Makala hii nimeiona kwenye mtandao mmojawapo ya kublogu mwandishi anasema imetoka gazeti la jana la mtanzania, is this PR machinery at work au ni honest expression of thought?
NDUGU Kapteni Ukiwaona Ditopile Ramadhan Mwinshehe Wa Mzuzuri. Jina lake tu lilitosha kumpandisha juu kisiasa. Nililisikia kwa mara ya kwanza kupitia redio wakati ningali shule ya msingi miaka ile ya 80.
Ilikuwa ni kwenye moja ya chaguzi za ndani za CCM. Nayakumbuka majina mawili tu katika uchaguzi ule uliotangazwa moja kwa moja redioni. Ni majina ya Ndugu Ukiwaona Ditopile na Ndugu Idd Simba. Maana, jina la Ukiwaona Ditopile likikuwa refu mno na lenye kuvuta sikio. Wajumbe wa Mkutano ule Mkuu wa CCM nao walionekana kuvutwa na jina lake hata kabla hajatoa maelezo yake binafsi. Na mara ile jina la Ndugu Idd Simba lilipotamkwa, zililipuka kelele za Simba! Simba! Simba! Kana kwamba ilikuwa ni kwenye mechi ya Simba Uwanja Wa Taifa.
Nakumbuka yalisomwa maelezo binafsi ya Ukiwaona Ditopile kama mtu aliyeanzia kwenye utangazaji redioni na baadae kujiingiza kwenye siasa. Bila shaka, Ditopile angependa apande na kubaki juu kisiasa. Na hata kama kushuka kisiasa, basi asingependa iwe kama ilivyomtokea. Ditopile hakushuka, ameanguka na labda ameporomoka kisiasa.
Anayeshuka kisiasa walau anajua akanyage wapi katika ngazi za kuteremkia. Ditopile, kwa kutumia lugha na mazingira ya kwao Pwani, ni kama mtu aliyekwea kwa taabu sana mnazi mrefu. Amefika kileleni, amekwanyua nazi zake kwa mikono yake. Ameangusha chini, nazi moja baada ya nyingine.
Umewadia muda wa kuteremka mnazi akusanye nazi zake, ghafla amejikuta anaanguka chini ardhini. Sio tu ameanguka kwa kishindo kikubwa, bali pia amejeruhiwa vibaya mno. Katika yote mazuri aliyoyafanya kwa chama chake, serikali na kwa watu wa nchi hii, Ditopile ana hatari ya kukumbukwa daima kwa tukio analotuhumiwa sasa; kumwua kwa bastola dereva wa Daladala, Marehemu Hassan Mbonde.
Naam. Ditopile anatuhumiwa kwa mauaji. Nchi hii ina sheria zake. Tuna imani mkondo wa sheria utafuatwa ili haki itendeke. Hata hivyo, Ditopile anabaki kuwa ni binadamu kama wewe na mimi, hakukamilika. Na kama binadamu, inatupasa kujaribu kuingia kwenye hali yake na kujaribu kumwelewa yuko katika hali gani kwa sasa.
Huu si wakati wa kila mtu kutoa hukumu yake wakati kuna waliosomea kazi hiyo. Mathalan; kuandika magazetini vichwa vya habari kama vile; Ditopile kunyongwa! Ditopile amerogwa! na mengineyo yasiyo uthibitisho si kumtendea haki Ditopile. Kunazidi kuwaingizia simanzi zaidi ndugu zake wa karibu hata jamaa na marafiki zake. Hayo si maadili mema.
Tafsiri za tukio lile la mauaji zaweza kuwa nyingi. Lakini ukweli unabaki, kuwa Ukiwaona Ditopile anatuhumiwa kwa kumwua dereva wa daladala, ni mwananchi wa kawaida kabisa, mlalahoi. Siamini kama Ditopile alitaka mwisho wake wa kisiasa uwe ni namna ile. Lililomtokea ni dhahma na labda janga kubwa katika maisha yake binafsi, lakini pia kwa wote wenye kumhusu. Kama binadamu anastahili kupewa pole.
Hatujui kilichokuwa kikimzunguka Ditopile kwenye ubongo wake hadi kufikia kutenda jambo lile. Iko siku, katika utetezi wake, naye atapata fursa ya kuuelezea umma wa Watanzania juu ya usiku ule wa tukio uliopelekea mwisho wa huzuni na wenye majonzi kwa wengi, wenye kumhusu Ditopile na wale wenye kumhusu Marehemu Hassan Mbonde.
Ditopile, popote alipo, siyo tu ni mtu anayeshinikizwa na maradhi yake ya moyo na kisukari, bila shaka anashinikizwa na mzigo mzito wa fikara juu ya mustakabali wa maisha yake na ya wale wote wenye kumhusu. Ditopile anatuhumiwa kuyaondoa duniani maisha ya binadamu mwenzake ambaye hakuwa tu dereva wa daladala, bali pia alikuwa ni baba, kaka na mjomba wa wengi. Ana wenye kumpenda na kumtegemea.
Vivyo hivyo, kwa Ukiwaona Ditopile, naye hakuwa Mkuu Wa Mkoa na mwanasiasa tu. Ditopile ni Baba, babu, kaka na mjomba wa ndugu zake wengi. Nao pia wanampenda na kumtegemea.
