Mikosi, Kila kitu kibaya Mimi. Dhambi zangu hazijai hata kikombe lakini niliyoyapitia ni magumu kuliko umri wangu.
Lakini ukitazama wengine kwenye matendo maovu yote huwakosi, Ila wamejaa neema tele. Kila kitu kizuri kwao.
Ninapoelekea naenda kutokumwamini huyu kiumbe wa kuitwa Mungu. Maana kama kweli yupo ni mtesaji na mnyanyasaji kweli.
NIMEMALIZA.
Pole sana. Kupitia magumu ni maisha ambayo yanafikirisha sana, ila kunakuimarisha na kuwa mfano kwa wengine wa kutokata tamaa (kuwa mvumilivu) kunakotakiwa katika maisha. Kila mmoja wetu anapitia katika maisha fulani, ambayo anaweza kuyaona ni magumu kuliko ya watu wengine, na wakati huo huo wengine nao wanaoonekana wana maisha mazuri wanatamani wangeishi maisha tofauti na hayo. Mfano, wewe unaweza kuwa unatamani maisha ya X na X anatamani maisha ya Y na Y anatamani maisha ya Z, nk.
Niliwahi kuishi Malawi na jirani yangu alikuwa mtu mwenye maisha mazuri sana (kwa jinsi alivyoonekana): nyumba nzuri, gari zuri, mke mzuri na alikuwa akiwasaidia sana ndugu zake kutoka kijijini na hata watu wengine. Kama uko karibu naye na ukikwama ukimwomba msaada wa fedha anakuuliza "ungetaka nikupe cash au nikurushie kwenye simu"? Ukisema "cash" anakupa, na ukisema "nirushie" anakurushia kiasi ulichomwomba. Kwa hiyo, mimi na mke wangu nilimwona ni mtu mzuri na mwenye moyo wa kusaidia watu, lakini watu wa nyumbani kwake, akiwemo mkewe, walimwona mtu asiye mstaarabu na wakati fulani hata mkewe alimkimbia na kurudi kwao kwa madai kwamba anamnyanyasa na hakuona kama maisha wanayoishi ni maisha ya heri. Hata ndugu zake waliokuwa naye walikuwa hawana raha, hasa anapokuwepo nyumbani, labda kama yuko safarini au kazini. Kwa nini wakati ni familia iliyokuwa inaonekana mambo yanawaendea vizuri almost katika kila jambo na watoto walikuwa wakisoma shule nzuri - walikuwa wakifuatwa kwa gari na kurudishwa nyumbani kwa gari? Watoto wa watu wengine walikuwa wakitembea kwenda shuleni na kurudi nyumbani.
Kuna mfano mwingine pia, familia yenye uwezo kifedha ambayo familia nyingine zilikuwa zikitamani maisha yake, mke mtu alizaa na fundi aliyekuwa akifanya matengenezo nyumbani kwao, tena mara 2. Umeshawahi pia kuona baadhi ya watu wenye uwezo kimamlaka au kifedha wanavyolindwa! Unakuta mtu X ana nyumba nzuri sana iliyozungushiwa ukuta mrefu na juu ya ukuta ameweka nyaya za umeme, mageti imara kwenye lango kuu lna dogo la ukuta, na hata kwenye mlango wa nyumba na milango ya vyumbani, na ana walinzi wenye silaha na yeye ndani ana bastola na silaha nyingine pia.
Lakini unaweza kukuta mtu maskini kijijini, nyumba yake ni ya nyasi na mlango kaweka gunia na upepo ukivuma unaona hata kitanda chake au anaweza akawa ameweka mlango wa matete ambao kufuli lake ni kamba na hata kama amefunga kwa hiyo kamba unaweza kufungua na kuingia bila shida. Lakini je kati ya yule anayelindwa kwa silaha na huyu ambaye mlango wa nyumba yake ni gunia, ni nani unadhani anaishi bila wasiwasi wa maisha? Nani anaona hana usalama wa kutosha?
