SURA YA 19
KIONGOZI ANATAKIWA KUEPUKA KUCHUKIWA NA KUDHARAULIKA
Baada ya kuongelea kuhusu sifa kuu hapo juu, zingine zilizobaki nitaziongelea kwa pamoja kama ifuatavyo: kiongozi, kama nilivyokwisha gusia, anatakiwa kufikiria sana jinsi ya kuepuka mambo yatakayomfanya achukiwe au kudharaulika; na kama akifanikiwa kuepuka mambo hayo, atakuwa ametimiza wajibu mkubwa na kujitoa katika hatari hata kama ana sifa zingine mbaya.
Kama nilivyokwisha sema huko nyuma, hakuna jambo litamfanya rais achukiwe haraka kama kuwa mporaji, kuingilia mali za raia wake na wake zao. Hivyo, kiongozi anatakiwa kuepuka sana mambo hayo. Watu huishi kwa amani na kuridhika iwapo heshima na mali zao visipoguswa. Kiongozi anachotakiwa kufanya ni kushughulika na wachache tu ili wasipate nguvu kupita kiasi, na kitu hicho si kazi ngumu.
Kiongozi atadharaulika iwapo ana sifa zifuatazo; kutokuwa na msimamo, muoga, mwenye mizaha, kukosa maamuzi, au kukosa ushupavu. Kiongozi anatakiwa kujilinda sana asionekane ana sifa hizo, na badala yake ajitahidi matendo yake yamuonyeshe kuwa ni mtu mwenye busara, mkuu, na mwenye nguvu. Na anapokuwa anashughulika na raia wake katika faragha, anatakiwa kufanya maamuzi yake kuwa ndiyo ya mwisho, na kuonyesha sifa ambazo hakuna mtu atathubutu kumzoea kupita kiasi, au kumshawishi kufanya jambo asilolitaka.
Kiongozi anayejionyesha kuwa ana sifa hizo, huheshimiwa sana, na yule anayeheshimika ni ngumu kufanyiwa njama, haitakuwa rahisi kumvamia iwapo anajulikana kuwa ni kiongozi mzuri, na anaheshimiwa na wananchi wake. Kiongozi hukabili hatari mbili; moja ni kutoka kwa raia wake, na nyingine kutoka kwa adui wa kigeni. Dhidi ya huyu adui wa pili, anaweza kujilinda kwa kuwa na jeshi imara na washirika wazuri, na kama ana jeshi imara, mara zote atakuwa na washirika wazuri, na utaweza kuwadhibiti adui wa kigeni. Na ukiweza kuwadhibiti adui wa kigeni, itakuwa rahisi kuwadhibiti adui wa ndani, labda kuwe na njama. Na hata kama kuna njama, lakini hakuna adui wa kigeni, kiongozi anayeishi kwa njia nilizoanisha hapo juu, na akiwa hajakata tamaa, ataweza kuhimili shambulio lolote lile, kama nilivyosema; hilo lilitokea kwa Nabis msparta.
Kuhusu raia wake, iwapo hakuna adui wa kigeni wa kushugulika naye, anaweza kuwa na wasiwasi kwamba wanaweza kula njama dhidi yake. Kiongozi anaweza kuwa salama dhidi ya hilo kwa kuepuka kuchukiwa, kudharaulika, na kuwa na uhusiano mzuri na raia wake. Na jambo hili nimeshalizumgumza kwa kirefu sana, ni muhimu kwa kiongozi kutochukiwa wala kudharauliwa na raia wako, ndiyo njia bora kiongozi anayoweza kutumia kujilinda dhidi ya njama. Sababu yule anayefanya njama, mara zote hutafuta kuwafurahisha wananchi kwa kumuua kiongozi. Lakini akiona kuwa, badala ya kuwafurahisha atawaudhi, hawezi kuwa na ujasiri wa kutimiza njama yake. Vikwazo wanavyopitia wala njama ni vingi, na japo tumeona njama nyingi zikitokea, ni chache zimefanikiwa.
Na zaidi ni kuwa, mla njama huwa hawi peke yake, wala hawezi kuchukua mtu yoyote na kula naye njama, isipokuwa wale anaoamini wana vinyongo. Lakini napo, mara tu unapompa mipango yako mtu ambaye anakinyongo, unakuwa umempa njia ya kuondoa kinyongo chake, na kwa kukusaliti anakuwa anajipatia manufaa yote yeye peke yake(Kwa njia zote za kukusaliti atafaidika, kwa kuiba mpango wako, au kwa kutoa siri zako). Na kwa kuona kuwa kwa upande mmoja kuna faida ya hakika, na upande mwingine, jambo la hatari na lisilo na uhakika. Kama akificha siri yako, atakuwa rafiki yako mkubwa huku akiwa adui mkubwa wa kiongozi wake.
