MTIZAMO WANGU KUHUSU BODI YA MCC KUSITISHA
MSAADA WA MCC 2 KWA SERIKALI YA TANZANIA
Na Alexander Mhando
Utangulizi;
Tukianza na nukuu ya Baba wa Taifa alisema “…….
Inapotokea taifa kuuza uhuru wake kwa ajili ya misaada ya kiuchumi au kukubali kukaliwa na majeshi ya nje, taifa hilo linakuwa limepotea na litanyonywa na watu wake watakuwa wanakandimizwa popote pale……” alisema Mwalimu.
Katika swala la msaada wa pesa za
Millenium Challenge Corporation’s (MCC) ambazo huwa tunapewa nchi zinazoendelea kama msaada kwa ajili ya Maswala ya maendeleo kwa Nchi zetu, Pesa hizi hutolewa na Bodi ya
Shirika la changamoto za Milenium (MCC) ambayo inamilikiwa na serikali ya marekani ili kusaidia nchi zinazoendelea.
Katika kikao cha Bodi ya MCC kilichokaliwa jana tar 28/3/2016 kimefikia uamuzi wa kutishia kusitisha pesa za msaada za MCC kwa Tanzania kwa sababu walizozitoa wao ambazo ni swala la uchaguzi wa Zanzibar na swala la sheria za makosa ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika uchaguzi wa Zanzibar na wa mwaka jana.
Tukikumbuka Katika kikao cha tar 16 December mwaka jana cha Bodi ya MCC, Bodi ya MCC katika kikao chake ilijadili pendekekezo la mkataba mpya na serikali ya Tanzania wenye thamani za Dola za Kimarekani Millioni 472.8 na kuamua pesa hizo zitolewe baada ya Tanzania kutimiza kigezo cha kuzuia Rushwa. Msaada huo ulikuwa ni maalumu kwa ajili ya kuimarisha secta ya umeme nchini, likiwa lengo ni kuwawezesha watanzania wengi zaidi kupata nishati hiyo kwa uhakika na kwa bei nafuu. Lakini pia kuimarisha taasisi zinazohusika na usambazaji wa nishati ya umeme na usimamizi wake.
Katika hali ya kushangaza swala la Rushwa limeshafanyiwa kazi na serikali ya awamu ya Tano kwa kasi kubwa kupambana na Rushwa na Ufisadi lakini bado Bodi ya MCC wanakuja na hoja nyingine nakuaacha ile ya kwanza ya Swala la Rushwa na ufisadi. Sasa swali la kujiuliza je, MCC wanataka tuuze uhuru wetu na utu wetu kwa pesa za msaada??
Mtizamo wangu;
Hatutakiwi tudharau misaada yoyote tunayopewa lakini tusikubali katu kuuza uhuru wetu au mali zetu kwa sababu ya msaada, tukikumbuka mwalimu Nyerere mwaka 1964 alikubali kuvunja uhusiano na Ujerumani Magharibi pale walipotaka kuingilia umoja wetu na Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar. Lazima tujue kuwa MCC ni sehemu tu ya Bodi inayojitegemea na sio serikali ya Marekani japo inasimamiwa na serikali ya Marekani, kwa hiyo kukosa msaada wa MCC hautatuathiri chochote katika uhusiano wetu na Taifa la Marekani kwani kauli ya MCC sio Kauli ya Serikali ya Marekani. Uhusiano wetu na Taifa la Marekani bado uko palepale na hautatetereka kwa sababu ya pesa za MCC.
Tukikumbuka AZIMIO LA ARUSHA la mwaka 1967 chini ya TANU lilikuwa na maudhui mbalimbali, moja lilikuwa ni swala la Pembe tatu za ukombozi ambapo lilitambua kwamba uhuru wanchi hautakuwa na maana wala hatutakuwa salama kama tukiendelea kuwa tegemezi , yaani kutegemea misaada , mikopo na uwekezaji kutoka nje. Kwa sababu mikopo haitapatikana ya kutosha na hiyo kidogo itakayopatikana itaambatana na masharti yatakayodidimiza nchi zaidi. Isitotoshe hata kama tungepata misaada, mikopo na uwekezaji kwa ajili ya maendeleo vitahatarisha uhuru wetu. Mwalimu Nyerere katika kitabu cha Azimio la Arusha amesema,
“Kujitawala ni kujitegemea, kujitawala kwa kweli hakuwezekani ikiwa Taifa moja linategemea misaada na mikopo kutoka Taifa jingine kwa maendeleo yake” mwisho wa kunukuu.
