Huu ni msemo maarufu ambao unatumika na waamini mungu wengi siku ya leo lakini muanzilishi wake ni mwanahisabati na mwanafalsafa Mfaransa Blaise Pascal katika Karne ya 17, hoja hii imepwa jina la kamari ya Pascal. Inasema kwamba mtu yeyote mwenye busara anapaswa kuishi kana kwamba Mungu yupo, kwa sababu thawabu inayowezekana (furaha isiyo na mwisho mbinguni) ni kubwa isiyo na kikomo ikilinganishwa na gharama yoyote yenye kikomo (kuacha baadhi ya starehe za dunia), hivyo kuamini kunaonekana kuwa dau lenye mantiki zaidi.
Mantiki Kuu (Matokeo Manne)
Pascal anaeleza imani kwa Mungu kama uamuzi unaofanywa wakati ambapo hakuna uhakika au uthibitisho, akitumia jedwali la hali nne zinazowezekana:
1. Ikiwa Mungu yupo na unaamini: Unapata kila kitu—furaha isiyo na mwisho na wokovu.
2. Ikiwa Mungu yupo na huamini: Unapoteza kila kitu—mateso yasiyo na mwisho au kutengwa na Mungu.
3. Ikiwa Mungu hayupo na unaamini: Unapoteza kiasi kidogo tu—baadhi ya starehe au anasa za muda mfupi za kidunia.
4. Ikiwa Mungu hayupo na huamini: Unapata kiasi kidogo tu—uhuru wa muda mfupi bila dini.
Pingamizi Kuu;
Wanafalsafa wameibua ukosoaji kadhaa dhidi kamari ya Pascal (Pascal’s Wager):
1. Pingamizi la Miungu Wengi:
Hoja ya Pascal inachukulia kuwa kuna chaguo mbili tu (Mungu wa Ukristo dhidi ya kutokuwepo kwa Mungu). Kwa uhalisia, kuna dini nyingi na mitazamo mbalimbali kuhusu Mungu, na baadhi ya hiyo miungu kama ipo huenda ikamwadhibu mtu mwisho wa maisha yake kwa kumwamini mungu mwingine asiye sahihi.
2. Kutokuwa Mkweli/muadilifu: Kumwamini Mungu kwa sababu tu ya kujilinda dhidi ya hatari au kama njia ya kupata thawabu ya Mbinguni ni kutokuwa mwaminifu na kutokuwa mkweli kihisia na ikiwa Mungu ni mjuzi wa yote, atatambua kwamba mtu anafanya tu hesabu ya faida na hasara bila imani ya kweli.
3. Binadamu kutoweza kuwa na imani kama bidhaa nyingine tu ya kuchagua: Imani si kama swichi ya taa ambayo unaweza kuiwasha au kuizima kwa hiari kwa kutegemea hesabu ya gharama na manufaa; kwa kawaida, mtu huamini kwa sababu ameshawishika kwa dhati kwamba jambo fulani ni kweli.
Ushahidi (Evidentialism): Si jambo la kimaadili wala la kiakili kushikilia imani au msimamo wa kina bila kuwa na ushahidi wa kutosha wa kitafiti au kimantiki.