SERIKALI TATU ZANZIBAR NA TANGANYIKA NDIO ZITAONYESHA UPANDE GANI WA MUUNGANO UNA WEZI NA UPI UNA WAADILIFU KWANI MAENDELEO BAADA YA KUANZA HIZO SERIKALI YATAONEKANA KWENYE UPANDE WENYE WAADILIFU.
Tunataka Serikali tatu - Razza
na Martin Malera
MFANYABIASHARA maarufu Zanzibar, Mohammed Razza, amesema kuna mgogoro mzito unaohusu nafasi ya Zanzibar ndani ya Muungano na kupendekeza muundo wa serikali tatu.
Mbali na hilo, Razza alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inapaswa kutangaza mgogoro wa kikatiba, na kupendekeza hatua kadhaa za kuchukua, ikiwemo ya kuwataka marais wastaafu wa pande mbili za Muungano, viongozi na wazee maarufu wakutane haraka ili kuunusuru Muungano ambao alisema Watanzania wengi bado wanaupenda.
Razza ambaye amewahi kuwa Mshauri wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wake na vyombo vya habari, katika Ukumbi wa Hoteli ya Starlight, jijini Dar es Salaam.
Akifafanua muundo wa pendekezo lake hilo, Razza alisema kuwe na serikali tatu ikiwemo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hoja ambayo ilipata kutolewa na wabunge wa kundi maarufu la G55 miaka ya mwanzo ya 1990 na kukataliwa.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa na Razza ni pamoja na kutaka iundwe mahakama ya kikatiba ili kuangalia suala hilo, kwa vile hakuna mahakama yoyote inayoweza kutoa uamuzi wa kikatiba kama huu na kusisitiza umuhimu wa kuwaomba marais wastaafu, viongozi na watu maarufu kukaa chini na kulipatia ufumbuzi tatizo hilo ambalo alisema kwa miaka 40 sasa limeshindwa kutatuliwa.
Alisema ameamua kutoa kauli hiyo baada ya kushtushwa na kauli mbili nzito zilizotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma kuwa, Zanzibar si nchi, huku Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Iddi Pandu Hassan, akipinga kauli ya Pinda na kusisitiza kuwa Zanzibar ni nchi. Kwenye suala la nchi, sina urafiki na mtu. Bunge la Jamhuri ya Muungano linasema Zanzibar si nchi, Baraza la Wawakilishi linasema Zanzibar ni nchi. Vyote hivyo ni vyombo vya kutunga sheria na viongozi waliotoa kauli hizo ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali zote ni za CCM. Hii ni hatari kubwa, na si jambo la kulifumbia macho hata kidogo, alisema Razza na kutoa msimamo kwamba Zanzibar ni nchi yenye mamlaka kamili.
Zanzibar ina rais, ina mahakama kuu, ina baraza la wawakilishi, ina serikali yake, ilishawahi kuwa na mabalozi nje ya nchi, kabla ya Muungano, ina bendera yake, ina wimbo wa taifa, wanapofika viongozi wa nje, wanapigiwa mizinga 21, kwenye sherehe za Muungano na zingine, Rais wa Jamhuri anaingia kabla ili kumpokea Rais wa Zanzibar, bado mnasema si nchi, iitweje? alihoji Razza.
Alisema ni makosa kuita Zanzibar sehemu ya Jamhuri ya Muungano na kutaja mfano wa baadhi ya mikoa kama Kilimanjaro, Arusha, Tanga na mingine kuwa nayo ni sehemu ya Jamhuri, lakini haiwezi kufananishwa na Zanzibar, kwa vile ni nchi kwani ina mamlaka na madaraka kamili ya kujiongoza.
Akirejea historia ya kuanzishwa kwa Serikali ya Muungano, Razza alisema wakati waasisi wake, Mwalimu Nyerere na Mzee Amani Abeid Karume walipoamua kuufanya Muungano, nchi zote zilikuwa na hadhi sawa bila kujali kwamba Zanzibar ilikuwa na watu wachache kuliko Tanganyika.
Turejee kwenye utamaduni, viongozi wetu Nyerere na Karume waliunganisha nchi mbili huru, zilizokuwa sawa, marais wao walikuwa sawa, iweje leo Zanzibar isiwe nchi? Basi kama si nchi basi tuambiwe tuiteje na rais wake aitwe nani? alisema Razza na kulazimika kunukuu sehemu ya katiba ambayo alidai inasema Zanzibar ni nchi.
Mfanyabiashara huyo mwenye ushawishi mkubwa wa siasa za Zanzibar, alirejea kesi ya uhaini ya baadhi ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao katika utetezi wao waliwasilisha hoja mahakamani kutaka waachiwe huru kwa madai kuwa, wasingeweza kufanya uhaini kwa vile Zanzibar si nchi, na mahakama ilikubali, lakini CCM tulipiga kelele kwa kudai Zanzibar ni nchi.
Kitu cha ajabu leo, CCM iliyokuwa inatetea kwamba Zanzibar ni nchi, inasema Zanzibar si nchi. Kwa hiyo CUF walikuwa sahihi na CCM ni waongo, hali hiyo si nzuri katika siasa za Zanzibar, alitahadharisha Razza.
Alisisitiza kuwa endapo mzozo huo utaachiwa, unaweza kuleta athari kubwa hasa visiwani Zanzibar ambako wananchi wamekuwa wakijadili kwa mtazamo tofauti hoja ya ama Zanzibar ni nchi au sehemu tu ya Jamhuri ya Muungano. Waswahili wanasema kila penye tumbo la shari, huzaa heri. Zanzibar wanaona Muungano ni mzigo, Bara wanaona Muungano ni mzigo.
Tunataka serikali tatu, lakini kama tutaambiwa tuwe na serikali moja, bora mtulipue kwa mizinga, ibaki miti tu, alisema Razza.
Mjadala wa Zanzibar ni nchi au la, uliibuka na kushika kasi baada ya Pinda kujibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim Issa (CCM), aliyetaka kujua iwapo Zanzibar ni nchi au la.Issa katika swali lake kwa Pinda, alibainisha kuwa Zanzibar imefikia hatua ya kuwa na rais wake, mihimili yake pamoja na wimbo wake wa taifa, kisha akashangaa Pinda anawezaje kusema Zanzibar si nchi!Mbunge huyo aliuliza swali hilo Juni 26, mwaka huu, siku kadhaa baada ya Pinda kunukuliwa akisema wakati akijumuisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake kuwa Zanzibar si nchi.Kauli na majibu hayo ya Pinda yaliibua mjadala mzito ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ambako hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Iddi Pandu Hassan, alisimama na kumpinga Pinda akisisitiza kuwa Zanzibar ni nchi.Mwanasheria huyo alisema Zanzibar, kama zilivyo nchi nyingine, ina mihimili mitatu ya utawala inayojumuisha Serikali, Mahakama na Baraza la Kutunga Sheria hivyo ni nchi.
TUNAOMBA MAWAZO YENU KWENYE HILI.