Mmuya aagiza kasi upatikanaji wa hati za ardhi sasa kupatikana ndani ya saa 48

Mmuya aagiza kasi upatikanaji wa hati za ardhi sasa kupatikana ndani ya saa 48

Wizara ya Ardhi

Govt Institution
Joined
May 14, 2024
Posts
306
Reaction score
165
ed04a8cc-cbbf-43aa-8979-131171b9e108.jpeg

★ Aelekeza kuanzishwa Kliniki ya Upimaji wa Mashamba
★ Awasisitiza wawekezaji kuendeleza maeneo yao kuepuka migogoro

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amesema kipaumbele cha Wizara kwa sasa ni kuongeza kasi ya utoaji wa hati za miliki za ardhi ili kuhakikisha wananchi wenye ardhi wanapata umiliki unaotambulika kisheria.

Mhe. Mmuya ameyasema hayo Oktoba 4, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, alipofanya ziara katika Shamba Na. 274, Mhukulu Lilahi, lenye ukubwa wa hekta 4,679.72 na linalomilikiwa na Kampuni ya Soagro Co. Ltd kwaajili ya shughuli za Ufugaji.

Amesema mwombaji ambaye taarifa na nyaraka zake hazina changamoto anapaswa kupata hati ya miliki ndani ya saa 48, akieleza kuwa matumizi ya mfumo wa e-Ardhi yamewezesha sehemu kubwa ya mchakato wa utoaji huduma kufanyika kidijitali.

Amesema mfumo huo umepunguza ulazima wa wananchi kufuatilia huduma kwa kufika ofisini katika kila hatua, kwa kuwa taratibu mbalimbali sasa zinaweza kufanyika kupitia mfumo.

Aidha, Mhe. Mmuya amewataka wananchi wanaodai kumiliki ardhi kuhakikisha wanapata hati za miliki, akisisitiza kuwa umiliki unaotambulika kisheria ni muhimu katika kulinda haki zao na kuepusha migogoro ya ardhi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mmuya ameelekeza kuanzishwa kwa Kliniki ya Upimaji wa Mashamba, itakayowezesha wananchi wenye mashamba na maeneo ya kilimo kupata huduma za upimaji na utambuzi wa mipaka kwa urahisi zaidi.

Amesema huduma hiyo itasaidia wananchi kufahamu mipaka ya maeneo yao na kuweka utaratibu unaotambulika katika matumizi na umiliki wa ardhi.

Kadhalika, Mhe. Mmuya amewataka wawekezaji nchini kuhakikisha wanaendeleza maeneo waliyopangiwa kwa mujibu wa masharti ya umiliki na matumizi ya ardhi, akisisitiza kuwa kutokuyatumia maeneo kwa madhumuni yaliyokusudiwa kunaweza kuchochea migogoro na changamoto nyingine za ardhi.
 
Back
Top Bottom