Naona maneno mengi yanayotajwa na wadau ni yale yanayoangukia katika sayansi na teknolojia. Haya kupata tafsiri ya moja kwa moja ni vigumu ndiyo maana mara nyingi inabidi yatoholewe kama yalivyo. Hata lugha zingine zimepitia shida hiyo na siyo Kiswahili pekee. Kiingereza, kwa mfano, kimechukua maneno mengi katika tanzu hizi kutoka katika Kilatini na Kigiriki (cha kale); na kuyakopa kama yalivyo. Ndiyo maana misamiati kama ya kwenye taaluma za udaktari na uhandisi, kwa mfano, ni migumu kweli kweli. Ingependeza kama mjadala ungejikita katika maneno ya kawaida; na yanayotumiwa na watu wa kawaida mtaani katika mazingira yasiyo rasmi (mf. Katika elimu)
Kwa hapa Tanzania BAKITA ndiyo wenye jukumu la kuunda hizi istilali za maneno mapya katika Kiswahili na huchapisha vitini au vikamusi mara kwa mara katika tanzu mbalimbali zikiwemo zile za sayansi na teknolojia. Tatizo hata hivyo ni kwamba lugha ni mali ya wanajamii; na jamii ndiyo huamua neno gani litumike. Ni kwa sababu hii misamiati mingi inayopendekezwa na BAKITA wamebaki nayo huko huko BAKITA makabatini kwao wakati mtaani jamii inatumia maneno inayotaka. Na hakuna juhudi zo zote za makusudi hata katika mazingira rasmi (mf. kwenye vyombo vya habari na mashuleni) kuhakikisha kuwa maneno rasmi yaliyopendekezwa na BAKITA yanatumika ili yazoeleke. BAKITA, kwa mfano, walipendekeza kompyuta iitwe tarakilishi (mashine yenye akili na yenye uwezo wa kukokotoa tarakimu) lakini mtaani neno kompyuta limeshika na BAKITA hawana la kufanya maana lugha ni mali ya jamii. Baobonye - keyboard, ugiligili - liquid...n.k.
Kuhusu utohoaji wa maneno BAKITA huzingatia misingi kadhaa; na hawatafsiri tu kiholela.
1. Huangalia katika lahaja zingine za Kiswahili kama wanaweza kupata neno linaloshabihiana kimaana/kidhana na neno jipya. Lipo dai kwamba Kiswahili ni lugha tajiri sana na hakukuwa na sababu ya kukopa maneno mengi kutoka katika Kiarabu (na Kiingereza) kwa sababu karibu kila neno la mkopo linaweza kupatiwa tafsiri yenye asili ya Kibantu kama tungechimbua kwenye lahaja zingine za Kiswahili hasa zile za muda mrefu mf. Kimvita. Hawa huwa wanahoji ni kwa nini lahaja ya Kiunguja iliteuliwa kuwa lahaja teule wakati ni lahaja ambayo tayari ilikuwa "imeshaharibiwa" sana na Kiarabu. Kama lahaja za kale kama Kimvita zingeteuliwa kuwa msingi wa usanifishaji, Kiswahili cha sasa kisingekuwa na maneno mengi ya Kiarabu, maneno ambayo mengi yamekopwa na kusanifishwa bila sababu za msingi maana kuna maneno shabihi katika lahaja zingine za Kiswahili. Pengine kulikuwa na njama za makusudi "kukiharibu" Kiswahili kwa "kukiarabisha" na "kukiingerezesha". Kumbuka kwamba mchakato wa kukisanifisha Kiswahili ulisimamiwa na Waingereza!😳
2. Tukikosa neno katika lahaja za Kiswahili basi tuangalie katika lugha zingine za Kibantu. Hapa ndiyo tunapata maneno kama ikulu (Kinyamwezi), shiganga (Boulder-Kisukuma) n.k.
3. Tukikosa katika lugha za Kibantu basi tuangalie katika lugha zingine za Kiafrika ambazo si za Kibantu
4. Wakati mwingine inabidi kuangalia dhana ya kitu tunachojaribu kutohoa (mfano wa kompyuta hapo juu - tarakilishi - ma
shine yenye a
kili inayokokotoa
tarakimu).
5. Kutohoa maneno kama yalivyo. Hii ndiyo njia inayopendwa na jamii na tayari maneno mengi yameshazoeleka kama yalivyo (bicycle - baisikeli, radio - redio, helicopter-helikopita). BAKITA hujaribu kupendekeza maneno mapya lakini jamii inakuwa imeshatohoa moja kwa moja maneno na mapendekezo yao mengi huwa hayashiki.
Pia kuna hatua zingine za kuzingatia katika utohoaji wa maneno mbali na huu mwongozo wa jumla wa ukopaji wa maneno.
Kiswahili ni lugha inayokua na itaendelea kukopa hasa katika hii misamiati ya kisayansi na kiteknolojia. Hili ni jambo la kawaida maana lugha zote zimepita huko. Japo tuna BAKITA lakini mwamuzi hasa wa lugha ni jamii yenyewe.
View attachment 3028238