Huo ndiyo ukweli, tena wa heri. Rais na Mwenyekiti wangu wa CCM Taifa Dr. John P. Magufuli leo 'amenyakua' fomu ya 'kuchukua' tena Urais kupitia CCM. Kila mtanzania anajua kuwa tayari Dr. Magufuli 'ameshapitishwa' kimaneno na kivitendo kuwa mgombea Urais wa CCM kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Hata TLP ya Mrema imempitisha. Leo hakuchukua fomu ya kuomba kugombea.
Angekuwa amechukua, kama ilivyo kwa watani zetu CHADEMA, basi makada wengine wa CCM wangejitokeza na kuchukua. Wenye sifa za Urais ndani ya CCM wamejaa tele kuliko mchele. Lakini, hakuna mwenye uthubutu hata kiduchu wa kuja hapa Makao Makuu ya CCM Dodoma kuchukua fomu. Ni kama fomu ya kugombea Urais ndani ya CCM ilichapishwa moja tu kwa ajili ya Dr. Magufuli. CCM tumekubali utaratibu umeze matakwa ya Katiba na Kanuni zetu za CCM.
Maneno na matendo ya watoa-fomu yanakataza kusogelea chumba cha kuchukulia fomu. Macho yao yanaogopesha makada kujitokeza na kuomba fomu za Urais. Ilipaswa Dr. Magufuli aanze kupimwa ndani ya chama kuhusu kukubalika kwake. Angepimwa na makada wengine juu ya kwanini yeye apewe bendera ya CCM uchaguzini katika nafasi ya Urais. Angepita au kutopita kidemokrasia. Haipo hivyo. Haikuwa hivyo. Haitakuwa hivyo.
Kwanini tushupalie demokrasia kwa watani zetu (vyama vya upinzani) huku demokrasia chamani mwetu ikiminywa? Nani tunamtapeli ikiwa ukweli ni kuwa hautakiwi upinzani ndani ya CCM kwa nafasi ya Urais?
Uchaguzi huu utaingia kwenye maajabu ya dunia!
Mzee Tupatupa wa Lumumba, Dodoma