Nilivyomkomesha tapeli wa viwanja Kivule Dar es Salaam

shikamkono01

JF-Expert Member
Joined
Mar 26, 2016
Posts
685
Reaction score
2,055
NILIVYOMKOMESHA TAPELI WA VIWANJA KIVULE

Habari zenu wadau wa JF!

Leo nami nimeonelea niwasimulie kisa changu jinsi nilivyomkomesha tapeli maarufu wa viwanja maeneo ya Kivule ajulikanaye kama Juma Kasangu,mnamo mwaka 2014 mwanzoni nikiwa katika harakati zangu za kutaka kujipatia eneo nikamshirikisha rafiki yangu mmoja ambaye yeye alishakuwa na eneo kule Kivule maarufu kama kwa mama Anna Mkapa

Huyu jamaa yangu alishaanza na ujenzi akawa ameshaweka msingi ila kutokana na changamoto za kiuchumi akawa ameliacha kwanza avute nguvu ndipo nami baada ya kumueleza tamanio langu naye akanipeleka nikapaone eneo analojenga nami baada ya kufika kiukweli nikapapenda sana kwanza pako tambarare, mazingira rafiki, mji ulikuwa umepangiliwa kwani Serikali ya mtaa ilichora njia kabisa na walikuwa wakali hadi kufikia kupita mara kwa mara kwenye maeneo ya ujenzi kuhakikisha hakuna anayejenga kiholela, mpangilio wa mitaa ulitiliwa mkazo sana, hizo ni mojawapo wa sifa kuu zilizopelekea kupapenda eneo lile.

Sasa kwakuwa huyu jamaa yangu alinunua eneo kutoka kwa huyu Juma Kasangu nami akaniunganishia kwake ili niweze kupata eneo maeneo karibu na eneo la kwake,(waweza kushangaa imekuwaje nimpe sifa ya utapeli wakati aliyenipeleka nae aliuziwa eneo na huyo huyo tapeli😂😂)

Kiukweli huyu Kasangu ni mbwa miongoni mwa mambwa koko wakubwa sana kiukweli sijui hatima yangu na namuomba sana Mungu anijaalie mwisho mwema ila huyu jamaa ana mzigo mzito sana kesho mbele ya muumba wake kama hajajirekebisha (sina uhakika kama bado yuko hai).

Huyu jamaa yangu nae wakati wa kimbembe changu ndipo akaja kupewa mkanda wake ponapona yake ilikuwaje hadi kutofikia kutapeliwa, kumbe kilichomuokoa ni kuwahi kuanza kujenga lile eneo kwani kumbe pale alipouziwa jamaa yangu mwenye eneo ni baba mkwe wake Kasangu (baba wa mkewe) na walipoona pameshaanzwa ujenzi ikabidi wakamalizane kiukwe na kutoyatoa hadharani (naamini hata huyo baba mkwe hakupewa chochote)

Turudi sasa katika sakata langu, siku hiyo mimi na jamaa yangu na ndugu yangu mwingine baada ya kumpanga bwana Kasangu, Jumamosi moja tukatoka makwetu wakati huo mimi nakaa Ilala Sharifu Shamba na wenzangu walikuwa wanatokea maeneo ya Ilala sokoni (kiuzawa mimi nimezaliwa maeneo ya Ilala sokoni) tukaelekea eneo la tukio kwa kupanda gari hadi Banana pale tukapanda hadi Kivule napo tukatembea mdogo mdogo kwenda huko kwa mama Mkapa (kulikuwa hakuna vigari wakati huo ni bodaboda tena hazikuwa kihivyo kuna mchanga sana ila nasikia siku hizi daladala zinafika)

Kasangu akaja na vijana wake wawili (Kasangu kikabila ni mnyamwezi)hao vijana walikuwa ni wakurya nao ni Marwa na mwingine sikuwa nimemtambua kwa jina vizuri maana ni siku hiyo tu sikumuona tena wakati wote wa sakata hili

Marwa nilimtambua kwakuwa uko mbele pia nilipata msaada wake, sasa tukafika eneo la tukio na akatuonesha viwanja vitatu ambavyo viko kama mita 120-150 kutoka eneo ambalo jamaa yangu ameuziwa, tukavikagua na mwishowe nikakichagua cha kukichagua na ikafika muda wa kufanya malipo na yule mtu aliyekuja nae pamoja na Marwa alinitambulisha kama mjumbe wa eneo lile kwani pia alikuwa na mihuri kabisa na mauzo yalikuwa ni 1,200,000/= (mauzo yote yalikuwa ni 1,500,000) nikampatia pesa na mashahidi wakaweka saini zao na nikamtaka lazima twende Serikali ya mtaa kukamilisha makubaliano ndio nimmalizie hiyo 300,000 yake

