Naziona dalili za kuvunjika kwa Muungano wa Tanzania. Kuna matamshi kuwa Zanzibar imekuwa koloni la Tanganyika, mipaka ya Zanzibar ni maili kumi ndani ya Tanganyika mengine mengi. Kwa sasa Zanzibar wanayo katiba yao, bendera yao, wimbo wao wa taifa na wanasema Zanzibar ni nchi kamili. Rais wa SMZ anapigiwa mizinga 21 katika sikukuu za SMZ. Kama Rais wa Jamhuri yupo anakuwa kama Rais mgeni mualikwa toka nchi ya kigeni ilhali yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania.
Sishangai Rais John Magufuli akiacha kushiriki sherehe hizo. Ninachofikiri ni kuwa tunapaswa tuuanze upya huu muungano. Kama upo uhalali wa kuwepo SMZ ndani ya muungano ni vyema kukawa na uhalali huo huo wa kuwepo serikali ya Tanganyika ndani ya muungano iliyo na katiba yake, wimbo wake wa taifa, bendera yake na kiongozi wake anaye pigiwa mizinga 21 katika sikukuu za nchi yake. Vinginevyo kiuhalisia muungano mimi siuoni labda huu unaolindwa na jeshi.