Nyuma ya mtoto aliye imara kuna mzazi aliyepambana kimyakimya.
Naona wazazi ni watu wanaotakiwa kuheshimiwa sana. Si kwa sababu tu wanatulea, bali kwa sababu ya uzito wa jukumu walilobeba tangu siku ya kwanza tulipoingia duniani. Uzazi sio tu tendo la kuleta kiumbe hai, bali ni safari ya maisha inayojaa sadaka, upendo usio na masharti, na maumivu yasiyoonyeshwa hadharani.
Ukiwa mzazi unakua na ule upendo ulioandikwa kwenye biblia UPENDO WA AGAPE ule usiochoka, usiotegemea malipo, na usiohitaji sababu. Ni upendo unaokusukuma kukesha usiku mzima mtoto akilia, kukubali kula chakula kilichopoa kwa sababu mtoto alihitaji kushiba kwanza. Ni upendo unaosamehe bila kusema, hata pale mtoto anapokosea kwa makusudi.
Mtoto hata akikosea, baada ya muda mzazi anasahau na kumsamehe hata asipoomba msamaha.
Unajikuta bado unamtafutia maisha bora, unamkubali, unampenda.
Mzazi anapotazama macho ya mtoto wake, anaona wajibu. Ushamleta mtu duniani; unakua na moyo wa kuhakikisha yupo salama kiakili, kimwili apate mahitaji yote. Lakini hiyo siyo mwisho. Bado uhakikishe anakua mtu mwema kwenye jamii. Kama ni mvulana, aje kuwa mwanaume kamili mwenye maadili, heshima, upendo na kujitegemea.
Kama ni msichana, aje kuwa mwanamke kamili mwenye utu, heshima, upendo na kujitambua.
Bado uhakikishe anakua imara kupambana na changamoto za dunia hii.
Ni majukumu mengi, ya kimwili na ya kiroho. Na mara nyingi, mzazi huyafanya yote haya kwa kimya.
Hakuna anayejua kilio cha usiku, hofu ya kesho, na maumivu ya kuona mtoto wako akiteseka.
Ila sasa naona wazazi hua wanapitia mawazo ya kimyakimya. Haya ni mawazo yanayokuja kimya kimya, yakitafuna nafsi kama
"je nitamlea vema? Nitamfikisha alikokusudiwa? Atanielewa? Atanikumbuka?
Siku zote mzazi hutaka mema tu kwa mtoto wake. Unamtunza,
Unamsihi,
Unamwombea.
Lakini kuna wakati anachagua njia tofauti, au dunia inambadilisha. Na hapo ndipo mzazi huumia sana. Maumivu ya mzazi hayapimwi kwa macho ni maumivu ya ndani ya moyo, ya nafsi. Lakini bado yuko tayari kumpokea, kumsamehe, kumpa nafasi ya pili.
Kwa kweli, mzazi ni kiumbe wa kipekee. Anabeba uzito mkubwa moyoni, lakini anaonesha tabasamu usoni. Anapambana kwa ajili ya mtu mwingine kila siku, bila malipo ya moja kwa moja. Na ndiyo maana, mzazi anastahili siyo tu heshima bali shukrani ya maisha yote.
Kwa hiyo, tukumbuke kuwasikiliza wazazi, Kuwaheshimu na Kuwapenda.