Zitto
Former MP Kigoma Urban
- Mar 2, 2007
- 1,562
- 10,888
Nasubiri Bandari Kubwa ya Lamu izuie Bandari Ndogo za Dar na Mombasa: Namna Maarifa Madogo Yanavyoiua Bandari ya Bagamoyo na Kuifaidisha Kenya
Kumekuwa na mijadala mikali kuhusu Mradi wa Eneo la Kiuchumi la Bagamoyo. Mjadala huo wenye malumbano ya kurushiana shutuma umekuwa mjadala mbovu sana kwenye jambo nyeti la kiuchumi Kama vile Mradi wa Bagamoyo SEZ. Wanaounga mkono wanaona fursa za maendeleo katika Mradi, wanaopinga wakiona hasara nchi itapata. Wanaopinga wanawashutumu wanaounga mkono kuwa wanataka kuuza Nchi.
Kundi la wanaopinga linaongozwa na Rais John Magufuli, Spika wa Bunge ndg. Ndugai mwanzoni alikuwa kinara wa kuunga mkono Mradi kwa hoja nzito zenye nguvu. Lakini baadaye alisalimu amri kwa hoja dhaifu sana na hivyo kujisalimisha kwa Rais Magufuli kwenye hoja nyepesi zilizojaa woga na zisizo na tafakuri yenye mwono mpana wa Uchumi wa Jiografia.
Sasa inadhihirika kuwa Rais Magufuli anatumika dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maslahi ya Jamhuri ya Kenya. Nitafafanua.
Kila nchi ina picha kubwa katika mambo inayotaka kuwa (a grand vision). Picha hiyo kubwa inapaswa kuzingatia mazingira ya nchi husika (context) na namna ya kuyatumia mazingira hayo kufikia hiyo picha kubwa. Tanzania na Kenya ni nchi ndugu ndani ya familia ya Afrika Mashariki. Nchi hizi pia ni Nchi shindani kiuchumi. Ni nchi pekee za Afrika Mashariki ambazo zote zina pwani ya Bahari (access to the sea). Lakini Tanzania ina Pwani ndefu zaidi kuliko Kenya na hivyo kuipa fursa kubwa zaidi.
Nchi zote mbili zinapakana na nchi ambazo hazina pwani. Kenya inapakana na Ethiopia, Sudani Kusini na Uganda. Tanzania inapakana na Uganda, Malawi, Zambia, Kongo DRC, Burundi na Rwanda. Tanzania ina fursa zaidi kuliko Kenya kutokana kupakana na Nchi nyingi zaidi. Kenya kwa muda mrefu imekuwa ikishika biashara ya nchi inazopakana nazo na isizopakana nazo pia. Tanzania imekuwa ikisuasua kufaidika na nafasi yake kijiografia katika kushika biashara ya eneo hili la maziwa makuu. Miji inayoongoza ushindani wa Biashara wa nchi hizi ndugu ni Mombasa na Dar es Salaam. Ni miji ya Bandari, yote ikitawaliwa na Sultan wa Zanzibar wakati fulani na baadaye wababe wa Vita za Dunia Uingereza na Ujerumani kugawana miji hiyo - Mombasa kwa Waingereza na Dar es Salaam kwa Wajerumani.
Hata hivyo Bandari zote hizi 2 zimekuwa ni Bandari za mizigo inayopita (transit goods) kwa kuwa vina vyake ni vidogo hivyo kuweza kupokea Meli ndogo tu. Meli kubwa kutoka China hufika Singapore na kupakua mizigo kuweka kwenye Meli ndogo zinazokuja kutia nanga Mombasa au Dar es Salaam. Meli kubwa kutoka Ulaya hushusha mizigo kwa Meli ndogo huko Bandari ya Salalah, Oman. Ili kuwezesha Meli kubwa kufika Pwani ya Afrika Mashariki, Nchi ndugu za Kenya na Tanzania zikaanza kuwaza na kuwazua miradi ya kufanya ili kuwa Kituo Kikubwa cha Biashara ya Bahari Eneo la Afrika Mashariki (transshipment hub). Mzozo wa kimkakati ulianzia hapo katika ya Nchi rafiki Kenya na Tanzania.
