Tibaigana, Mssika wasimulia alivyojisalimisha polisi
Na Ester Bulaya
KONDAKTA Thomas Mwita aliyeshuhudia kifo cha dereva wake, amedai kuwa mshitakiwa Ditopile Mzuzuri (58), aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, alimzaba vibao na kumtishia kwa bastola dereva wa akiba kabla ya kumuua Hassan Mbonde.
Mbali na Mwita abiria aliyekuwa amekaa kiti cha mbele katika basi hilo, Masasi Luenge, alidai Ditopile alimtishia kumpiga risasi na kumtukana baada ya kumueleza aache kumuamuru dereva Mbonde ashuke chini.
Kauli hizo ni maelezo ya mashahidi wa upande wa mashitaka yaliyosomwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Michael Luguru aliyesikiliza maelezo ya mashahidi hao 24 yatakayotumika katika kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa Mahakama Kuu.
Akisoma maelezo ya Mwita, Mwendesha mashitaka Gilvanus Muhume alidai Luenge alizambwa vibao baada ya kushuka kuangalia jinsi gari la Ditopile lilivyoharibika baada ya ajali hiyo.
" Aliposhuka alikutana na mshitakiwa (Ditopile) aliyemuuliza unafanya nini, ambapo Luenge alimjibu 'samahani mzee naangalia tulipo gonga' ghafla Ditopile alimzaba vibao na kumuamuru aondoke huku akimuonyeshea bastola kichwani," alidai Mwita katika maelezo yake.
Mwita ambaye ni kondakta wa daladala hilo lenye namba za usajili T 816 AGT, alidai siku ya tukio walikuwa wakielekea Tegeta saa moja usiku njia panda ya Kawe, wakati wakiwa kwenye foleni lilikuja gari aina ya Prado ambalo lilienda 'kuchomekea' ghafla mbele ya gari yao, ambapo kwa bahati mbaya gari lao liligonga tairi ya akiba iliyokuwa nyuma ya gari.
Alidai baada ya kuona mwenzake amenyooshewa bastola, aliondoka na kuingia ndani ya gari, huku Ditopile akizunguka dirisha alilokuwa amekaa dereva na kumlazimisha ashuke.
Mwita alidai Mbonde alimjibu: "Samahani mzee siwezi kushuka kwa kuwa gari lipo kwenye kilima na breki siyo nzuri hivyo nitaua abiria."
Kwa mujibu ya maelezo ya Mwita, baada ya marehemu kujibu hivyo, Ditopile alimwambia kuwa anajali abiria kuliko gari lake na kumlazimisha asishuke ambapo alipandisha vioo na 'kuloki' mlango wake.
Ditopile baada ya kuona hivyo 'alikoki' bastola na kumfyatulia dereva Mbonde risasi mbili za kichwa.
Alidai baada ya kumpiga risasi, abiria walianza kulia huku wakipiga kelele kuwa ameua ndipo mshitakiwa alipoingia na kumgusa dereva huyo.
Mwita alidai abiria walianza kumzonga huku yeye akimshika kwa nguvu asitoroke kwa ajili ya kumpeleka polisi.
Alidai wakati wakimzuia, alitokea dereva wa Ditopile ambaye naye alichomoa bastola na kuwanyooshea huku akiwakataza kumshika bosi wake na hivyo kufanikiwa kuondoka naye katika eneo la tukio.
Shahidi Masasi Luenge ambaye alikuwa abiria katika daladala hilo, alidai dereva wa Ditopile ndiye 'aliyechomekea' na kusababisha ajali hiyo.
Luenga ambaye alikuwa amekaa kiti cha mbele alidai baada ya marehemu kupigwa risasi alimuangukia na kufa papo hapo.
Alidai kabla ya kushambuliwa, marehemu alimuomba msamaha na kueleza sababu za kutoshuka.
Hata hivyo, alidai Ditopile alimtukana na kumuelekezea bastola.
Kwa upande wake, dereva wa akiba katika daladala hiyo, Edward Girvas ambaye siku hiyo alikuwa kama kondakta, alidai alitishiwa kupigwa risasi ya kichwa na Ditopile, baada ya kushuka na kumuomba msamaha wakati marehemu alipogonga gari lao.
Alidai mshitakiwa kabla ya kumonyeshea bastola alimpiga vibao na kumtaka aondoke haraka.
Shahidi mwingine aliyetoa maelezo yake mahakamani hapo ni daktari Mgaya wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, na kuthibitisha kuwa marehemu aliuawa kwa kupigwa risasi mbili.
