Ndugu yangu, umesema labda unaweza kuamini. Hii ina maana kwamba huamini kuwa Mungu yupo. Lakini hebu fikiria uhai wako, hewa unayovuta, ulimwengu wenye utaratibu kamili—unafikiri vyote hivi vilitokea kwa bahati tu kama huyo jamaa anavyodai? La hasha! Hata Waswahili wanasema "Ukiona vyaelea, vimeundwa"
Kila kitu kinachotuzunguka ni ushahidi kuwa kuna Mungu aliye hai na ndiye aliyetuumba. “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake.” (Zaburi 19:1)
Mungu alipoiumba dunia, wanadamu wa kwanza Adam na Hawa walitenda dhambi kwa kula tunda la mti waliokatazwa. Mungu akasema, kwakuwa wamefanya dhambi hiyo watakufa. Kuanzia wakati huo, kifo, dhambi na uovu viliingia duniani. Ndiyo sababu kila mtu anayezaliwa anakuwa katika hali ya dhambi. Jiulize kwanini mtoto mchanga akinyimwa titi na mamaye anampiga, nani amemfundisha kupiga? Ni asili ya dhambi iliyomo ndani yake.
Dhambi hii ilitutenganisha na Mungu. Ila kwakuwa Mungu ana upendo, alichukua hatua ya kumtuma Yesu Kristo duniani ili aje atuokoe. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yohana 3:16)
Ilibidi damu yake Yesu imwagike msalabani ndio tuweze kupatanishwa na Mungu na kusamehewa dhambi zetu. Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu—ikiwa ni pamoja na dhambi ya kutoamini. “Bali Mungu aonyesha pendo lake mwenyewe kwetu, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” (Warumi 5:8)
Ili uupate msamaha huo, unahitaji kufanya haya yafuatayo:
Amini na kukiri moyoni mwako kuwa Yesu alikufa na kufufuka kwa ajili yako. Warumi 10:9-10 –
“Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.”
Tubu dhambi zako zote na uziache kabisa. Matendo 3:19 – “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana.”
Mpokee Yesu moyoni mwako kwa imani awe Bwana na Mwokozi wako. Yohana 1:12 – “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake."
Ukifanya hayo tu utakuwa umeokoka. Utakuwa umeokoka hukumu ya moto wa milele na utakuwa umepata "tiketi" ya kuingia mbinguni siku Yesu atakaporudi. Wasioamini wote watatupwa katika moto wa milele. Ufunuo 21:8 –"Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na waabudu sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili."
Kwahiyo nakusihi, usikubali moyo wako uendelee kutoamini. Usikubali shetani akudanganye eti Mungu hayupo. Shetani ameishahukumiwa kutupwa katika ziwa liwakalo moto.
Mpokee Yesu sasa na utaona nguvu yake na uwepo wake maishani mwako.
Kama uko tayari kufanya hayo niliyokuambia, omba(fuatisha sala hii ya toba) kwa moyo wako wa dhati, Mungu atakusamehe na kukuhesabu kuwa mtoto wake sasa hivi:
Omba hivi:
"Ee Mungu Baba, nimetambua mimi ni mwenye dhambi. Leo nakuja mbele zako nikiomba msamaha wako. Natubu dhambi zangu zote na kuziacha. Nakiri kuwa Yesu Kristo ni Bwana, na Yeye ndiye Mwokozi wa ulimwengu. Yesu karibu moyoni mwangu utawale maisha yangu kuanzia leo. Naomba unipe nguvu ya kushinda dhambi na kuishi maisha matakatifu. Namkataa shetani na kazi zake zote. Asante Yesu kwa kuniokoa. Katika Jina la Yesu Kristo, ninaomba na kushukuru. Amen.”
Kama umeomba sala hiyo kwa moyo wako wa dhati, tayari umeokoka. Anza kusoma Biblia kila siku na kumuomba Mungu akusaidie kuendelea vizuri kiroho. Tafuta pia Kanisa lolote linalohubiri wokovu na kufundisha utakatifu, watakupa msaada zaidi wa jinsi ya kukua kiroho.
Karibu kwenye familia ya wanaoamini kuwa Mungu yupo na wanaokwenda kwake mbinguni kwenye raha ya milele!