Kitendo hiki kilichofanywa na hawa askari wa Mtwara na wale wa Zombe wakati ule, na wengi wa aina kama hiyo ni sehemu ndogo ya ushenzi, uonevu, ukatili na uovu mkubwa unaofanywa na jeshi la polisi dhidi ya raia wake nchi nzima. Ni bahati tu kwamba kesi hii imefika hapa kwasababu ya nguvu ya mkono wa kiongozi kigogo mmoja serikalini,vinginevyo hii nayo ingeishia chinichini kama zilivyo kesi nyingi zingine zilizopita.
Jambo la kusikitisha ni kwamba matendo ya kiovu yanayofanywa na jeshi la polisi ni 'reflection' ya jamii nzima ya kitanzania ilivyo kwa sasa, lakini ukigeukia sekta zingine mambo yako hivyo hivyo - yaaani ni ukatili, uonevu na uovu kwa kwenda mbele. Matendo ya polisi hawa hayana tofauti na wayafanyayo maofisa wa TRA wanapowafanyia dhuluma wafanya biashara, hayana tofauti na baadhi ya walimu, wahadhiri wa vyuo vikuu wanaotoa alama na ufaulu kwa rushwa ya fedha na ngono kutoka kwa wanafunzi, hayana tofauti na raia wa kawaida mashuhuda wa ajali badala ya kuwaokoa majeruhi wa ajali ya gari lakini badala yake wanawapora majeruhi hao fedha zao, simu zao wakiwa mahututi, hawana tofauti na mwananchi aliyetumiwa fedha kwa simu kwa makosa na hata pale anapoambiwa kwamba rudisha au toa ushirikiano hataki na harudishi fedha hizo, hawana tofauti na maofisa ardhi wanafanyia kila aina dhuluma wananchi kuhusu haki zao za ardhi. Hawana tofauti na viongozi wanaoendesha Ma -V8 wasio na shida na wala wasioathirika na mgao wa umeme, upungufu wa maji lakini wala hawana hata chembe ya huruma na wananchi wanaotaabika na shida zinazoweza kutatulika kwa haraka.
Wanaotoa mawazo ya kulivunja jeshi la polisi, inabidi pia watafakari kuvunja TRA, NHIF, Halmashauri zetu, maana hizo ni vichaka vilivyojaa uonevu na kila aina ya uovu kila kukicha.