Mwezi Juni mwaka 2019 palizuka mjadala mkubwa sana kuhusu mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo-Bagamoyo Special Economic Zone (SEZ) ambao Wachina walitaka kuwekeza pale Bagamoyo zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 10 (Trilioni 23) ambazo zingetolewa na Wachina kwa zaidi ya asilimia 90. Wengi waliitaka Serikali kukubali na kuchukua maamuzi ya kuingia makubaliano ya kutekeleza mradi huo haraka iwezekanavyo.
Moja ya watu waliounga mkono na kupigia chapuo mno ujenzi wa Bandari hiyo kwa kutaja sifa kedekede za mradi huo alikuwa ni Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai ambaye alinukuliwa Bungeni akishangaa kwanini Serikali inashindwa kufanya maamuzi ya ujenzi wa Bandari hiyo ambao ungegharamiwa na Wachina kwa kiwango kikubwa huku ikiwa Bandari kubwa zaidi ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Bwana Ndugai anasema alikwenda China na kukutana na hilo kampuni ambalo lilipanga kujenga hiyo Bandari ambapo anasema alichoambiwa na hao jamaa na namna mradi huo ulivyokuwa na faida nyingi alishangaa kwanini Serikali ilikuwa inajivuta kufanya maamuzi ya ujenzi wa Bandari hiyo.
Siku chache baada ya Ndugai kupigia chapuo mradi huo, Rais Magufuli wakati huo aliibuka na kutaja mambo ya ajabu ajabu na hovyo ambayo alinukuliwa kuwa ni kichaa tu ndiye angeweza kukubali yaliyowekwa na hao Wachina kama masharti ya uwekezaji wa ujenzi wa Bandari hiyo. Masharti hayo yalikuwa ni, kwa miaka 33 hakuna TRA kufika hapo kukusanya kodi, baada ya kuanza mradi huo, nchi yetu isingeruhusiwa kuendeleza Bandari yoyote nchi nzima, kuwapa ardhi yetu na kuwapa guarantee ya miaka 99 bila ya kuwauliza chochote, kuwapa fidia ya kuchimba Bandari hiyo na mengine mengi ambayo yaliwashangaza wengi sana.
Baada ya Rais Magufuli kueleza masharti magumu ya mradi huo wa Bandari ya Bagamoyo, mjadala wote wa ujenzi wa Bandari hiyo ulikufa na hakuna aliyepata hamu tena ya kusikia ukijengwa hasa kwa namna ulivyokuwa na masharti magumu na ya ukichaa.
Sasa siku chache baada ya kifo cha Rais Magufuli, Bwana Ndugai ameibuka tena Bungeni na hoja hiyo ya ujenzi wa Bandari hiyo huku akiendelea kuupigia chapuo mradi huo na zaidi akisema Rais Magufuli alidanganywa na wasaidizi wake na kwamba masharti aliyoyataja wala hayakuwa ya kweli na mengi alishauriwa vibaya na wasaidizi wake.
Hoja hii ya Ndugai kudai kwamba Rais alidanganywa na wasaidizi wake kuhusu masharti yale magumu waliyotoa Wachina inazua maswali mengine mengi ya msingi. Kama Rais alidanganywa, kwanini yeye Ndugai kipindi kile kile asingemuomba Rais na kwenda kusahihisha hapo anaposema Rais alidanganywa? Kwanini asubili Rais amefariki ndipo aibuke kutaka mradi uendelee kisa Rais alidanganywa?
Zaidi Bwana Ndugai anapigia debe mradi huo kwa kile anachosema fedha karibu zote za mradi zitatolewa na Wachina huku akisema Wachina walimwambia wanatushangaa kwanini hatuchukui maamuzi ya ujenzi wa mradi huo sasa na haraka kabla ya hao Wachina hawajastaafu kwenye hiyo kampuni. Kwa lugha rahisi Ndugai anashinikiza mradi huu ufanyike haraka kana kwamba yeye kuna kitu kinakwama mradi usipofanyika. Unaweza kudhani ni kama Ndugai amepewa chochote kitu na Wachina kuhakikisha mradi huu unatekelezwa na usipotekelezwa yeye mission yake inakufa.
Mimi namshangaa zaidi yeye, hivi ni toka lini Mataifa haya yakaweka fedha zao Mabilioni mengi hivi kama hawajaona faida yao? Ndugai anataka kusema mradi huu una manufaa sana kwetu kuliko wao? Kwamba Wachina wanaona tunakosa faida sisi kuliko wao? Well!
USHAURI WANGU KWA SERIKALI KUHUSU MRADI HUU
Kwanza, mpaka sasa Serikali imeweka fedha nyingi sana kwenye uboreshaji wa Bandari zetu kuu 3 za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga na karibu Bandari zingine zote nchi nzima kwahiyo mradi huu sio mgeni au kwamba hatuna kabisa kiasi cha kwamba tunahitaji sana huo, nchi hii ni moja ya Mataifa machache duniani imebarikiwa Bandari nyingi na za kutosha sana kwahiyo hatuna haja ya kukurupukia kitu kama vile hatunacho kabisa wakati tunacho. Tunahitaji kujiridhisha.
Binafsi natamani sana kila eneo lililopitiwa na bahari liwe na Bandari kubwa na ya kisasa ili kuinua uchumi wa nchi yetu na watu wa maeneo hayo lakini tunahitaji umakini mkubwa sana kuingia mikataba hii mikubwa (grand project) ya matrilioni mengi mno. Sipingi mradi huu mkubwa wa uwekezaji wa Bandari kwa ukanda wa Bagamoyo lakini tunahitaji umakini sana kwani tunafahamu makampuni makubwa kama haya hayawezi kuweka hela nyingi kiasi hiki sehemu kama hawajaona faida na interests zao zaidi.
Serikali sasa inatekeleza miradi mikubwa ya ukarabati na uboreshaji wa Bandari zetu zote kuu za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na zote za maziwa yetu Makuu pale Victoria, Tanganyika, Nyasa na nyingine nyingi. Matrilioni mengi yamewekwa kuboresha Bandari zetu, kwangu ni bora Serikali iendeleze zaidi hizi zilizopo ambazo tuko nazo na umiliki wote kuliko kuingia ubia na mikataba hii mikubwa na haya makampuni ambayo tunajua mengi yamekuwa yakiangalia zaidi faida zao wao kuliko zetu
Kama tunataka kuingia hii mikataba ya grand project kubwa namna hii basi mikataba yake iwe wazi na ikaguliwe kwa umakini kwa kila kipengele na iwe kweli yenye manufaa kwetu kama nchi na sio kuingia mkenge wa mikataba mibovu itakayogharimu vizazi vyetu na vijavyo huko mbele.
Tusiingie mkenge wa kutekeleza hii miradi kwa msukumo wa mtu au watu fulani ambao inawezekana wana interests binafsi kwenye miradi hii. Ndio maana nasema Bwana Ndugai asitake kutupeleka jalalani na kutuingiza mkenge, tujiridhishe kwa umakini sana then tufanye maamuzi. R.I.P JPM
ASANTE JOHN