Pia tuambue kuwa Serikali ya Tanzania kwa awamu hii ya Tano chini ya Raisi Dr John Pombe Magufuli, imejipanga kikamilifu katika kukusanya kodi na kutafuta pesa kwa ajili ya kuendesha serikali bila hata kutegemea misaada ya wahisani ambayo ina masharti magumu na yenye ukandamizaji na unyonyaji ndani yake. Katika Pesa hizi za MCC lazima tujiandae kisaikolojia na sio kupotosha kwani Tukipatiwa pesa hizi au Tusipopatiwa pesa hizi bado tunaamini tutaweza endesha serikali yetu na maisha yetu kama kawaida. Tukumbuke kuwa pesa hizi zilianza kutolewa mwaka 2008 , Je, kabla ya hapo serikali ilikuwa inajiendesha vipi? Kama Tuliweza kujiendesha maisha yetu na serikali kwa kipindi hicho , hata sasa tutaweza. Hatudharau pesa za msaada na za wahisani lakini tusitumie kama kigezo cha kuondoa uhuru wetu na utanzania wetu kisa pesa za misaada. Lakini pia tutambue kuwa pesa za MCC sio marekani pekee anayechangia zipo nchi nyingine .
Lakini pia Vyama vyetu vya siasa nchini vijifunze utaifa na uzalendo, Ni aibu kuona chama cha Siasa cha Tanzania kinaungana na maadui wakutoka nje wasioitakia mema nchi yetu kwa kushabikia kila nia yao ovu juu ya maendeleo ya nchi yetu, tutambue kuwa si kila nchi kwa sasa inafurahia mafanikio ya Tanzania mfano uwepo wa Gesi, Madini yakutosha aridhini, wanyama pori wa kila aina, mlima Kilimanjaro,samaki wakutosha ziwani na baharini, ardhi ya kutosha, Bandal, misitu mikubwa, n.k hivi vyote tutambue si kila taifa litafurahia sisi kuwa navyo wanatamani tuvunje amani yetu ili waje wachukue mali zetu.
Rai yangu kwa Vyama vya upinzani nchini jaribuni kuweka utaifa kwanza na siasa baadae, swala la kukaa kushabikia vibaraka weupe wenye lengo la kutukandamiza sio jambo zuri hata kidogo na huo sio uzalendo. Katika Tamko lililotolewa na CHADEMA lenye kichwa cha Ujumbe “Hatma ya msaada wa Fedha za MCC kwa serikali ya Tanzania” ni tamko linaloonesha kushabikia swala la MCC kuikandamiza Tanzania. Tusilete siasa kwenye maswala ya kitaifa na maendeleo ya wananchi. Na hii inaonesha kuwa vyama hivi kama vitapewa dora vitaongoza nchi kwa kutegemea kuombaomba kwa wazungu na mwishowe vinaweza hata kuuza mali za nchi ili kutafuta msaada nje, kwa hili upinzani badilikeni wekeni utaifa mbele na sio tamaa ya uongozi.
Mwisho;
Lazima tujue kuwa msaada mtu anahiyari yake akusaidie au la. Vile vile misaada ni silaha kubwa kwa nchi za magharibi kulidumaza bara la afrika na kuhakikisha haliwezi kujitegemea bali liwategemee wao kwani misaada mingi inayotolewa na nchi hizi hailengi sehemu za maendeleo ya nchi na wananchi wake, na siku zote riba zake huishia kuwa kubwa kuliko misaada yenyewe na kwa kweli nchi yenye kujitambua haiwezi kujiendesha kwa kutegemea misaada hasa kutoka nchi kama marekani utanynyasika tu.
COPIED AND PASTED
Ni mtizamo wako juu ya MCC , binasfi namuunga mkono aliyeandika huu waraka kiukweli sio muda wa kumbembeleza msaada , bora tupambane tujitegemee.