Nape ni aina ya mwanasiasa ambaye mimi binafsi hunivutia mara chache sana; akiwa na madaraka hujisahau kirahisi na kuwa jeuri. Akiwa nje ya madaraka hujitambua na kuwa mnyenyekevu. Pamoja na huo udhaifu kwa hili analolalamikiwa kuwa anamsema vibaya marehemu namuelewa; anayo sababu ya kutosha kufanya hivyo. Anayesemwa na Nape pamoja na raia wengine wengi siyo marehemu wa kawaida tu; huyu ni marehemu aliyeaminiwa na kukabidhiwa mamlaka ya umma. Nape alindwe na aachwe atumie uhuru wake kwa kuyasema yote ambayo hakuyapenda; wenye mazuri ya kuyasema nao wafanye hivyo hivyo! Hii ndiyo njia pekee ya yeye Nape kujifaraji nafsi yake na kujipunguzia machungu ya ule udhalilishaji wa kutembezwa kwa miguu mbele ya kamera kwenda mbele ya "mtukufu" kufanya toba na kuomba msahamaha wa dhambi.
Akiwa kiongozi wa kuchaguliwa na watu, kibinadamu siyo jambo rahisi yeye Nape binafsi pamoja na wananchi waliomwamini na kumchagua kusahau na kusamehe huo udhalilishaji aliofanyiwa. Mambo mengine ni ya kishetani na hayasahauliki wala kusameheka; kutaka kufanya hivyo kirahisi ni sawa sawa na kufungamana na shetani na kazi zake zote na mambo yake. Nchi hii inahitaji kuweka utaratibu wa kitaifa wa kutafakari, kutubu na kuomba msamaha kwa uovu wote wa kipindi kile cha giza. Hili siyo jambo la kuwataka watu mmoja mmoja wanaotoa hisia zao za maumivu hadharani kunyamaza kwa sababu tu aliyewaumiza kwa kutumia mamlaka ya umma amefariki. Isitoshe, mamlaka hayo yaliyotumika kuumiza raia sasa yamekabidhiwa mtu mwingine! Kwani kuna tatizo gani kama mamlaka hayo yakitumika sasa kwa hekima kuwaomba radhi raia ambao wameumizwa kwa matumizu mabaya ya hayo mamlaka?