MWAUWASA: Ujenzi wa matanki ya Maji kwa Wananchi umeanza ili maeneo ya milimani yapate maji kwa uwiano sahihi

MWAUWASA: Ujenzi wa matanki ya Maji kwa Wananchi umeanza ili maeneo ya milimani yapate maji kwa uwiano sahihi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
3,984
Reaction score
13,760
Baada ya hoja za Wanachama kadhaa wa JamiiForums.com kuelezea kuhusu changamoto ya huduma ya maji katika baadhi ya maeneo Jijini Mwanza, ufafanuzi umetolewa na Mamlaka husika...

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) inaendelea na utekelezaji wa Miradi mbalimbali inayolenga kutatua changamoto ya usambazaji wa maji katika Jiji la Mwanza na viunga vyake.

Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Mradi wa Chanzo cha Maji cha Butimba kilichoongeza kiwango cha uzalishaji maji kwa kiasi cha Lita Milioni 48 kwa siku, sasa kazi kubwa inayoendelea ni utekelezaji wa mpango wa usambazaji maji.

Hivi sasa, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Matenki ya kuhifadhi na kusambaza maji kwa Wananchi umeanza kutekelezwa kwa kasi ili kuwezesha maeneo ya milimani yanapata maji kwa uwiano sahihi.

Matenki hayo yatajengwa katika maeneo ya milima inayozunguka Mji wa Mwanza ikiwemo Nyamazobe (lita milioni 5), Buhongwa (Lita milioni 10), Fumagila (Lita milioni 10) na Usagara (lita milioni 1) na Kisesa (lita milioni 5).

Aidha Utekelezaji wa mradi huu wa thamani ya Tsh. Bilioni 49 umeanza na unatarajiwa kukamilika kwa awamu, ndani ya miaka miwili ifikapo Desemba 2026.

Wakati miradi mikubwa ikiendelea kutekelezwa, Wizara ya Maji kupitia MWAUWASA imeendelea na utekelezaji wa Miradi inayoleta matokeo ya haraka ili kuimarisha upatikanaji wa huduma katika maeneo mbalimbali.

Miradi hii inafadhiliwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa lengo la kuimarisha huduma. Moja ya Miradi hiyo na ambao umeleta ahueni kubwa ni mradi wa dharura wa Sahwa - Buhongwa ambao tayari umekamilika na umeendelea kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo la Sahwa, Lwanhima na Buhongwa.

Mradi mwingine unaotekelezwa hivi sasa pia kupitia Wizara ya Maji ni wa ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji wa thamani ya TSH. Bilioni 1.8 ambao unalenga kuondoa mabomba chakavu yaliyopo na kuboresha mtandao katika maeneo ya Buhongwa, Mkolani na sehemu ya Luchelele. Mradi huu umeanza utekelezaji eneo la Luchelele.

Mradi mwingine unaotarajiwa kutekelezwa mara baada ya taratibu za kifedha kukamilika utahusisha Kishiri, Igoma na maeneo jirani. Mradi huu utatekelezwa kupitia mkopo wa masharti nafuu unaotarajia kutolewa na Mfuko wa Taifa wa Maji na Benki ya TIB ukihusisha ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji na kunufaisha wakazi wa kata za Kishiri, Igoma na Nyamhongolo.

Miradi hiyo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuhakikisha kuwa jiji la Mwanza linakuwa na huduma bora ya usambazaji maji.

Miradi kama hiyo pia inaendelea katika Wilaya ya Ilemela, na miji ya Misungwi, Magu.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano
MWAUWASA

Pia soma
~
Kero: Kuna shida kubwa sana ya maji jiji la Mwanza (Nyamagana)mitaa ya Igoma, Machinjioni, kwa Kibeshi, Mhandu
~ Mwanza: Wakazi wa Buhongwa hatuna maji ya uhakika, hufunguliwa usiku wa manane
 
Back
Top Bottom