Kwa ufupi niseme hivi; upande wa wala njama kuna mashaka, husda na adhabu kali, vitu hivyo ni vikwazo kwake kukuunga mkono. Lakini kwenye upande wa kiongozi kuna utaratibu wa sheria, utukufu wa kifalme, ulinzi kutoka kwa rafiki na serikali; na ukiongezea suala la maslahi ya umma, haiingii akilini kwa mtu kula njama harakaharaka. Japo kwa kawaida mla njama huwa na matatizo kabla ya kutenda uovu wao, lakini mazingira haya(kama kiongozi anapendwa) atakuwa na wasiwasi pia baada ya kukamilisha njama yake. Raia ndiyo watakuwa adui zake, naye hatakuwa na tumaini lolote la kuwa salama
Kuna mifano mingi sana kuhusiana na jambo hilo, lakini nitaelezea tu yale yaliyotokea enzi za mababu zetu. Kiongozi wa Bologna, Bwana mkubwa Annibale Bentivoglio, ambaye ni babu wa huyu Bwana mkubwa Annibale wa sasa, alifanyiwa njama na kuuwawa na Wa-Canneschi, hakuacha mrithi yeyote isipokuwa Bwana mkubwa Giovanni ambaye alikuwa mtoto mchanga wa kubebwa. Mara tu baada ya mauaji hayo, raia wakaasi na kuwaua Wa-canneschi wote. Hili lilisababishwa na jinsi Wa-Bentivogli walivyopendwa katika Bologna; familia hiyo ilipendwa sana kiasi kwamba baada ya kifo cha Bwana mkubwa Annibale hakuna aliyeweza kupewa kuongoza, kulikuwa na imani kuwa mtu wa ukoo wa Bentivogli (ambaye wakati huo ilisadikika ni mtoto wa mhunzi chuma), alikuwa akiishi huko Florence. Wananchi wa Bologna walimfuata na kumuamini kuongoza mji wao, na aliongoza hadi Bwana mkubwa Giovanni alipokuwa na umri wa kutosha kuongoza.
Kwa ufupi ni kuwa, kiongozi hana sababu ya kuogopa njama iwapo wananchi wake wanamheshimu na kumpenda; lakini kama wana chuki dhidi yake na hawaridhiki na utawala wake, anapaswa kuogopa kila mtu na kutomuamini yeyote yule. Nchi zinazoongozwa na viongozi wenye hekima zimehakikisha kuwa watu wa nasaba bora wanatimiziwa mahitaji yao vizuri, huku raia wa kawaida wakiishi kwa kuridhika. Hili ni jambo la muhimu sana kwa kiongozi kulizingatia.
Moja ya serikali inayoongozwa vizuri katika nyakati zetu ni ile ya Ufaransa. Ndani yake kuna taasisi nzuri zisizo na idadi, hizo ndiyo zinalinda uhuru na usalama wa mfalme, na iliyo muhimu kuliko zote ni bunge na mamlaka yake. Aliyeunda na kuipa katiba mamlaka hayo, alijua tabia ya watu wa nasaba bora ya kutaka makuu na kujikweza, hivyo aliona kuna umuhimu wa kuwadhibiti. Na ili kumlinda mfalme dhidi ya vinyongo na chuki, basi ilionelewa kuwa lisiwe jukumu lake kushughulika na watu. Na hilo lilimlinda dhidi ya husda za watu wa uzao bora kwa kuwapendelea raia wa kawaida, au chuki ya raia wa kawaida kwa kuwapendelea watu wa uzao bora. Hivyo alichaguliwaa mtu wa
kati kuwa msuluhishi, ambaye bila kusema kuwa mfalme anahusika aliweza kuwadhibiti watu wa nasaba bora, huku akiwainua wananchi wa kawaida. Hakuwezi kuwa na njia nzuri, ya busara na uhakika ya kumlinda mfalme na ufalme kama hiyo. Hapo tunapata somo lingine, ni kuwa; kiongozi anatakiwa kuwaachia wengine washughulike na maswala yanayohitaji uwajibikaji, huku yeye akibaki na masuala yanayohitaji rehema na zawadi. Na tena, kama nilivyosema; kiongozi anatakiwa kujijengea heshima kubwa na kuepuka kuwa chukizo kwa wananchi wake.