Naamini, Ukiwaona Ditopile ni mhanga wa mfumo alioshiriki kuujenga. Mfumo uliopelekea kupitisha Sheria ya mauzo ya silaha; (Arms and Ammunition Act No.2, 1991) . Kwa kosa analotuhumiwa kulitenda Ditopile , anatusaidia kuamsha tena mjadala juu ya suala la uuzaji na umilikaji wa silaha hapa nchini. Tuna lazima ya kuufanya kuwa ni mjadala wa kitaifa.Suala si kuwapima akili wanaomilikishwa silaha kama inavyotakiwa na baadhi ya wabunge wetu. Wengi wa wanaomilikishwa silaha tunaamini huwa ni wenye akili nzuri kabisa kabla ya kushika silaha hizo. Lakini mara tu wakiwa na silaha kwenye makoti yao ndipo hapo baadhi yao akili huwaruka na kudhani kuwa wao ndio mwanzo na mwisho. Hawakawii kutishia watu; Nitakupiga risasi! hata kama amedhulumiwa chenji ya elfu moja tu!. Huo sasa ndio uwendewazimu ambao mtu huyo hakuwa nao kabla ya kumilikishwa silaha. Mjadala huu wa silaha unahitaji makala yake.
Turudi kwenye mada. Hakika Ukiwaona Ditopile si mwanasiasa wa msimu mmoja. Ditopile ni mwanasiasa wa misimu yote. Ana uzoefu wa miaka mingi katika mapambano ya kisiasa. Haikuwa ajabu kwamba Jakaya Kikwete alimtumia ipasavyo katika kinachoitwa Mtandao wake.
Mwanazuoni Profesa I. K. Bavu kwenye kitabu kiitwacho; Tanzania; Democracy In Transition alichoandika na wanazuozi wenzake anaulezea mchuano wa kisiasa kati ya wagombea wawili wa CCM katika uchaguzi wa mwaka 1985; Ni Martha Wejja aliyekuwa anatetea kiti chake na Ukiwaona Ditopile Mzuzuri aliyekuwa anajaribu kibarua kilimchomshinda mtoto mwenzake wa mjini; Mzee Kitwana Kondo kwenye uchaguzi wa mwaka 1980. Kitwana Kondo alishinda uchaguzi, lakini baadae Mahakama ilitengua matokeo na kumpa ushindi Wejja.
Ditopile ana uwezo wa kunusa kisiasa na hata kusoma mwelekeo wa upepo. Kwamba siku moja tu kabla ya kufikishwa mahakamani, Ditopile amemwandikia Rais barua ya kujiuzulu inaonyesha pia uelewa na uzoefu wake wa kisiasa. Yeyote mwenye kufikiri kwa undani anafahamu kuwa hata bila kuandikwa kwa barua ile, Ditopile alistahili kujiuzulu, kwa kuandika barua ya kujiuzulu kabla ya kushinikizwa kufanya hivyo , Ditopile amejiongezea pointi kwenye vita ya maoni. Wengi mitaani wanaamini kuwa Ditopile amechukua hatua ya kistaarabu kujiuzulu na hilo lina athari chanya kwake juu ya mwelekeo wa maoni ya wananchi.
Katika kitabu kile cha Profesa I. K. Bavu na wenzake, inaandikwa zaidi jinsi Ditopile alivyopambana na kupanda juu kisiasa. Kuwa, mara tu Ditopile alipohutubia kwenye mkutano wa kampeni ya ubunge pale Pugu Kajiungeni mwaka 1985 , alisikia wanafunzi wale wa Sekondari ya Pugu wakiimba. Kura Zetu! Tumpe Wejja! Ditopile alisikika akiwatamkia wapambe wake; That is a lost territory! Akiimanisha eneo hili tumeshalipoteza!
Kwenye mkutano wa kampeni Kariakoo, kwa Ditopile ilikuwa ni kama kuchezea uwanja wa nyumbani. Zilitumika mbinu ngumu za kisiasa kummmaliza Wejja. Mathalan, liliulizwa swali gumu kutoka kwa mpiga kura lenye kumtaka Wejja afafanue kwanini ametoa maelezo yenye kutofautiana juu ya mahala alipozaliwa kwa uchaguzi wa 1980 na ule wa 1985.
Na katika mkutano mwingine wa kampeni wa Ilala, Ditopile aliomba Bwana mmoja aliyejulikana kama Sharifu, aondolewe mkutanoni. Inaandikwa, kuwa Sharifu yule kwenye mkutano wa kampeni wa Mchikichini alisikika akitamka kuwa mkutano wa Ilala utakuwa wa mwisho kwa Ditopile kutokea hadharani. Wakati huo ilibaki mikutano sita ya hadhara kabla ya uchaguzi. Matokeo ya uchaguzi ule Ditopile alimshinda Martha Wejja na kuingia bungeni. ( I. K. Bavu, Tanzania : Democracy in Transition; Uk. 88-100)
Naam. Kwa ufupi tu, huyu ndiye Ukiwaona Ditopile Ramadhan Mwinshehe Wa Mzuzuri. Ni dhahiri, kwa sasa ana wakati mgumu katika maisha ya kawaida na maisha ya kisiasa. Lakini, kwa kuiangalia historia ya mtu huyu Ukiwaona Ditopile, nasita kuandika, kuwa ukurasa wa mwisho wa historia yake kisiasa umeshaandikwa