Jamhuri ya Kenya ilitumia diplomasia ya Hali ya Juu kuunganisha Nchi za Rwanda, Uganda, Ethiopia na Sudan ya Kusini kwenye Mradi wa picha kubwa wa Bandari ya Lamu. Ikazaliwa kinachoitwa ‘Northern Corridor’. Tanzania ikatengwa katika Afrika Mashariki (EAC) kikaanzishwa kitu kinaitwa ‘Coalition of the Willing’. Kenya wakazindua kwa fujo Mradi wa Bandari ya Lamu ili kuwa Bandari ya Meli kubwa za Afrika Mashariki. Marais wa nchi zote za coalition of the willing za EAC na nje ya EAC walikusanyika huko Lamu kuanzisha Mradi huo.
Uongozi wa Awamu ya Nne wa Tanzania chini ya Rais Jakaya M Kikwete nao wakaamua kutumia mtaji mkubwa wa diplomasia aliouacha Mwalimu Nyerere kujibu mapigo. Mapigo ya Lamu ni Bagamoyo. Rais Kikwete akafanikiwa kuwashawishi Rais Xi Jinping wa China na Sultan Qabos Bin Said wa Oman kuisadia Tanzania katika mpambano wa kuishika Bahari ya Hindi. China na Oman wakakubali kuanzisha Mradi mkubwa wa kituo cha Meli katika Afrika na Eneo Huru la Uchumi pale Bagamoyo. Mradi wenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 10.
Rais Jakaya Kikwete alifanya kosa analolijutia, naamini, mpaka sasa. Aliondoka madarakani bila kutia saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi. Makosa haya yanaigharimu Nchi sasa kwani ushindi wa kuimiliki na kuitawala Biashara ya Bahari ya Hindi upande wa Magharibi umekwenda Kenya bila hata risasi moja kurushwa. Mradi wa Bagamoyo umehujumiwa. Umekufa.
Baada ya Utawala wa Awamu ya Tano kuingia madarakani waliokuwa ‘coalition of the willing’ wakajisogeza karibu. Rwanda ikatangaza kuegemea Central Corridor. Tanzania ikabadili mpango wake wa Kujenga Reli kutoka Dar es Salaam kupitia Uvinza mpaka Musongati nchini Burundi na sasa ikaamua kuielekeza reli Isaka kwenda Rwanda. Badala ya Uvinza kuwa Kituo cha Biashara na Mizigo kwa Nchi za Maziwa Makuu, Sasa itakuwa Kigali, Rwanda.
Rwanda tayari imefungua Kigali Logistics Platform na Bandari huru ya Masaka (Kigali) yenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 35. Bandari hiyo itaendeshwa na Kampuni kubwa duniani ya kuendesha Bandari iitwayo Dubai World. Kwa mkakati huu Rwanda itabeba mzigo wote kutoka DRC na kuhudumiwa kupitia Kigali, na hivyo Uvinza (Kigoma) kujifia kwa kukosa Biashara. Tanzania imepoteza kwa Rwanda.
Kenya kwa upande wake ilianza vibaya mahusiano yake na Tanzania ya utawala mpya. Katika hali ya kuweka maslahi ya nchi yao mbele wanasiasa wa Kenya waliamua kuungana katika kile kinachoitwa ‘handshake’, na ndugu Raila Amolo Odinga akapewa rasmi kazi ya kuhakikisha anasimamia hiyo diplomasia ya Kenya inafanikiwa. Propaganda kali dhidi ya Bagamoyo zikaanza na safari za Raila kuja kuonana na Magufuli zikawa nyingi pengine wakikutana Chato na pengine kwa Siri.
Baadhi ya watendaji wakanyweshwa sumu za ubovu wa mkataba wa Mradi wa Bagamoyo (ambapo hapakuwepo na Mkataba). Serikali ya Awamu ya Tano ikatamka rasmi kuwa hawataki Mradi ule kwa sababu za kitoto kabisa, kwani walitumia nyaraka za majadiliano na Mwekezaji. Spika wa Bunge alipoinua sauti yake akanyamazishwa. Vyombo vya Habari vikalishwa sumu na Mradi ukanuka. Msemaji wa Mradi wa Bagamoyo siku zote ni Wizara ya Viwanda na Biashara, lakini ghafla Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) ndio ikawa ndio Msemaji badala ya Wizara. Na baadhi ya Watendaji wa Serikali wenye mwono wa mbali walipotoa mawazo yao wakaondolewa kwenye nafasi zao.