Wengine wanaweza kudhani kuwa; iwapo maisha na vifo vya watawala wengi wa Himaya ya Roma vikichunguzwa, itaonekana kuwa vinatoa mfano ambao ni kinyume na mtazamo wangu. Sababu ni kuwa; baadhi yao walioishi maisha mema na wakajionyesha kuwa ni watu watu wenye sifa nzuri, walipinduliwa na hata kuuwawa na raia wao ambao walikula njama dhidi yao.
Kujibu hoja hiyo, nitaelezea sifa za baadhi ya watawala hao, na hivyo kuonyesha kuwa sababu za kuanguka kwao hazina tofauti na zile nilizozianisha. Na ili kufanya hilo lieleweke vizuri, nitatoa mifano ambayo inaweza kueleweka vizuri na watu waishio sasa. Hivyo, nitazungumzia watawala kutoka utawala wa Marcus mwanafalsafa hadi wakati wa Maximinus. Watawala hao ni, Marcus, Commodus na mwanawe Pertinax, Julianus, Severus na Caracalla mwanawe, Macrinus, Heliogabalus, Alexander na Maximinus.
Kwanza lazima tutambue kuwa, katika falme nyingi, kiongozi anakuwa na kazi ya kuwadhibiti watu wa nasaba bora, na uasi wa raia tu. Lakini watawala wa Roma walikuwa na changamoto nyingine, nayo ni ukatili na uporaji wa wanajeshi wao, ilikuwa ni changamoto kubwa hadi kupelekea kuanguka kwa wengi wa watawala hawa. Sababu kubwa ni kwamba, ilikuwa ni ngumu kwao kuwaridhisha raia wao na wanajeshi kwa pamoja; raia ni wapenda amani hivyo walipendelea kiongozi mwenye busara na mtulivu, lakini wanajeshi walipendelea kiongozi mpenda vita, mkatili, mporaji, na aliyekuwa tayari kutumia sifa hizi kwa raia wake, hii ni ili waweze kujipatia pesa zaidi, na kufanya ukatili wao, uporaji na matendo yao ya pupa.
Kwahiyo, wale watawala ambao hawakupatikana kwa kurithi au kwa uwezo wao wenyewe, hawakuweza kuwa na mamlaka ya kuwadhibiti raia na wanajeshi wao, hilo lilipelekea maangamizi yao. Wengi wao, hasa waliokuwa wageni katika utawala, walipokutana na changamoto hiyo wakaamua kuwaridhisha wanajeshi, na kutojali kuwaudhi wananchi. Na kwa kweli hili lilikuwa ni muhimu kwa wao kufanya, sababu ni kuwa, kwanza kabisa, kiongozi anatakiwa kuepuka kuchukiwa na watu wa matabaka yote, lakini kama hawezi kuepuka kuchukiwa, anatakiwa ajitahidi asichukiwe na tabaka la watu wenye nguvu. Kwa sababu hiyo, watawala waliokuwa wapya walikuwa na uhitaji mkubwa wa kuungwa mkono, hivyo wakaamua kufungamana na jeshi na si watu. Njia hii ilikuwa na manufaa au hasara kadri kiongozi alivyojua jinsi ya kuwadhibiti.
Kwa sababu hizo, ikatokea kuwa, Marcus, Pertinax na Alexander, kwa kuwa walikuwa viongozi wapole, wapenda haki, wanaochukia ukatili na wenye rehema, hawakuwa na mwisho mzuri, isipokuwa Marcus. Marcus pekee ndiye aliyeweza na kuishi na kufa kwa heshima. Hii ni sababu yeye alikuwa ni mtawala kwa kurithi, na si kupitia upendeleo wa wanajeshi au raia. Na pia alikuwa na sifa zilizomfanya aheshimika, hilo lilimuwezesha kudhibiti makundi yote, hakuchukiwa wala kudharaulika.
Lakini Pertinax alichaguliwa kuwa mtawala kinyume na matakwa ya jeshi. Na kwa kuwa walizoea maisha ya kishenzi wakati wa utawala wa Commodus, hawakuweza kustahimili nidhamu ambayo Pertinax alitaka kuirudisha. Kwa hiyo, kwa kufanya achukiwe, na kwa kuwa alikuwa anadharaulika sababu ya uzee wake, alikuwa ameshindwa mara tu alipoanza kuongoza.
