- Source #1
- View Source #1
- Source #2
- View Source #2
Tangu zamani nasikia stori za mwanamke akifanya mapenzi kwa mara ya kwanza (kutolewa bikra kama wanavyoita) lazima atoke damu. Japo kumekuwa na baadhi ya wanawake wanasema hawakuwahi kutokwa damu, hii imekaaje?
Je, ni kweli mwanamke akitolewa bikra lazima atoke damu? Na kama ndiyo hao wanaodai hawajatoka wanakuwa wanadanganya?
- Tunachokijua
- Bikira nini?
Bikira ni mtu yoyote wa kike au kiume ambaye hajawahi kufanya ngono. Hii ikiwa inamaanisha kwamba uume wa mwanaume haujwahi kuingia kwenye uke wa mwanamke wala mwanamke hajawahi kuingiliwa na uume wa mwanamke.
Japo ngono zipo za aina nyingi kama ngono ya mdomo nk ila hapa tunajikita kwenye ngono inayohusisha uume kuingia ukeni.
Ifahamike kwamba Neno bikira huweza kumaanisha tofauti na ngono wakati mwingine, kwa mfano neno bikira huweza kutumika kumaanisha mtu ambaye hajawahi kufanya kitu fulani( hujawahi kunywa pombe, ni bikira wa pombe), Ardhi haijawahi kuguswa kwa matumizi yoyote ardhi hiyo huweza kuitwa bikira.
Mtoto wa kike anapozaliwa kabla hajafanya ngono huwaje?
Baadhi ya watoto wa kike wanapozaliwa uke huwa na kizinda, ni baadhi kwa kuwa si wote huzaliwa na kizinda hicho.
Kizinda ni nini?
Kizinda ni kipande kidogo, chembamba cha tishu kwenye mlango wa uke. Inaundwa na vipande vya tishu vilivyobaki kutoka kwa ukuaji wa fetasi. Ukubwa, umbo na unene wa kizinda ni cha kipekee kwa kila mtu na kinaweza kubadilika kwa wakati.
Mtoto wa kike anapozaliwa, kizinda huwa ni kipande cha tishu chenye umbo la pete ambacho huzunguka uwazi wa uke. Nyakati nyingine hufunika sehemu ya chini ya uwazi wa uke. Katika hali nadra, kizinda hufunika uwazi wako wote wa uke na husababisha matatizo na hedhi. Tofauti na tishu nyingine kuwa na kazi maalum, kizinda hakina kazi maalum ya kufanya.
Hata ivyo pamoja na uwepo wa tishu hiyo lakini uke hubaki na eneo kubwa la wazi ambapo huweza kupitisha Damu ya hedhi
Je Mwanamke anaposhiriki ngono mara ya kwanza lazima atoke damu?
Kuna hadithi iliyoenea kwamba kila mwanamke anayeshiriki ngono kwa mara ya kwanza huvuja damu na kuhisi maumivu pindi uume unapoingia ukeni.
Ni kawaida na imezoeleka kutokwa na damu mara ya kwanza unapofanya ngono, lakini si lazima mwanamke kutokwa na damu au kuhisi maumivu anapofanya ngono kwa mara ya kwanza na wapo wanawake wengi hawavuji damu hata kidogo na hii haimaanishi hawakuwa bikira.
Kwa nini wanawake wengine hutokwa damu na wengine hawatokwi na damu wanapofanya ngono mara ya kwanza?
Watu mara nyingi huamini kuwa kufanya ngono "hupasua" kizinda, na kusababisha kufunguka na kutokwa na damu lakini hii si kweli. Kizinda huwa tayari kina tundu au hakipo kwa baadhi ya watu wakati wanapofanya ngono kwa mara ya kwanza. Fikiria Je, damu ya hedhi ingetokaje iwapo kizinda kimeziba?
Wanawake wengine hutokwa na damu kwa sababu ya kupenya kwa nguvu kwa uume kunararua tishu nyembamba (kizinda) na ivyo kusababisha damu kutoka, na wengine ni nguvu kubwa inayotumika kuweza kumuingilia (purukushani) ivyo kusababisha kupata majeraha ukeni yanayosababisha damu kutoka. Wingi wa damu hutegemea uimara wa tishu na nguvu iliyotumika kuingia ukeni. Kizinda ni utando karibu na mlango wa uke.
Hata ivyo wanawake wasiotokwa damu husababishwa na Utayari wao kufanya ngono hufanya uke kuwa na majimaji ambapo uume hupita bila kusababisha jeraha wala kizinda kuraruriwa kwa kasi na ivyo kusababisha damu.
Pia uume kuingia ukeni taratibu kwenye uke uliotayari kuingiliwa mwanamke hawezi kutokwa damu au akaja kuona kama alama ya damu kwenye nguo yake ya ndani baadaye sana baada ya tendo la ngono.
Lakini yawezekana kizinda kilishatoka chenyewe kutokana na sababu mbalimbali kama michezo, kuendesha baiskeli au kuingiliwa na kitu ukeni kama baadhi ya vipimo vya hospital
JamiiForums, imepitia na kusoma makala nyingi mbalimbali ikiwepo na tafiti za kitaalamu na kujiridhisha kuwa, si kila mwanamke huweza kutokwa na damu anapofanya ngono kwa mara ya kwanza, japo haindoi ukweli kuwa wapo wanawake hutokwa damu kama ilivyoelezwa kwenye mada hii.
Kwamba kutokwa damu si tafsiri ya mwanamke kuwa bikira kwa kuwa kizinda kimeshindwa kuwa kielelezo sahihi cha ubikira na anaweza kutokwa damu kwa kuwa aliingiliwa kwa nguvu na anaweza asitokwe damu kwa kuwa aliandaliwa na kuwa tayari kwa ngono. Ivyo kutokutokwa damu hakumaanishi mwanamke hakuwa bikira.