Mkurya romantic
Member
- Jul 21, 2022
- 41
- 61
Katika orodha ya watu muhimu waliofariki nchini mwaka 2020, Jina la Erasto Barthlomeo Mpemba halimo! Watu waliofariki mwaka huo, na misiba yao kuadhimishwa kitaifa mwaka huo, wamo Rais mstaafu Benjamin Mkapa, John Kijazi, Mchungaji Rwakatare, Jaji Agustino Ramadhani, Waziri Agustine Mahiga—wote, ama ni wanasiasa, au viongozi flani.
Kwa kifo chake kutoripotiwa na chombo chochote cha habari, umuhimu wa Mpemba ulizidiwa hata na matukio ya kawaida kabisa ya mwaka huo kama vile, Tanzania kuingia uchumi wa kati, Bwana Laizer kupata jiwe kubwa la Tanzanite kuwahi kutokea na hafla ya marais wasaafu kuzawadiwa ndege wa tausi kutoka Ikulu.
Inawezekanaje mtu anayetambuliwa na taasisi za kisayansi duniani kama mgunduzi akafa, asiadhimishwe na habari zake zisiandikwe na chombo chochote cha habari nchini mwake?
Hata hivyo hatupaswi kushangaa sana—katika jamii yenye utamaduni wa kuadhimisha wanasiasa na watumbuizaji peke yake, jambo hili linawezekana.
Leo ukijaribu kuandika popote mtandaoni neno “Mpemba”, utashangaa kuona wingi wa link zinazomtambulisha Mtaanzania, Erasto Mpemba na ugunduzi wake uliokuja kupewa jina la “Mpemba Effect”!
Wakati akisoma katika Sekondari ya Magamba mkoani Tanga huku akijikimu na biashara ya kutengeneza Ice cream, Mpemba aligundua kuwa, maji ya moto na yale ya baridi yakiwekwa pamoja katika jokofu au freezer, maji moto huganda mapema kuliko maji baridi.
Ugunduzi wake ulikuja kuchochea tafiti na makala nyingi sana za kisayansi kutaka kujua kwa nini maji moto yagande haraka kuliko ya baridi. Mwaka 2012 Mpemba alikaribishwa kujiunga na wanasayansi wa Royal Society of Chemistry nchini Uingereza ambako ilitegemewa mshindi wa shindano la kutegua kitendawili cha Mpemba angetangazwa na kuzawadiwa. Kabla ya tukio hilo, RSC ilikuwa imetangaza shindano la kutengua kitendawili hicho. Jumla ya watu 22,000 kutoka nchi 122 walishiriki shindano la nadharia ya Mpemba.
Japo wapo pia wanaodai kuwa ugunduzi wa Mpemba umepata kugusiwa na watu wengine kama Aristotle zamani kabla Yesu Masihi hajazaliwa, bado hoja ya maji moto kuganda kabla ya maji baridi inatambulika zaidi na jamii ya wanasayansi kama hoja ya “Ice cream man“, Erasto Barthlomeo Mpemba.
Taarifa mitandaoni zinasema kuwa, Erasto Mpemba, mhitimu katika chuo cha African Wildlife Management huko Moshi, na baadae shahada ya kwanza na ya uzamili katika vyuo vya University of Canberra nchini Australia na Alpine, Texas Marekani, na aliyekuja kulitumikia Taifa kama Afisa mwandamizi katika Wizara ya Maliasili na Utalii alifariki mwaka 2020. Hakuna tarehe. Hakuna mwezi.
Pengine swali la kujiuliza hapa ni kwamba: Inakuwaje mtu kama huyo afariki, pasiwe na mjadala wowote nchini kwake, asiandikwe na chombo chochote cha habari na kifo chake kizidiwe umashuhuri na kifo cha Agnes Masongange?