Tukatoka eneo la tukio salama na jamaa yangu akanisisitiza kuanza ujenzi japo msingi wa vyumba viwili kwani jambo la moto unalifanya na moto wake nisipoe tena nami baada ya kama miezi minne nakumbuka nikaanza kujipanga na kuanza ujenzi (pesa yake iliyobaki nikawa nampa kidogo kidogo mara 50 mara 20)


Itaendelea...
 
NILIVYOMKOMESHA TAPELI WA VIWANJA KIVULE

Sehemu ya 2

KASHESHE LILIPOANZA
Baada ya kama miezi 6 nikaanza na utaratibu wa kumtafuta fundi wa kuweza kufanya zoezi la ujenzi na kupitia yule jamaa yangu ambaye ni mwenyeji wangu kule tukashauriana tumpate mjenzi kutoka eneo la karibu na ujenzi na tukampata mzee mmoja ajulikanaye kama mzee Ndevu (alikuwa mwema sana kwangu)na akanipa gharama na mahitaji ya ujenzi na kazi ikaanza

Ilipofika siku ya tano toka ujenzi kuanza nikiwa katikati ya mji nikiwa katika mihangaiko yangu ya mtu mweusi nikapigiwa simu na namba ngeni nikaipokea na yule jamaa baada ya salamu akajitambulisha kwangu majina yake, umiliki wake wa eneo nami sikupaniki kwa yale maelezo yake na wala sikutaka kumbishia kuhusiana na umiliki wake ila kikubwa nikamuomba tukutane kwa kujuana, kujuzana zaidi na mengineyo (kiukweli upokeaji wangu wa simu na kuongea nae kiungwana kulinisaidia sana sana)

Basi yule jamaa akanielekeza anapokaa ambapo ni Kinondoni Mkwajuni na wakati huo mimi nilikuwa nimeshatoka Sharifu Shamba na kuhamia Magomeni kanisani hivyo usiku wa siku hiyo hiyo muda wa saa 2 nikaenda Mkwajuni kukutana na yule jamaa, nikakutana na yule jamaa (jina lake nimelisahau nilitamani sana nimtaje kwa jina kwani nae alinipigania sana)pale maeneo ya Katumba bar na tukazungumza kindugu sana na jamaa kwanza alikuwa ni mwanajeshi na yupo makao makuu yao kule Upanga na akanieleza mengi kuhusiana na yule Kasangu kuwa ni msumbufu sana na amekuwa na tabia ya kuuza maeneo ya watu sana tena amekuwa akilindwa na mapolisi wa kituo cha Staki shari katika uovu wake ila aliniahidi kuwa tutakuwa pamoja na kweli tulikuwa pamoja wakati wote wa sakata hili na akanishauri kwa hatua ya awali niende kufungua jalada pale Staki shari.


Siku iliyofuata nikaelekea huko na kufungua shauri na nikapewa mpelelezi mmoja aitwae Juma, huyu jamaa dah yaani wakati mimi nina moto wa kesi yeye akawa nikifika ananitoa tunaenda pale nje ya kituo ananambia mi sijanywa chai njoo tuongelee pale mgahawani yaani ikawa mimi tena ndio naumizwa zaidi na baada kama ya wiki tatu za kalenda yule jamaa akaenda likizo uko kwao Tabora na simu zikawa hazikauki mara vocha, mara huku kijijini nipush na mengine mengi na hadi wakati huo sakata langu halijapata mwanga wowote na wakati ameenda likizo faili langu likahamishiwa kwa mpelelezi mwingine mtu mzima hivi na nadhani alikuwa katika nyakati zake za mwisho ofisini (huyu alikuwa tatizo kuliko yule Juma😂).

