Kile kinachoendelea Mwanza si hitilafu ya kawaida, bali ni
aibu ya wazi, uzembe wa makusudi na kutowajibika kwa kiwango cha juu kabisa kutoka MWAUWASA. Mwezi mzima uliopita Nyegezi haikuwa na tone la maji. Hakuna taarifa, hakuna maelezo, hakuna uwajibikaji—mpaka wananchi walipopiga kelele ndipo maelezo ya kubuni yakatolewa.
Walisema chanzo cha Butimba kilipata hitilafu. Wakaahidi mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa
tatizo halitarudia tena.
Lakini sasa, mwezi huu mzima wa kumi na moja,
Nyegezi IMEKAA BILA MAJI TENA, na MWAUWASA inajifanya haioni, haisikii, wala haitoi taarifa. Huu ni
udharau wa kiwango cha juu dhidi ya wananchi wake.
Ukweli mchungu ambao wanaficha ni kwamba
chanzo cha maji kimetoboka tena, kimeharibika tena, na mfumo mzima wa usambazaji maji Mwanza ni dhaifu kupita maelezo. Wanajua, lakini hawasemi.
Wananchi hawajui kinachoendelea, na MWAUWASA
imejigeuza taasisi isiyowajibika wala kuheshimu wateja.
Udhaifu umefika pabaya kiasi kwamba walimualika Mheshimiwa Rais kuja kuzindua chanzo cha maji ambacho wao wenyewe wanajua
hakikai hata miezi kadhaa bila kuharibika. Huu ni
udanganyifu wa kitaasisi. Ni kujipiga picha mbele ya Rais wakati ukweli halisi ni kwamba Mwanza haina mfumo wa maji wa kueleweka.
Kichekesho kilichogeuka machozi ni kwamba
mikoa jirani inapata maji kutoka Mwanza, lakini Mwanza yenyewe haina maji.
Huu si uzembe tu—ni
udhalilishaji wa wananchi. Ni ishara ya wazi kuwa kuna watu wanatumia mgogoro huu kama
mradi binafsi wa kuuza maji kwa magari huku wananchi wakiteseka.
Wakazi wa Mwanza tumechoka:
- Tumechoka kunywa maji kwa taabu kwenye jiji linalojiita la kimkakati.
- Tumechoka kuambiwa uongo kila siku.
- Tumechoka ahadi za kila baada ya miezi miwili huku maji yakikatwa kwa mwezi mzima.
- Tumechoka taasisi inayoshindwa kazi yake ya msingi—kutoa maji.
MWAUWASA lazima ijibu maswali haya:
- Kwanini tatizo linaendelea kujirudia?
- Kwanini hakuna taarifa kwa wananchi?
- Kwanini chanzo kipya cha maji hakidumu?
- Kwanini mikoa jirani inapata maji lakini Mwanza haina?
- NANI ananufaika na mgogoro huu?
Ni wakati uongozi wa MWAUWASA
uwajibike, utoe taarifa rasmi, urejeshe huduma, na kuweka mpango wa dharura wa
uhakika—si longolongo na ahadi zisizotekelezeka.
Mwanza si jiji la kuendeleza miradi ya watu wachache.
Wananchi tunataka maji. Sasa. Sio kesho.