Hivyo, utagundua kwamba maisha unayoyatamani kuyaishi kwa sababu unaona mtu au watu wengine wakiyaishi vizuri, watu hao pia wanatamani maisha tofauti na kila mtu yuko hivyo. Hali hii yote inaonyesha maisha yetu wote - awe tajiri au maskini - yana upungufu fulani na tunatamani tufikie ukamilifu na huo ukamilifu tunaoutamani ndipo Mungu alipo au niseme ndiye Mungu mwenyewe na kila mmoja wetu anatamani hivyo. Kwa hiyo, hiyo hali unayokutana nayo kiuhalisia unatamani ukamilifu wa maisha yako, maana umeona kwamba maisha unayoyaishi hayatoshi, unatamani maisha tofauti na hata ukiwa na maisha tofauti na uliyonayo kwa sasa, bado utaona tu kuna mambo hayaendi hadi hapo utakapofikia ukamilifu wenyewe. Katika maisha ya ndoa tunapitia 'experience' hiyo pia.
Unapokuwa kijana ukimwona msichana fulani anakuvutia na unaona ni mzuri kuliko wengine na unatamani umwoe. Utakwenda kuwaambia wazazi na ndugu zako kwamba umepata mchumba, lakini baada ya kuoana utaona kwamba uzuri uliokuvutia hauko kwa huyo uliyemwoa, na utaanza kutamani umwoe msichana au mwanamke mwingine unayeona ni mzuri kuliko huyo uliye naye, na unaweza kuoa hata mke wa pili, ambaye unadhani ni mzuri zaidi ya huyo uliye naye. Ukishaoa, baadaye utaona si mzuri kama ulivyodhani, na utatamani mwingine uliyemwona mahali fulani na unaweza kufanya juu-chini umwoe huyo. Naye ukishamwoa, bado utaona kama mwanamke mwingine uliyekutana naye mahali hivi karibuni ndiye mzuri zaidi na ndiyo maana unakuta mtu kaoa/kaolewa, lakini anachepuka na mke/mume wa jirani...na hali hii itaendelea vivyo hivyo hadi wewe mwenyewe utakapoona kwamba huoi tena...na hii yote ni kuonyesha kwamba uzuri hauna mwisho na kila mara utaona ulichonacho si kizuri, bali cha mwenzako ndicho kizuri zaidi - hadi utakapofikia ukamilifu wa maisha yako, ambao ndiye Mungu mwenyewe.
Kuna mfano fulani kwamba mtu fulani aliona maisha yake ni magumu zaidi kuliko ya watu wengine. Siku moja katika kulalamika kwake alikutana na "Mungu" na akamwambia "kwa nini umenipa maisha kama haya tofauti na ya wengine?" Huyo "Mungu" akamuuliza, "una uhakika?" Akasema "ndiyo." Basi Bwana Mungu akamchukua ili akachague maisha anayoyapenda, kisha arudi duniani ayaishi. Maisha ya watu wote alikuwa ameyapanga kwa mfano wa msalaba. "Mungu" akamwambia achagua aina ya 'msalaba' ambao anaona ni mwepesi kwake. Aliponyanyua 'msalaba' wa kwanza akaona ni mzito sana, akaachana nao, akaenda kwa wa pili, nao akaona bado ni mzito.
Basi aliendelea hivyo, hadi akafika mahali akaona 'kamsalaba', alipokanyanyua, akaona kepesi, na akaona "haka kananifaa, maana ile misalaba mingine ni mizito sana.' Basi akamwendea Bwana Mungu na kumwambia "nimeridhika na haka kamsalaba." Bwana Mungu akamuuliza, "umejiridhisha kama kanakufaa, labda ungetafuta kengine!" Yeye akasema "kati ya misalaba yote, hako ndiko nimeona ni nafuu zaidi." Basi Mwenyezi Mungu akamwambia "safari njema". Huyo mtu alirudi duniani na alipofika kuanza kuishi akakuta "kale kamsalaba" alikokachagua ndiko kalikuwa "maisha yake ya awali".
Fundisho la simulizi hili ni kwamba, kila mtu ana maisha ambayo anaweza kuyamudu. Chukulia wewe ni mwanafunzi umepewa mitihani miwili ya kufanya (Hisabati): mtihani mmojajawapo (mtihani A) maswali yake ni rahisi sana na ungeweza kujaza hata umefumba macho na ulipoufanya ukapata 100% na mwingine wenye maswali magumu sana (mtihani B) na ulipofanya ukapata pia 100%. Je, ni mtihani upi utapenda kuwaonyesha rafiki zao kwamba umeufaulu vizuri zaidi? Ni mtihani A au mtihani B, na kwa nini? Asante.