Na hapa inatakiwa kukumbukwa kuwa, mtu anaweza kuchukiwa kwa kufanya jambo baya, zuri au sababu zingine. Na kama nilivyokwisha sema, kiongozi anayetaka kulinda mamlaka yake, mara zote atalazimika kutokuwa mwema. Sababu, iwapo tabaka moja, liwe la raia, jeshi au watu wa nasaba
bora, ambalo unaona ni muhimu kupata uungwaji mkono wao ni ovu, utalazimika kuendana nalo na kuruhusu uovu wao, matendo ya wema yatakufanya utengwe nao.
Acha sasa tumuangalie Alexander. Inasemwa yeye hakuwa mtawala wa kawaida, na amepewa sifa nyingi sana. Imeandikwa kuwa, katika miaka kumi na nne ya utawala wake hakuwahi kutoa adhabu ya kifo kwa yoyote bila kumfikisha mahakamani. Pamoja na hayo, alionekana ni dhaifu, na kusemwa kuwa anaongozwa na mama yake. Hilo lilimfanya adharaulike, na jeshi likala njama dhidi yake na kumuua.
Tukigeuka na kuangalia sifa za Commodus, Septimius Severus na Caracalla, tutaona kuwa wote walikuwa ni viongozi katili na waporaji kabisa. Watu ambao ili kuliridhisha jeshi hawakusita kuwatendea ubaya wa aina yoyote raia wao. Na wote, isipokuwa Severus, walipatwa na mwisho mbaya. Severus alikuwa na haiba yenye nguvu iliyomfanya awe rafiki wa wanajeshi japo aliwakandamiza watu wake. Hilo lilimuwezesha kutawala kwa mafanikio mpaka
mwisho wa maisha yake. Sababu ni kuwa, uhodari wake ulimfanya akubalike machoni pa wanajeshi na machoni pa raia. Raia walishangazwa naye na kumstaajabia na wanajeshi walimheshimu na kuridhika naye.
Na kwa sababu matendo yake hayakuwa ya kawaida kwa kiongozi mpya, nitasema kifupi jinsi alivyoelewa namna ya kujivika aina zote za utu, kuwa simba na kuwa mbweha, kama nilivyokwisha sema huko nyuma, ni muhimu kwa kiongozi kuwa na sifa hii.
Kwa kujua uzembe wa mtawala wa Roma, Julianus, Severus alilishawishi jeshi ambalo alikuwa analiongoza huko Illyria. Aliliambia kwamba ulikuwa ni wajibu wao kwenda Roma na kulipa kisasi kwa kifo cha Pertinax ambaye aliuwawa na walinzi wakipretoria. Kwa mbinu hii, na bila kuwaambia lengo lake la kutawala, akawa amefanya jeshi lake kusonga na kufika Italia bila kujulikana. Alipofika Italia, bunge kwa uoga likamchagua kuwa mtawala wa himaya ya Roma na kumuua Julianus. Baada ya kuchukua hatua hii ya kwanza, bado kukawa na vizingiti viwili kwa yeye kuwa mtawala pekee wa himaya yote ya Roma; huko Asia, Pescennius Niger ambaye alikuwa anaongoza majeshi ya mashariki alikuwa kafanya atangazwe kuwa mtawala; mwingine huko magharibi, Albinus, ambaye alikuwa kamanda huko, naye akafanya atangazwe kuwa mtawala. Severus alitambua kuwa ni hatari kutangaza vita dhidi ya wote. Hivyo aliamua kumkabili Niger kwa jeshi na kumkabili Albinus kwa ujanja. Alimuandikia Albinus kuwa, kwa sababu amechaguliwa na bunge kuwa mtawala, angependa kushirikiana naye cheo hicho, hivyo akampatia cheo cha Ukaizari, na kulingana na azimio la bunge, atamchukulia kama mtawala mwenza. Albinus alikubaliana na maneno hayo. Lakini mara tu Severus alipompiga na kumuua Niger, na kuweka utulivu huko mashariki. Alirudi Roma na kulalamika katika bunge kuwa Albinus hana shukrani kwa wema aliomtendea, na amepanga hila kumdhuru; hivyo alikuwa anawajibika kwenda na kumuadhibu kwa kukosa kwake shukrani. Hapo akasonga kwenda mkoa wa Gaul ambako alimvua Albinus cheo chake na kumuua.
