Matumizi ya nguvu kubwa inayotumiwa na Polisi, inatokana na uwezo mdogo wa kutenda kazi zao. Wengi wao hawapewi mafunzo stahiki ya upolisi. Haishangazi kuwasikia wakubwa wao wakisema wanawaajiri ili kulinda kwenye mabenki na maeneo mengine.
Sasa mtu unaemwajiri kulinda Taasisi fulani, ukimpa jukumu la kufanya upelelezi wa mambo mazito yanayohitaji hekima, maarifa, nidhamu na maadili usitarajie afanye vizuri. Lazima atazidiwa, suruhisho linabakia kuwa ni matumizi ya nguvu.
Haishangazi polisi wetu kila siku wanazuia mikutano ya vyama vya siasa ya ndani na nje kwa kisingizio cha usalama, huku wao wenyewe wakienda kwenye mikusanyiko mikubwa ya kimichezo na hakuna hata mende anaekanyagwa.
Polisi wetu wanapokutana na changamoto zinazohitaji maarifa zaidi kuliko nguvu, utawaonea huruma.
Ukisoma historia ya jeshi la polisi Duniani, malengo na dhamira yao, halafu njoo utazame yanayofanyika kwetu, ama Afrika kwa ujumla, utabaki ukiumia moyoni.
Dhana ya usalama wa Raia na Mali zao iliondoka na Mwalimu Nyerere.
Kibaya zaidi ni pale polisi ilipokubali kutumikia siasa badala ya Wananchi. Kwa Polisi ndio Taasisi ambayo kila mtumishi wake huingia kazini kufanya kilicho tofauti na miongozo yao. Na anaefanya vizuri sana kwenye kupindisha haki, huyo ndo huonekana ana sifa za kula mema ya Nchi.