http://www.mwananchi.co.tz/mwananchisite/Mwananchi/Habari/Habari0.asp
Mahakama yamwachia Ditopile nduguze wazusha vurugu
Na Tausi Ally
WAKATI Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri ameachiwa kwa dhamana, ndugu zake wamefanya fujo na kuwapiga waandishi wa habari katika Mahakama Kuu Dar es Salaam jana.
Dhamana hiyo ilitolewa saa 7:45 mchana na Jaji wa Mahakama Kuu, Augustino Mwarija, baada ya upande wa utetezi kuwasilisha ombi la dhamana mahakamani.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Mwarija, alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, ameona hakuna kipingamizi cha kutoa dhamana hiyo kwa kuwa kosa aliloshitakiwa nalo mtuhumiwa la kuua bila kukusudia, linastahili dhamana.
Awali, mawakili wanaomtetea Ditopile wakiongozwa na Profesa Jwani Mwakyusa, waliiomba mahakama imuachie huru kwa dhamana mteja wao kwa maelezo kuwa hawezi kuruka dhamana na kwamba anaweza kujidhamini mwenyewe na akiwa huru atapata muda wa kutosha wa kujiandaa kwa utetezi.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Vicent Tango, ulieleza kuwa hauna pingamizi la dhamana kwa kuwa kosa hilo linadhaminika.
Jaji Mwarija alikataa hoja ya mawakili wa utetezi kuwa mtuhumiwa anaweza kujidhamini mwenyewe na badala yake akautaka upande huo kuandaa wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya Sh20 milioni kila mmoja, akiwamo Ditopile mwenyewe ambaye naye alitakiwa kusaini bondi ya kiasi hicho cha fedha.
Mbali na masharti hayo, Jaji Mwarija pia alimtaka Ditopile kuwasilisha hati za kusafiria kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na asitoke nje ya Jiji la Dar es Salaam bila kibali cha Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Ditopile alifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 2.54 asubuhi akiwa amevalia suruali nyeusi na shati la mistari ya kijivu na mieusi na kofia yake aina ya pama yenye rangi nyeusi iliyofunika uso wake pamoja na miwani.
Lakini katika hali isiyo ya kawaida, mara baada ya kufika mahakamani hapo, kundi la skari polisi zaidi ya 10 waliokuwa wakimlinda, walimuongoza kuingia ndani ya mahakama kupitia mlango unaotumiwa na majaji, kitendo ambacho si cha kawaida kwa watuhumiwa.
Hali hiyo iliwashangaza watu wengi akiwemo Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Prophir Lyimo, aliyehoji kitendo hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari, Lyimo alisema kitendo hicho cha kumpitisha mtuhumiwa katika mlango wa majaji kimeikera mahakama na hawakufarahishwa nacho.
"Kitendo hiki si cha kawaida na hakijawahi kutokea, askari hao hawajaruhusiwa kumpitisha mtuhumiwa huyo huko na wala hawajawahi kuruhusiwa kufanya hivyo," alisema Lyimo kwa masikitiko.
Alisema kutokana na kitendo hicho, amewasiliana na Kamanda wa Polisi kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna, Alfred Tibaigana, ili afuatilie suala hilo na kwamba ameahidi kufanya uchunguzi.
Hata mlinzi aliyekuwepo katika mlango wa majaji, alisikika akilalamika kwamba alipigwa kikumbo na askari hao waliokuwa wakimpitisha Ditopile, hivyo ilimbidi akae pembeni, na kwamba anahofia kupoteza kazi kutokana na kitendo kwani tayari alikuwa ametakiwa kuandika barua ya kujieleza.
Kama hiyo haitoshi, wakati mtuhumiwa huyo akiingizwa katika mahakama ya wazi namba moja, askari kwa kushirikiana na ndugu wa mtuhumiwa walianza kupambana na waandishi wa habari hasa wapiga picha, wakitaka kuwanyang'anya kamera ili wasiweze kumpiga mpicha Ditopile.
Ndani ya mahakama hiyo ya wazi, kulikuwa kumefurika watuambao kati yao walikuwamo familia ya Ditopile, makarani wa mahakama ambao waliacha shughuli zao, waandishi wa habari na wananchi wa kawaida waliotaka kujua hatma ya ombi la dhamana la mtuhumiwa huyo.
Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Jaji Mwarija kutoa dhamana kwani wakati mtuhumiwa akitoka mahakamani kurudi nyumbani kwake majira ya saa 8.01 mchana, ndugu zake walianza vituko vya kuwafanyia vurugu waandishi wa habari ili wasiweze kuona namna mtuhumiwa huyo anavyoondoka katika eneo la mahakama.
Watu hao walianza kushika kamera ili picha zisipigwe, kuwarushia ngumi, mateke na kutoa lugha chafu kwa waandishi wa habari, huku wengine wakiwa wamemzunguka mtuhumiwa na kumfunika kwa kanga kiasi cha kufanya asionekane kabisa kabla ya kuingia kwenye gari ndogo aina ya Toyota balloon namba T 723 AFD na kuondoka naye.
Katika sakata hilo lililodumu kwa zaidi ya dakika 10, mwandishi mmoja alijeruhiwa kwa kuchanika mdomoni huku wengine wakiumizwa sehemu mbalimbali za mwili.
Katika hali ya kushangaza, pamoja na kuwapo kwa askari wengi katika eneo hilo, hakuna askari hata mmoja aliyechukuwa hatua ya kuzuia vitendo hivyo vya ndugu zake Ditopile na badala yake walisimama pembeni na kuangalia kama sinema.
Hii ni mara ya pili kwa watu hao kufanya vurugu mahakamani, kwani hivi karibuni wakati kesi hiyo ikiwa bado katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, walifanya vurugu kubwa ambayo ililaaniwa na waendesha mashitaka.
Mara ya mwisho kesi hiyo ilipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, upande wa mashitaka ulitoa maelezo ya mashahidi 23 wa upande huo.
Katika maelezo ya mashahidi hao ambao watasimama dhidi ya Ditopile wakati kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, walieleza namna tukio zima la mauaji ya dereva wa daladala, Hassan Mbonde lilivyotokea.
Kwa upande wake, Ditopile kupitia maelezo yake yalivyoandikwa na ASP Sabasi na kusomwa mahakani hapo na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Germanus Mhume mbele ya Hakimu Michael Luguru, naye alieleza mazingira ya tukio hilo lilivyotokea kabla ya kujisalimisha polisi.
Ditopile alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 6 mwaka jana akikabiliwa na tuhuma za kumuua dereva wa daladala Hassan Mbonde.
Anadaiwa kuwa Novemba 4, mwaka jana, majira ya saa 1.00 usiku, katika eneo la njia panda ya Bagamoyo na Kawe wilayani Kinondoni Ditopile alimuua bila ya kukusudia dereva huyo wa daladala.