Mikataba yagonganisha vichwa serikali, Bunge
- Wabunge kutaka kuijadili kabla ya kusainiwa
- Mwanasheria Mkuu asema hajapata maombi
- Spika asema serikali ipeleke muswada bungeni
Ramadhan Semtawa na Tausi Mbowe
KILIO cha wabunge kutaka kushirikishwa katika kuijadili bungeni mikataba yote kabla ya kusainiwa, kinaonekana kugonga ukuta kutokana na Bunge na serikali kutegeana.
Uwezekano wa mikataba hiyo kuonwa na kujadiliwa na wabunge kuiona na kuijadili kabla ya kutiwa saini na serikali unapaswa kuwapo baada ya kuwasilishwa muswada wa hoja hiyo bungeni na kutipishwa, kisha kutiwa saini Rais ili iwe sheria.
Wakati utaratibu ukiwa wazi kwa pande zote mbili, ombi hilo la wabunge kutaka kushirikishwa katika kuona na kuijadili mikataba, Spika wa Bunge Samuel Sitta, amesema serikali ndiyo yenye jukumu la kupeleka muswada huo bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na wabunge.
Akizungumza na waandishi wa gazeti hili mwishoni wiki iliyopita, Sita alisema kazi yakupeleka muswada ni ya serikali kupitia mawaziri wake na kwamba wao ni watekelezaji kwa kujadili baada ya kufikishwa bungeni.
"Hatuwezi kufanya kazi zote sisi, wabunge wanatakiwa kujadili kwa kuukosa, kutoa marekebisho na kuupitisha mswaada huo mpaka unapofikia hatua ya kuwa sheria, hivyo si kazi yetu kuandaa muswada huo na sisi wenyewe kuupitisha, kwani huwezi kuwa mgonjwa na kujitibu mwenyewe, " alisema Sitta.
Hata hivyo, Sitta alisema suala la wabunge kujadili mikataba ya nchi kabla haijatiwa saini ni jambo zuri na endapo litatekelezwa ni wazi kuwa wananchi wataweza kujua kilichopo katika mikataba hiyo badala ya hivi sasa ambapo ni siri.
Alitoa mfano wa nchi ya Thailand ambayo wabunge wake wana uwezo wa kujadili mikataba hiyo na kusema kuwa hali hiyo inaonyesha uwazi na uwajibikaji zaidi katika utawala.
Sitta alisema kuwashirikisha wabunge inaonyesha jinsi serikali inawashirikisha wananchi wake katika maamuzi yao wenyewe kwa kuwa wabunge hao wapo kwa niaba ya wananchi wao.
"Hii inajenga umoja, Bunge ni chombo chetu cha Kitaifa kinasimama badala ya wananchi, kuwashirikisha ni sawa na kushirikisha mwananchi mmoja mmoja katika maamuzi, "alisistiza Sitta.
Kwa mujibu wa Katiba ya nchi (Ibara ya 63 (d), Bunge ndilo lenye jukumu la kutunga sheria, chini ya utaratibu maalumu wa kanuni za chombo hicho (sehemu ya tisa).
Taratibu hizo zinahusu muswada wa sheria katika hatua mbalimbali, kabla ya haujafikishwa bungeni, namna utakavyowasilishwa na kujadiliwa (pamoja na kamati zake), na hatimaye kupitiwa kuwa sheria.
Muswada wa sheria waweza kuwa wa serikali, ambao huwasilishwa na Mwanasheria Mkuu, Waziri au wa Mbunge ambaye si waziri, mwanasheria wa serikali na pia unaweza kuwa wa kamati ambao utawasilishwa na mwenyekiti au mjumbe.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Johnson Mwanyika alisema wiki iliyopita alisema kwamba suala hilo halijafika kwao kama ombi.
"Umesikia wapi hilo, sisi hatujalisikia kaulize oOisi ya Bunge wao watakuwa wanajua vizuri zaidi," alisema Mwanyika kwa kifupi.
Hivi karibuni kumueibuka mjadala ambapo wabunge wanasema kuna haja ya kuiona mikataba na kuijadili bungeni kabla serikali haijatia saini.
Miongoni mwa mikataba mibovu ya hivi karibuni ambayo imeibua mjadala ni pamoja wa Kampuni ya kufua kuzalisha umeme ya Richmond Development Corporation (RDC) na mgodi wa dhahabu wa Buzwagi.
Source: Mwananchi