Nianze kutoa pole kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA,Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho kwa kifo cha Alphonse Mawazo,aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wa mkoa wa Geita. Pole pia nazitoa kwa familia,ndugu na jamaa wa marehemu. Namuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Kamanda Mawazo mahali pema peponi, Amina.
Nakwepa kuzungumzia namna na mahali kilipotokea na kilivyotokea kifo cha Mawazo kwakuwa hayo ni mambo ya vyombo vya dola. Najielekeza moja kwa moja kwenye hoja yangu. Nikiri mapema kuwa namfahamu Hayati Mawazo kwa kiasi kidogo sana.
Kadiri ninavyojua,Hayati Mawazo alihama vyama viwili. Alihama TLP kuhamia CCM na baadaye akahama CCM kwenda CHADEMA. Alipokuwa CCM,Hayati Mawazo alifanikiwa kugombea na kushinda Udiwani wa Kata ya Sombetini kule Arusha Mjini.
Alihamia CHADEMA akiwa bado Diwani wa Sombetini na kusababisha uchaguzi mdogo uliowapa CHADEMA ushindi. Hayati Mawazo alihama vyama akihama na fikra zake alizozisimamia hadi kifo chake.
Hayati Mawazo alitamani na kusimamia demokrasia Tanzania.Alikuwa na ushawishi kwa ujenzi wa hoja alipokuwa vyama vyote vitatu. Alitamani na kusimamia ubishani wa kujenga hoja za kuimarisha demokrasia. Ndiyo maana hakuchoka kushiriki kutangaza na kuimarisha vyama vyake. Kila chama kilichomkosa kiliathirika. Hata CHADEMA itaathirika ingawa fikra zake zitaendelezwa. Demokrasia ni watu kusikia,kujua na kupambanua. Hayati Mawazo aliyafanya hayo yote.
Pia,Hayati Mawazo alikuwa na fikra za kuleta maendeleo kwa watu na uthubutu. Katika kuyasimamia hayo,alikuwa Diwani wa Sombetini na hata kugombea Ubunge huko Busanda mwaka huu. Kama kijana,amekuwa mfano wa kuthubutu na kufanya.
RIP Hayati Alphonse Mawazo