Suala la umhimu wa kuwa na Katiba mpya naliunga mkono. ila kwamba vyama vya upinzani wanajiandaa kuandika rasmi ya katiba mpya linanitia shaka kidogo. Hii ina maana vyama vya upinzani wanataka kuleta katiba mbadala ambayo kwa maoni yao ni nzuri kuliko iliyopo? Rasmi hiyo ya katiba ya vyama vya upinzani itakuwa katika sura gani? Itawakilisha maslahi ya kisiasa ya vyama vya upinzani au maslahi ya watu? Kama vyama vya upinzani wameshindwa kukaa pamoja na kuunda kambi ya upinzani bungeni wataweza kukaa pamoja na kuandika rasmu ya katiba itakayo kubalika kwa vyama vyote vya upinzani achilia mbali watu wote?
Kwa maoni yangu suala la mabadiliko ya katiba ni suala la watu wote. Linahitaji kuwashilikisha watu wote ili kuweza kupata maoni yao ya namna wanavyotaka katiba yetu iwe. Na kama tunataka mabadiliko ya Katiba yenye manufaa ya kudumu kwa Taifa letu tukubali kwamba suala hilo linahitaji muda wa kutosha sio la kuharakisha tu. Awali ya yote, wananchi ambao wengi wetu hatujui katiba ni nini na katiba yetu ya sasa hivi ikoje tunapaswa kupewa elimu ya kutosha ya katiba na uraia kabla hatujatakiwa kutoa maoni yetu juu ya mabadiliko ya katiba. Nionavyo mimi, ili wananchi tuwe katika nafasi nzuri kuyabainisha mapungifu ama mazuri yaliyomo katika katiba yetu tunapaswa kuwa na ufahamu kiasi kuhusiana na katiba. Vinginevyo, wengi kati yetu tunaweza kufata mkumbo bila kujua tunafanya mabadiliko gani na kwa sababu gani?
Ni ukweli usiopingwa kwa wale wenye ufahamu kwamba katiba yetu inayo mapungufu ya msingi na ya kawaida. Jambo la kujadili baada ya kuwapa mwanga wananchi juu ya katiba ni namna mapungufu katika katiba yetu yanavyoweza kuondolewa ima kwa kuifuta katiba iliyopo na kuandika katiba mpya au kuifanyia marekebisho ya msingi. Yoyote kati njia hizi inaweza kutumika ili mradi wananchi wanashirikishwa vya kutosha ili kuwafanya waione katiba kama zao lao na sio zao la viongozi wa kisiasa. Hilo litawafanya wananchi kuipa hadhi katiba inayofaa zaidi na kuyaheshimu na kuwa tayari kuyatetea yaliyomo katika katiba kwa kuwa yanatokana na wao.
Ni wazi kabisa kutokana na historia ya nchi kwamba ushirikishwaji wa wananchi katika uandikaji na urekebishaji wa katiba tuliyo nayo ulikuwa mdogo sana. Bila shaka hilo lilichangiwa pia na uchanga wetu wa demokrasia pamoja na mambo mengine.
Kutoshirikishwa kwa wananchi katika utungwaji wa katiba toka mwanzo kumeifanya nafasi ya wananchi katika maamuzi kuishia zaidi katika kuchagua viongozi. Marekebisho ya katiba bila kujali ni vifungu gani yamebaki kwa wabunge kwa taratibu mbalimbali kulingana na vifungu vya katiba vinavyotaka kubadilishwa. Kutokana na katiba iliyopo wabunge wana uwezo hata wa kuamua kujiongezea muda wao wa kuwa bungeni kutoka miaka mitano hata kumi au zaidi. Nani atawazuia kama kura zao zikitosha? Kwa maoni yangu, ilikuwa ni mhimu kuwa na vifungu katika katiba ambavyo haviwezi kurekebishwa bila kuwa na maoni ya wananchi. Vifungu kama vya ukomo wa bunge, ukomo wa ofisi ya raisi, haki za msingi za binaadamu, uhusiano wa mihimili mitatu ya dola, usekula wa dola yetu, mfumo wa vyama vingi, muungano, tume huru ya uchaguzi yawe ni baadhi ya mambo ambayo hayawezi kurekebishwa bila kuwepo referandum.
Mabadiliko katika masuala hayo yanaweza kufanyika kwa marekebisho au kutunga katiba mpya. Mhimu ni kwamba hayo mamabo yawemo katika katiba na mamlaka ya wananchi yawekwe wazi na kupewa nguvu za kisheria. Kwa sasa mamlaka ya wanachi katika maamuzi yanatamkwa tu kinadhalia katika ibara ya 8 ya katiba ambayo inaangukia katika Maelekezo ya Sera za Dola ambayo kitaalamu hayana nguvu za kisheria wala hayawezi kutekelezeka mahakamani.
Masuala mengine ya msingi ambayo yanapaswa kutizamwa vizuri ni haki ya kumiliki mali na kunufaika katika rasilimali za taifa. Hilo linahitaji maoni mengi kutoka kwa wananchi na ulinzi makini wa kikatiba.
Kuna hili suala la matokeo ya uchaguzi kupingwa mahakamani. Suala hilo lilizua mjadala mzito wakati tunaingia katika mfumo wa vyama vingi. Ni vizuri wananchi wakajulishwa mazuri na mabaya ya kuwepo kwa haki hiyo. Kwa maoni yangu binafsi suala la matokeo ya uchaguzi wa raisi kutopingwa mahakamani lingebaki hivyo hivyo ila nguvu zaidi zikapelekwa katika kuifanya tume ya uchaguzi na utaratibu wa kutangaza matokeo ya uraisi kuwa huru zaidi. Angalia kilichotokea Ivory Coast ambako haki hiyo imetamkwa katika katiba.
Mabadiliko ya katiba yasifanyike kwa njia ya zima moto. Tunaweza kuandika katiba mpya kwa kipindi kifupi na ikawa haina tofauti na hii tuliyonayo. Wananchi wanapaswa kuandaliwa, kuelimishwa na kushilikishwa vya kutosha katika mabadiliko ya katiba. Washiriki bila kuwa na upendeleo wa maslahi yao binafsi ya kivyama vya siasa wala ya kidini bali watizame maslahi ya kitaifa.
Yapo mengi ya kuchangia lakini ningependa kusikia kwa wengine pia.