Basi kuyafahamu yote hayo, fuatilia mfululizo wa matoleo ya makala katika gazeti hili ambapo tutakuletea mwanzo mwisho wa tukio hilo, kesi ilivyoendeshwa hadi kufikia uamuzi wa washtakiwa 11 kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Katika sehemu hii ya kwanza, tutaangalia tangu marehemu ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya Protected Area Management System (PAMS) na mkurugenzi mwenza walivyoondoka Arusha hadi anauawa Dar es Salaam.
Usiku wa Agosti 16, 2017, Wayne akiwa na mkurugenzi mwenza wa Pams walisafiri kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) pasipokujua kuna kifo kinamsubiri.
Hakufahamu kama dereva aliyemchukua kutoka Arusha mjini kwenda KIA ambaye wamemfahamu kwa miaka mingi na dereva teksi atakayewapokea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jullius Nyerere (JNIA), Jijini Dar es Salaam, wamekula njama ya kumuua.
Baada ya kutua JNIA, walipokelewa na dereva teksi wa siku zote anayewapokea aitwaye Michael Daud Kwavava ambaye wamemfahamu kwa zaidi ya miaka 10, aliwachukua kuelekea Babao Village ambako ndipo walipokuwa wakielekea.
Wakiwa njiani walipofika katika njiapanda ya Barabara ya Kaole na Haile Selassie katika eneo la Masaki, walizuiwa kwa mbele na gari lingine na kwa mshtuko ndani ya gari hiyo walishuka watu walioonekana ni majambazi.
Majambazi wawili walilisogelea gari lao na mmoja akachukua kompyuta mpakato (laptop) zao na baadhi ya nyaraka ambazo walikuwa wakizifanyia kazi, mmoja alikuwa na silaha na alimfyatulia risasi mwanaharakati huyo. Baadaye majambazi hao waliokuwa na gari aina ya Toyota IST, walitokomea kusikojulikana na Wayne alikimbizwa hospitali ya Sally International ambayo haikuwa mbali na eneo la tukio, lakini tayari alikuwa amefariki dunia.
Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza upelelezi kuwabaini nani wanaoshukiwa kuhusika na mauaji hayo na washukiwa 18 walikamatwa wakiwamo raia wawili wa Burundi na mwanamke Rahma Mwinyi. Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani na katika usikilizwaji wa shauri hilo Mahakama Kuu walipangwa kuanzia mshtakiwa wa kwanza Khalid Mwinyi au Banyata, hadi mshtakiwa wa 18, Almas Swedi maarufu kwa jina la Malcom.
Wengine kuanzia namba mbili walikuwa ni Rahma Mwinyi au Baby, Nduimana Ogisye ambaye ni raia wa Burundi, Godfrey Salamba, Chambie Ally, Allan Mafue, Ismail Mohamed au Machips, Leonard Makoi na Ayoub Seleman Kiholi.
Mbali na washtakiwa hao, walikuwepo Joseph Lukoa, Gaudence Matemu, Abuu Mkingie, Habonimana Nywandwi au Ogistee ambaye ni raia wa Burundi na Michael Kwavava aliyekuwa dereva teksi aliyewabeba Wayner kutoka JKIA.
Wengine katika orodha hiyo ni Emannuel Sonde, Kelvine Soko, Samia Hujat na Almas Swedi au Malcom na wote walikanusha mashtaka matatu ya kula njama kufanya mauaji na kumuua kwa kukusudia Wayne.
Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo na Jaji Leila Mgonya, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akawasilisha maombi kwa njia ya chemba ambayo yalikubaliwa, kwamba kesi iendeshwe faragha ili kulinda mashahidi.
Kutokana na ombi hilo ambalo lilikubaliwa na Jaji Lameck Mlacha katika uamuzi wake wa Desemba 8, 2020, mashahidi wote 32 waliotoa ushahidi walitambuliwa kwa vifupisho vya maneno AA hadi AZ na BA hadi BF 32.
Katika ushahidi huo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mawakili wa Serikali saba wakiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Yamiko Mlekano na mahakama ilipokea pia vielelezo 43 yakiwamo maelezo ya ungamo ya baadhi ya washtakiwa.
Mathalan katika mahojiano yaliyorekodiwa, mshtakiwa wa tatu ananukuliwa akieleza namna alivyoelezwa kuwa mzungu (Wayne) angekuja na usafiri wa ndege siku hiyo huku mwingine akinukuliwa akielezea mgawo wa fedha ulivyokuwa.
Ni katika maelezo hayo ya ungamo, unakuta simulizi za mshtakiwa wa nne, Salamba anavyoeleza walivyokwenda JNIA baada ya mauaji na mshtakiwa wa tatu aliyemfyatulia risasi marehemu, alikabidhiwa mgawo wake wa Sh20 milioni.
“Huyo Allan Mafue alitoa Sh20 milioni ambazo alikabidhiwa Zebedayo kama mgawo wake katika nafasi yake ya uuaji kama alivyoahidiwa, baada ya hapo tulimrudisha Zebedayo Temeke nyumbani kwa Fahami Karama,” anaeleza. Maelezo mengine ni ya mshtakiwa wanane, Makoi anayesema katika maelezo yake “Ni kwamba mwaka 2017 mwezi wa saba tarehe sikumbuki alinipigia simu mzee mmoja anayeitwa Machips jina kamili silifahamu akaniambia kuna biashara.
“Nilimuuliza ni kazi gani akaniambia kuna mzungu anayehusika na meno ya tembo anatakiwa auawe. Akaniambia kama kuna watu wanaweza kufanya hizo kazi niongee nao, ili tukubaliane kazi ifanyike,” ananukuliwa Makoi akisema.
Shahidi wa kwanza
Shahidi wa kwanza aliyetambulika kama AA ambaye ni daktari anayefanya kazi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anasema Agosti 19, 2017 alisaidiana na daktari mwenzake ndio walioufanyia uchunguzi mwili wa Wayne.
Katika uchunguzi huo walibaini marehemu alikuwa na jeraha karibu na mdomo na walipochunguza zaidi ndani waliona kipande cha chuma ambacho waliamini ni risasi ilipenya hadi mkono wa kushoto wa marehemu. Kutokana na risasi hiyo, mfumo wa upumuaji ulizibwa na damu na kwamba sababu za haraka za kifo ilisababishwa na kukosa hewa katika mfumo wa upumuaji kutokana na kuganda kwa damu.
Baada ya uchunguzi huo aliandaa ripoti ya uchunguzi ambayo ilipokelwa mahakamani kama kama kielelezo namba moja.
Itaendelea kesho