SEHEMU YA TANO
Wakuu nitajitahidi kuandika kwa urefu na nitajitahidi kuandika kila kitu ili mtu mwengine aweze kujifunza kitu. Hata matukio yangu ya aibu pia nitawaeleza ili mtu ajifunze kitu kupitia story yangu na Kama kuna Makosa nilifanya basi iwe rahisi kwa mtu mwengine kujifunza na kurekebisha.
Nilivyorudi kwa yule Dada wa Uhamiaji, alifungua Passport yangu bila kusema chochote aligonga Mhuri nikaondoka zangu. Nikajua kumbe mwanzoni alisema vile ili kunitengenezea mazingira ya kutoa rushwa.
Nilivyotoka tu pale Kaunta, wale Vishoka wakanifuata ili niwarudishie ile Pesa yao, Kwacha 50. Kumbuka hapo nilikuwa bado sijabadili pesa za Kigeni. Nikawauliza wale Jamaa, Kwacha 50 ni sawa na shilingi ngapi za Kitanzania ili niwarudishie pesa yenu, wakaniambia "Wewe tupe Laki Moja tu"
Nikaona wananiletea Ujinga, nikatoka mpaka nje kwa Jamaa ambae alikuwa anawabadilishia watu fedha, Wale Vishoka wapo nyuma yangu tu. Nikataka kubadilisha Pesa yule Jamaa akakataa akasema "Malizana kwanza na hao Jamaa zako".
Nikamwambia kuhusu hawa Jamaa niachie Mimi, wewe nipe huduma tu ya Kubadilisha Pesa, Jamaa alikataa. Nikamwambia basi niambie Kwacha 50 ni sawa na shilingi ngapi za Kitanzania, Hata hilo nalo alikataa aliendelea kusema " Maliza kwanza na hao Jamaa".
Nikaondoka pale kurudi kwenye Bus ili nimuulize Dereva au Konda, Wale Vishoka wapo tu nyuma yangu. Dereva na Konda nao walikataa kutoa ushirikiano kwa madai ya kwamba nimalizane kwanza na wale Vishoka.
Hapo Vishoka wanatoa maneno yote ya Shombo. Lakini nilijifanya kama Siwasikii vile, mwisho wa siku nikawaambia oya nyie sikilizeni Mimi hiyo Laki Moja sina fanyeni mnachotaka kufanya. Tukaanza kuvutana vutana pale na kurushiana maneno. Abiria wengine wapo kimya wanatusikiliza tu.
Mwisho wa Mabishano nilikubali kuwapatia Elfu 50. Roho iliniuma sana. Nilijua fika hapa nimepigwa. Baadae nilikuja kujua kuwa Kwacha 50 ilikuwa kama Elfu Nane ya Kitanzania. Ndo hivyo nilishapigwa.
Baada ya wale Vishoka kushuka ndani ya Bus niliwauliza Dereva na Konda kwa nini walikataa kunisaidia. Wakaniambia kuwa wao ile njia wanapita kila siku na hao Vishoka wapo hapo Boda ya Tunduma miaka na miaka. Kwa hiyo kama wangenisaidia basi Bus lao lingefanya kazi katika Boda hiyo kwa tabu sana pengine wangeweza kutobolewa matairi kila watakapokuwa wanapita hapo. Kwa kweli niliwaelewa.
Aisee kumbe sikuwa peke yangu niliyepigwa usiku ule. Mara waliingia Abiria wengine na Vishoka wengine wakigombana kama ilivyokuwa kwangu. Moyoni nikasema hapa itakuwa kuna mchezo unachezwa kati ya Maafisa Uhamiaji na hawa Vishoka. Ndo mana wanaruhusiwa kuingia hadi ndani.
Tulilala ndani ya Bus hadi asubuhi ndo tukaendelea na safari ya kuelekea Zambia.