Baada ya mradi wa Bagamoyo kuuawa, Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya Raila Odinga akapewa tuzo na nchi yake kwa kuifanya Kenya kuwa mtawala wa Bahari ya Hindi, tuzo ya ‘Maritime Champion of the Indian Ocean’. Na Rais Kenyatta akawa rafiki ya karibu ya Rais Magufuli. Nchi yetu ikiwa imepoteza miaka minne sasa bila kutekeleza mradi wa Bagamoyo.
Ujenzi wa Bandari yenye kina kirefu ya Lamu sasa kuzinduliwa rasmi Novemba, 2019. Sasa Lamu itapokea Meli kubwa za 4th Generation kama vile Suezmax, Neo-Panamax na Chinamax. Mizigo kutoka Meli kubwa itashushwa Lamu na kupakiwa kwenye Meli ndogo kuja Bandari ya Dar es Salaam na kwenda Bandari nyengine za Afrika kama Beira na Durban. Hii ndio kazi ilikuwa ifanywe na Bandari ya Bagamoyo - Mradi ambao umehujumiwa. Pia Kenya wameamua kuchukua mpango mzima wa Bagamoyo na kuutekeleza Lamu kwa kuanzisha Eneo Maalumu la Uchumi. Hapo kabla ilikuwa iwe Lamu Port Pekee.
Watawala wetu wameonyesha uwezo mdogo sana wa kung’amua mambo na kujikuta kuwa sehemu ya Hujuma kwa Nchi yetu. Faida ya kijiografia ya nchi yetu ambayo Mungu alitupa tumeipoteza. Baadhi ya watu wanashangilia ujinga huu wa kiuchumi ambao tumeufanya bila kujua. Shida kubwa ya watu wenye mamlaka ya Dola katika nchi yetu hawasomi kujiongezea MAARIFA ili kuepuka hujuma dhidi ya nchi yetu, hujuma ambazo zitaathiri vizazi na vizazi.
Tumepoteza fursa ya nchi kwa sababu za kitoto, zisizo na maana na za kipropaganda tu. Kuendesha bandari miaka 99 mara tunataka miaka 33 haiwezi kuwa sababu kwa mtu mwenye akili timamu wakati Mradi ni Joint Venture na Serikali ni mbia mwenye hisa zinazotokana na ardhi yake. Kuna mwekezaji atabeba ardhi ya Tanzania kuipeleka China au Oman? Eti Bagamoyo itaua Bandari ya Dar es Salaam, kwa hiyo Ujenzi wa Bandari ya Lamu utaua Bandari ya Mombasa? Nasubiri kuona Bandari ya Dar ikifa kwa sababu ya ujenzi wa Bandari ya Lamu.
Biashara ya Bandari ya Bagamoyo ingekuwa kwa Meli kubwa kuleta mizigo na Meli ndogo kuja kubeba kupeleka Bandari za Afrika nzima kazi ambayo haifanywi na Dar es Salaam na wala haitaweza kufanywa kwa sababu Eneo la Bandari ya Dar ni dogo. Kazi ambayo sasa itafanywa na Bandari ya Lamu.
Hujuma hii kwa Jamhuri ya Muungano haipaswi kupita bila kulipiwa. Rais Magufuli na Serikali yake wanapaswa kulipa gharama ya hujuma hii kwa Nchi yetu. Wasipolipia watakuja Viongozi wengine kuhujumu nchi yetu kama hawa. Wakiadhibiwa itakuwa somo kwa wengine. Kwa uelewa mpana kuhusu Uchumi wa Bahari soma Gazeti la The East African la October 26 - November 1, 2019: Inside Kenya’s plan to rule EA Coast.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge - Kigoma Mjini
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Oktoba 28, 2019