Taarifa zinasema Elon Musk alitumia kiwango hicho kikubwa ambacho ni pamoja na Ketamine ambayo hutumika kama dawa ya usingizi kabla ya upasuaji "anesthesia", lakini pia hupunguza msongo wa mawazo na maumivu.
Inasemekana mkuu huyo wa kitengo cha kusimamia ufanisi wa serikali nchini Marekani DOGE na mshirika wa karibu mno wa Rais Donald Trump alikuwa akisafiri na furushi la dawa mwaka uliopita wakati wa kampeni za Trump.
Jarida la New York Times la nchini humo limechapisha ripoti hii ikiwa ni siku ya mwisho ya Musk kuwepo kwenye Ikulu ya White House baada ya kutangaza siku ya Jumatano kwamba muda wake wa kuiongoza idara hiyo ulikuwa unafikia tamati.
Taarifa hiyo imesemma Musk alikuwa pia akitumia "uyoga wa maajabu" kwa kitaalamu psychedelic mushrooms ambao humfanya mtu kuona ama kusikia vitu visivyokuwepo, lakini pia kuhisi wasiwasi, hofu, misuli kutetemeka na mapigo ya moyo kuongezeka.
Jarida hilo likinukuu chanzo ambacho hakikutambulishwa limesema Musk aliwaambia watu wake wa karibu kwamba alikuwa akinywa dawa nyingi mno za ketamine kiasi cha kuathiri kibofu cha mkojo, ingawa si Musk wala mawakili wake waliokuwa tayari kuzungumzia hilo.
Lakini Musk aliwahi kukiri kuandikiwa dawa za ketamine kutibu msongo wa mawazo.