kesi zao kucheleweshwa.
Sakata hilo lilianza majira ya saa nne asubuhi, baada ya mahabusu hao kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na kutakiwa kushuka baada ya askari kufungua mlango, lakini wao wakaanza kuimba nyimbo mbalimbali za kuashiria mgomo.
Mahabusu hao walianza kupiga kelele wakidai waambiwe Ditopile katoa nini ili nao watoe, ili kesi zao zisikilizwe haraka. Walisema bila ya kupatiwa maelezo yanayoridhisha, hawatashuka katika gari hilo lenye namba za usajili STG 5699 aina ya Scania. Baada ya kufunguliwa kwa mlango wa karandinga hilo, askari walishuhudia mahabusu mmoja tu mwanamke, akishuka katika karandinga hilo huku mahabusu wote waliobaki wakigoma na kusababisha shughuli mahakamani hapo kusimama.
Hatua hiyo ya mahabusu kugoma kushuka na kuanza kuimba nyimbo na kupiga kelele, ilizua mtafaruku mwingine, kwani mahakama hiyo ipo jirani na Ikulu ndogo ambayo Rais Jakaya Kikwete, ambaye yupo mjini hapa kwa ziara ya kikazi, amefikia.
Kelele hizo ziliwalazimisha askari waliokuwepo katika Ikulu hiyo, kwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kuimarisha usalama. Hata hivyo, kuwasili kwa askari hao waliokuwa katika magari manne aina ya Land Rover Defender na pikipiki, kuliamsha ari ya mahabusu hao, ambao waliongeza kelele za kutaka waambiwe kiini cha kesi zao kuchelewa kusikilizwa.
"Tunaomba tuelezwe sababu ya kesi zetu kuchelewa kusikilizwa kwa madai ya uchunguzi kutokamilika, huku kesi za anayetajwa kuwa mwana mtandao kusikilizwa kwa haraka na kuachiwa kwa dhamana huku sisi tukiendelea kuteseka jela," walisema.
Kufuatia kelele hizo kuzidi, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) mkoani hapa, Kamanda Shilogile, alifika mahakamani hapo na kuwabembeleza mahabusu hao kushuka, lakini juhudi zake ziligonga mwamba. Baada ya kujadiliana na wahusika wengine kwa muda, aliamuru mahabusu hao warejeshwe magereza Lisongo.
Akizungumza na gazeti hili baada ya mgomo huo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Basilio Matei, alisema umetokana na mgomo uliotokea jijini Dar es Salaam na madai yao hayana tofauti na yale yaliyotolewa na mahabusu wa Dar es Salaam. Kamanda Matei alisema, hivi sasa anafanya utaratibu wa kuwasiliana na mamlaka zinazohusika na masuala ya kesi hizo ili kuangalia hatua gani za kufanya kutatua tatizo hilo linalolalamikiwa na mahabusu hao.
Hii ni mara ya pili kutokea kwa tukio kama hilo mkoani Arusha. Miaka miwili iliyopita, mahabusu wa kesi kubwa za jinai na mauaji waligoma wakilalamika kucheweshwa kwa kesi zao.
Kutoka Mwanza, Mwandishi Wetu, anaripoti kuwa, baadhi ya mahabusu katika gereza kuu la Butimba, wametishia kugoma kuteremka kutoka katika karandinga siku ya kupelekwa mahakamani kutokana na madai ya kesi zao kucheleweshwa kutolewa maamuzi, huku za vigogo na wale wenye uwezo kutolewa maamuzi haraka haraka.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa, baadhi ya mahabusu wamekuwa wakisubiri kusikilizwa kwa kesi zao kwa zaidi ya miaka mitano sasa. Walidai kuwa wapo tayari kuungana na wenzao wa Dar es Salaam ambao jana na juzi waligoma kushuka katika magari wakitaka kuelezwa sababu zinazochelewesha kesi zao.