Hata kumuita Malik pia yafaa sababu Malik maana yake ni "Mfalme" na wafalme wanaadamu wapo. Kisichofaa ni kujiita au kumuita mwengine "Mfalme wa Wafalme". Sababu Mfalme wa Wafalme ni Allah tu.
Soma zaidi maelezo yafuatayo nimeyatoa Alhidaaya.com;
Ama Kuhusu swali lako ni kwamba mzazi au mlezi anafaa kujiepusha kumpatia mtoto wake jina ambalo ni maalum kwa Allaah. Haifai kumuita mtoto kwa jina kama la Al-Ahad (Mmoja pekee), Asw-Swamad (Mwenye kukusudiwa kwa haja zote), Al-Khaaliq (Muumbaji), Ar-Razzaaq (Mwenye kuruzuku) na kadhalika.
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimbadilisha mtu aliyesilimu aliyekuwa akiitwa Abul-Hakam (baba wa Hukumu) akimwambia kuwa Allaah Pekee Ndiye Mwenye sifa hiyo ya Al-Hakam, na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza kama ana watoto na majina yao, yule mtu akataja wanawe watatu, Shurayh, Muslim na 'Abdullaah. Basi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Kuanzia leo wewe ni Abuu Shurayh.” [Abu Daawuwd].
Kadhalika Abuu Hurayrah alikuwa akiitwa 'Abdush-Shams (Mja wa jua) lakini alipoingia Uislamu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimbadilisha jina lakena kumuita 'Abdur-Rahmaan.
Hata hivyo, yapo majina mengine ambayo ni sifa ya Allaah ('Azza wa Jalla) na pia ya wana Aadam kama vile Maalik (mfalme). Kwa hiyo, kumuita mtoto jina hilo hakuna tatizo. Mbali na hayo ni vyema kuwaita watoto majina ya Allaah kwa kufuatanisha na 'Abd (mja). Kwa mfano majina hayo yatakuwa kama 'Abdu-Allaah, 'Abdur-Rahmaan, 'Abdul-Fattaah, 'Abdur-Razzaaq, 'Abdus-Salaam na kadhalika.
Kuhusu swali la pili, ni kwamba haifai kabisa mtu kuitwa 'Abdur-Rasuwl (Mja wa Rasuli), au 'Abdun-Nabbiy (Mja wa Nabbiy, au 'Abdul-Husayn (Mja wa Husayn). Majina haya utayakuta sana kwa Mashia na watu kutoka Asia.
Hakika majina kama hayo hayafai na ni makosa makubwa, kwani uja na utumwa ni wa Allaah Pekee na si wa kiumbe yeyote.
Hao wote kama Rasuli au Al-Hussayn ni waja wa Allaah na watumwa wake na ni wana Aadam na hawawezi katu kuwa waumba au waabudiwa. Hata ikiwa mtu hajakusudia kuwafanya ni waabudiwa au waumba, vilevile ni makosa na haifai.
Majina yapo mengi mazuri na yenye maana nzuri nzuri. Allaah Ana majina mengi ambayo mtu anaweza kuyatumia kwa uja wake na hakuna haja ya kuwatuza viumbe hadi kujipa uja kwao.
Hayo ni matatizo pia yanayosababishwa na ghuluww za watu wanaotukuza maimamu wao hadi kuwapeleka katika daraja ya uungu. Ni hatari kubwa sana kwa mja kuingia katika balaa hilo la kumpeleke katika ushirikina kwa kujua au kutokujua.
Na ikiwa mtu alipewa jina katika majina hayo yasiyofaa na wazazi wake, basi anapaswa kwenda kubadilisha jina hilo hata kama ameshafikia umri mkubwa ili ajiepushe na shirki.
Uislamu unamruhusu mtu kubadili jina lolote baya hata ikiwa kapewa na wazazi wake. Tuchukue mfano wa matukio tuliyotaja juu ya Maswahaba kubadilishwa majina yao na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Na Allaah Anajua zaidi