Yeyote atakayechunguza matendo ya mtawala huyu kwa makini, atagundua kuwa, ndani yake alikuwa na ukali wa simba na ujanja wa mbweha, na ataona sababu iliyofanya aogopwe na kuheshimiwa na watu, bila kuchukiwa na jeshi. Hivyo hatashangazwa kuwa, japo alikuwa ni mtawala mpya aliweza kudumu akitawala himaya kubwa sana. Sifa zake za kustaajabisha zilimlinda dhidi ya chuki ambayo pengine watu wangekuwa nayo kutokana na ukatili na uporaji wake. Mtoto wake, Caracalla, alikuwa naye kama baba yake, mtu hodari, akiwa na sifa zilizomfanya astaajabiwe machoni pa watu, na kupendwa na jeshi, maana alikuwa ni mtu wa vita. Japo alikuwa ni mwenye uzembe wa kupenda starehe za vyakula na mvivu, lakini ukali na ukatili wake ulikuwa mkubwa sana, ukatili ambao haujawahi kusikika popote(katika nyakati tofauti tofauti alikuwa ameua Raia wengi sana wa Roma, na aliua wakazi wote wa Alexandria kwa wakati mmoja), mambo hayo yalimfanya achukiwe na dunia nzima, na kuogopwa hata na watu wake wa karibu, mwishowe akaishia kuuwawa na afisa wa jeshi lake mwenyewe.
Hapa inatakiwa kujulikana kuwa, vifo vya namna hii vitokanavyo na watu waliojitoa mhanga na waliodhamiria haviwezi kuepukwa na viongozi. Mtu yeyote aliyejitoa mhanga anaweza kutekeleza jambo hilo. Lakini kiongozi hana sababu ya kuogopa jambo hilo sababu hutokea kwa nadra sana. Tahadhari pekee anayotakiwa kuchukua ni kutowatendea vibaya wale wanaomhudumia, au wale walio karibu naye kama maafisa wa baraza, Caracalla alipuuza tahadhari hiyo kwa kumuua kaka wa afisa yule kwa kifo cha aibu, na kwa kuendelea kumtisha afisa yule kila siku ambaye bado aliendelea kutumikia kama mlinzi wake. Jambo hili, kama matendo yaliyofuatia yalivyoonyesha, lilikuwa ni kosa kubwa lililotendwa bila kufikiri.
Sasa tumtazame Commodus, sababu yeye alipata utawala kwa kurithi, inatazamiwa atawale bila vikwazo. Kwa kuwa mwana wa Marcus, alichotakiwa kufanya ni kuiga mwenendo wa baba yake na hivyo kuwaridhisha raia na jeshi. Lakini sababu alikuwa ni mkatili na mwenye roho mbaya, na ili kutimiza tamaa yake ya ulafi wa mali hakujali raia, badala yake alitafuta kuungwa mkono na jeshi na kujiingiza kwenye kila aina ya anasa. Na mbaya zaidi, hakujali kabisa heshima yake, mara nyingi aliingia hadi ulingoni kupigana wakati wa maonyesho ya mapigano ya waroma, na kufanya matendo mengine mengi yasiyomstahili mtawala. Hayo yalimfanya adharauliwe na jeshi. Tendo la kuchukiwa na wananchi huku jeshi likimdharau lilifanya aliwe njama na kuuwawa.
Imebaki sasa kuangalia sifa za Maximinus. Huyu alikuwa ni mtu wa kupenda sana mambo ya vita, na baada ya kifo cha Severus Alexander ambaye tumekwisha muongelea huko nyuma, Maximinus alichaguliwa na kuwa mtawala na jeshi, jeshi ambalo lilikuwa limechukizwa na udhaifu wa mtawala aliyepita. Lakini hakufurahia cheo hicho kwa muda mrefu. Mambo mawili yalitokea yaliyosababisha achukiwe na kudharaulika; sababu moja ilihusiana na asili yake. Ilijulikana na wengi kuwa amewahi kuwa mchunga kondoo huko Thrace, hilo lilifanya wengi wamdharau. Sababu nyingine ni kuwa, baada ya kutangazwa kuwa mtawala, alichelewa kwenda Roma kuchukua cheo. Pia alipata sifa ya ukatili uliopita kiasi kwa sababu ya ukatili uliofanywa na wasimamizi wake huko Roma, na sehemu nyingine za himaya hiyo. Matokea yake ni kuwa dunia yote ilisimama pamoja kwa dharau juu ya asili yake, na chuki juu ukatili wake, Africa ikiongoza, huku bunge na wakazi wa Roma na Italia yote wakifuata katika vuguvugu hilo. Jeshi lake nalo likajiunga katika njama dhidi yake. Wanajeshi wake walipokuwa wameizingira Aquileja, baada ya kuona wanashindwa kuiteka, wakiwa wamechukizwa na ukatili wake, na baada ya kuona kuwa wengi wanampinga wakaacha kumuogapa, wakamuua.