Alidai risasi hizo zilipitia upande wa kulia na kutokea kushoto na kwamba kipande cha risasi kilibaki katika kichwa cha marehemu.
Kamishna msaidizi wa polisi, Abdallah Mssika, katika maelezo yake alidai Ditopile alimueleza kwamba hakudhamiria kumuua dereva Mbonde, lakini bastola aliyokuwa akimtishia ilifyatuka na kusababisha mauaji hayo.
Akisoma maelezo ya shahidi huyo (Mssika), aliyemhoji Ditopile, Muhume alidai katika maelezo hayo, mshitakiwa alimueleza kuwa
hakuwa na nia ya kufyatua risasi bali alishtukia risasi zimetoka zenyewe baada kugonga dirisha.
Kulingana na Ditopile, hali hiyo ilisababishwa na bastola hiyo ambayo ni 'Automatic'.
Alidai kitendo cha yeye kutoa bastola hiyo, kilitokana na marehemu (dereva) kumsonya na kugoma kushuka, baada ya kumgonga huku kondakta wa akiba akimtamkia maneno kwamba 'mzee hiyo ndiyo imetoka' matamshi aliyoyaona ni dharau kwake.
Mssika aliendelea kudai katika maelezo hayo kuwa Ditopile, baada ya kugundua risasi imefyatuka, aliamua kutoa risasi zote katika bastola yake ili isilete madhara zaidi.
Alidai baada ya kuhakikisha bastola yake iko salama, aliingia ndani ya basi hilo kuangalia jinsi dereva alivyoumia ili aweze kumsaidia ikiwa ni pamoja na kumpeleka hospitali.
Mssika alidai katika maelezo yake kwamba, Ditopile hakupata ushirikiano kutoka kwa abiria na badala yake walianza kumzonga na kumuambia 'umeua mwenyewe na umbebe kumpeleka hospitali' huku wengine wakimpiga.
Alidai katika kujiokoa kondakta wa gari hilo, alichukua chuma na kutaka kumpiga kichwani, lakini mshitakiwa alifanikiwa kukinga kwa kutumia mkono wake.
Kutokana na hilo, mshitakiwa alilazimika kukimbia huku akipiga kelele kuomba msadaa kutoka kwa dereva wake.
Mssika alidai kabla ya kuchukua maelezo ya Ditopile, mshitakiwa alimpigia simu kwa lengo la kutaka kujisalimisha na kumueleza juu ya tukio hilo.
Kamanda Mssika alidai baada ya kujisalimisha alichukua maelezo yake mbele ya wakili wake Ringo Tenga.
Akisoma maelezo ya Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, Mwendesha mashitaka Naima Mwanga alidai Tibaigana alieleza kushangazwa kumuona mshitakiwa akifika nyumbani kwake usiku wa manane akiwa na Mssika.
Naima alidai Kamanda Tibaigana alimkaribisha Ditopile kwa kumueleza 'Karibu Mheshimiwa na yeye alijibu kuwa mimi siyo mheshimiwa tena bali ni muuaji' na kuanza kumsimulia tukio hilo na kusisitiza kuwa hakuwa na nia ya kufanya hivyo.
Tibaigana alidai kuwa lalamiko kubwa la Ditopile ni kitendo cha dereva (marehemu) kumtukana na kukaidi kushuka ili waweze kufikia makubaliano.
Mbali na maelezo ya mashahidi hao, pia upande wa mashitaka utawasilisha vielelezo vitano ikiwemo taarifa ya daktari, maelezo ya ungamo la mshitakiwa, taarifa ya uchunguzi wa ripoti ya mlio wa risasi, ramani ya eneo la tukio na fomu ya gwaride la utambulisho.
Hata hivyo, upande wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na wakili Nimrod Mkono, uliomba dhamana kwa mteja wao, na kumueleza hakimu kuwa ana uwezo wa kutoa dhamana ingawa hana mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hata hivyo Hakimu Lugulu alikataa kusikiliza ombi hilo na kuwataka kuliwasilisha Mahakama Kuu.
Ditopile ambaye jana alikuwa akiendeleza mtindo wake wa kuingia mahakamani huku akiwa amevaa 'pama' kuficha uso jana alisomewa shitaka jipya la kuuawa bila kukusudia.
Katika shitaka hilo, anadaiwa kuwa Novemba 4, mwaka jana, njia Panda ya Kawe na Bagamoyo alimuua bila kukusudia Hassan Mbonde.
Awali, alishitakiwa kwa kosa la mauaji kabla ya kubadilishiwa shitaka hilo na Mkurugenzi wa Mashitaka mwishoni mwa Januari.