LOooh, mkuu 'William Mshumbusi', umeweka bonge la mada hapa, lakini najua, kama kawaida yetu siku hizi hapa JF, tutaigusagusa tu na kwenda zetu kwenye utani wetu wa CCM na CHADEMA!
Umeanza na mfano mzuri sana wa TAZARA, jinsi reli ile ilivyojengwa haraka na kwa ufanisi na wachina. Madhumuni wa ujenzi wa reli ile ulijulikana bayana, kuondokana na utegemezi wa nchi za mstari wa mbele katika ukombozi kuwategemea makaburu katika maswala yao ya uchukuzi na usafirishaji wa mizigo yao.
Kabla ya mchina kujenga ile reli, wafadhiri wa nchi za Magharibi waliombwa kusaidia kuijenga, wakang'aka, huku wakisema reli eneo hilo haina faida. Hao hao, walipoona mchina anaijenga reli, haraka wakawa mbioni kwenye ujenzi wa barabara. Unaweza kutafsiri mwenyewe maana ya hayo yote.
Reli, kama ulivyoeleza ilifanya kazi vizuri mwanzoni mwa utumikaji wake, na umeeleza kwa nini kadri miaka ilivyoendelea, ndio ufanisi wake ulivyozidi kufifia hadi sasa.
Binafsi ningependa sana ukazie hapa, penye udhoofu wa ufanisi. Ueleze sababu hasa ni zipi, pamoja na kwamba umegusia kama kawaida yetu sote siku hizi, lawama za kwamba serikali haiwezi kufanya biashara. Mimi sikubaliani na jibu hilo jepesijepesi hivyo. Serikali inaweza sana kufanya mambo yake kwa ufanisi iktaka kufanya hivyo. Nyakati hizi haifanyi hivyo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo hiyo ya sekta binafsi unayoipigia chapuo hapa, ikiwa ndio kikwazo kikubwa sana katika kudhoofisha shughuli za serikali.
Wenye malori bila shaka hawawezi kulaza damu wakiona shughuli za reli zinafana huku zikiwapunguzia wao wanachokitafuta. Tunaweza sana kulijadili hili, hata kama hatuwezi kukubaliana.
Matatizo yanayojitokeza ndani ya mashirika ya umma, yanaanzia huko huko kwenye sekta binafsi, na ukosefu wa usimamizi bora ndani ya mashirika yenyewe. Hii haimaanishi kwamba udhaifu huo hauwezi kudhibitiwa kama serikali ikiamua na kuwa na nia ya kufanikisha shughuli zake. Kusema serikali haiwezi kufanya biashara, ni sawa pia na kusema serikali haiwezi kufanya shughuli yoyote kwa ufanisi. Kwa hiyo tuondoe serikali tubinafsishe shughuli zote zinazofanywa na serikali?
Tusifanye uwekezaji ndio uwe muarobaini wa matatizo yetu, kila mara tunaposhindwa kwa uzembe tu, eti tukimbilie kwenye uwekezaji.