Sitahitaji kuwazungumzia Heliogabalus, Macrinus na Julianus, hawa wote walikuwa ni watu wa hovyo kabisa, na kuanguka kwao kulikuwa kwa haraka sana. Lakini nimalizie kwa kusema kuwa, viongozi wa nyakati zetu hawakabili magumu ya kujitahidi kuwapendeza wanajeshi wao siku zote. Japo wanahitaji kuwadekeza kwa kiasi fulani, uhitaji wa kufanya hivyo huisha mara moja sababu hakuna hata mmoja wa viongozi hao anayemiliki jeshi lake mwenyewe, jeshi ambalo kama lile la Roma, linaloimarika kadri serikali inavyoimarika. Na kama nyakati za Roma ilikuwa ni muhimu kuwaridhisha wanajeshi kuliko wananchi, sababu wanajeshi walikuwa na nguvu kuliko raia, nyakati hizi ni muhimu zaidi kwa viongozi wote isipokuwa wa-Turk na wa-Soldan, kuwaridhisha raia kuliko wanajeshi. Sababu ni kuwa raia wana nguvu kuliko jeshi.
Nimemtoa Turk kwa sababu mara zote anakuwa kazungukwa na wanajeshi kumi na mbili elfu waendao kwa miguu, na kumi na tano elfu waendao kwa farasi, hao ndiyo msingi wa ulinzi na usalama wa ufalme wake, hivyo anahitajika kuwa na uhusiano mzuri nao kuliko raia. Serikali ya Soldan ina hali kama hiyo, yeye pia kwa kuwa tegemezi wa jeshi, anatakiwa kuwajali zaidi ya raia.
Na hapa unatakiwa kutambua kuwa, taifa la wa-Soldan, tofauti na mataifa mengine yote, linafanana sana na utawala wa kanisa la kikistro, ni kwamba haiwezi kusemwa kuwa ni utawala mpya au umepatikana kwa kurithi. Sababu ni kuwa, baada ya kifo cha Soldan anayeongoza, watoto wake hawarithi uongozi, bali anakuwa kiongozi yule anayechaguliwa na wale wenye mamlaka ya kuchagua. Sababu huu ni utaratibu wa miaka mingi, utawala unaochaguliwa hauwezi semwa kuwa ni mpya, na kwa kuwa utawala unaochaguliwa haupati magumu yanayozipata tawala mpya. Japo utawala ni mpya lakini taasisi za taifa bado ni zilezile za zamani, na zimeundwa kwa namna ambayo inamfanya kiongozi aliyechaguliwa aonekane kama ametokana na kurithi.
Tukirudi kwenye mada yetu, ninasema kuwa: mtu akichunguza sababu zilizotolewa hapo juu, ataona kuwa kilichowaangusha watawala niliowataja kilikuwa ni kuchukiwa au kudharaulika. Na pia atatambua kuwa wengine walichagua njia moja na wengine nyingine ambayo ni kinyume chake. Na atatambua kuwa, kwa kila njia ni mtu mmoja tu aliyefanikiwa, wengine wote walikuwa na mwisho mbaya. Sababu Pertinax na Alexander walikuwa ni watawala wapya, ilikuwa ni hasara kwao kuiga matendo ya Marcus, mtawala aliyetokana na kurithi; hivyohivyo kwa Caracalla, Commodus na Maximinus, ilikuwa ni kosa baya kwao kumuiga Severus, sababu hawakuwa na sifa za kuwawezesha kufuata hatua zake.
Kwa kifupi, kiongozi mpya katika kutawala hawezi kuiga matendo ya Marcus, wala si muhimu kwake kuiga matendo ya Severus; lakini anapaswa kuiga kwa Severus yale matendo yanayohitajika katika kutengeneza msingi wa serikali yake, na kutoka kwa Marcus yale yanayotakiwa kuendelea kutawala na kuifanya ifanikiwe baada ya kusimama.