Huyu mpelelezi mpya nae nadhani alikuwa anaitwa mzee Juma kama sijakosea dah yaani suala langu ndio likawa limelala kabisaaa yaani kama mwanzo lilikuwa linatambaa hapa likawa limesimama na hakukuwa na mwelekeo na halikuwa linaeleweka linaelekea wapi


MUNGU SI ATHUMANI

Nikiwa nimekata tamaa sijui mwelekeo wa shauri langu siku hiyo nimekaa maskani nikaona simu inaita na mpigaji alikuwa yule Marwa dah nikajisemea anataka nini huyu mtu.

Nirudi nyuma kidogo kutoka kufungua shauri hadi hii siku Marwa ananipigia ilishapita zaidi ya miezi 6 na huyu Marwa alinambia ana matatizo ya kiafya nadhani alikuwa na tatizo la moyo au presha na kliniki yake alikuwa anaenda pale Mnazi mmoja hivyo kama mara mbili tatu alikuwa ananipigia anapita Ilala tunaongea nampa nauli na kiukweli hii ilinisaidia sana katika kupata mwanga wa shauri langu

Turudi kwenye simu aliyopiga Marwa, nikaipokea na kusalimiana nae na akaniuliza niko wapi nikamjibu nipo Kariakoo, akaniambia njoo haraka sana Staki shari kwani Kasangu amekamatwa na ndugu zake wanaangaikia kumtoa hivyo nimuwahi kabla hajatolewa, kiukweli nilichukua pikipiki hadi pale njia panda ya Segerea na nikawa natembea mbiombio kuelekea Staki shari na Mungu jaalia nafika kituoni ndio yule bwana alikuwa ameshadhaminiwa na yupo nje tu ya jengo, nikamdaka mkono na kumwambia turudi kule kituoni na kama anabisha ntamjazia watu na hatoamini macho yake!

Kiupole nikiwa nimemshika mkono wale jamaa zake wakawa wanashangaa imekuwaje tena mimi sikutaka kuwaeleza lolote wao wakawa wanajiuliza tu imekuwaje ndugu yao bila kupinga anakubali kurudi kituoni?

Nilipofika nae kaunta pale askari tuliyemkuta akawa anamuuliza yule Kasangu "Juma imekuwaje tena?" Mimi sikumpa nafasi ya kuzungumza nikamueleza kuwa yule ni mtuhumiwa wangu na nimemleta pale kutokana na suala hilo ,akaniuliza je unayo file number? Nikatoa simu yangu ndogo nikamsomea RB# na akatizama katika daftari lake kujiridhisha na akaona kweli, shauri lilifunguliwa kwa "UTAPELI WA KUUZA ENEO AMBALO SIO LAKE" na akaandika maelezo pale na kunitaka niende na kufika siku inayofuata na nikafanya hivyo.

Siku iliyofuata nikafika na kuonana na mpelelezi wangu yule mzee Juma ili kujua nini kinaendelea na nikamkuta tukazungumza kidogo na nilipotaka kujua kuhusu mtuhumiwa wangu akanambia yule bwana amedhaminiwa na niende nyumbani atanijuza siku mbili tatu, kiukweli shauri hili lilinipa ujasiri sana hadi katika maisha yangu ya sasa kwani nikamjibu pale pale hivi niende nyumbani unaona inatosha sio?

Yaani nimepoteza pesa wewe unamuachia mtuhumiwa ambaye nimefungua shauri miezi na leo nimemleta wewe unanijibu simple kabisa eti kadhaminiwa, nikamwambia dhamana ni haki yake lakini tambua haki ina wajibu mimi naenda na sitakaa eti kusubiri simu yako,nadai changu na nitakuja kadri nijisikiavyo kujua kinachoendelea kuhusu hili suala

Nikatoka nikiwa nimeghadhibika sana na kesho kutwa yake nikatimba tena pale kituoni kujua huyo aliyedhaminiwa yuko wapi akanipiga kalenda ila nikampa vipande vyake tena na nikaenda tena kama mara 4 hivi hadi yule mzee Juma akawa ananikaripia na kuniona mimi msumbufu dah kiukweli sikumkawiza nikamwambia wewe umempa dhamana mtuhumiwa wangu kwa maana umejiridhisha na documents zake sasa hao wadhamini wake wako wapi?

Je, umekwenda Serikali ya mtaa huko anapokaa kuwafatilia wale wadhamini wake? Nikamwambia mtuhumiwa nimemleta mwenyewe na ninamtaka hapa na sitakaa kimya hadi nijue hatima ya haki yangu na uliweke kichwani hilo

Sasa wakati nakwenda kwenda pale kituoni sura yangu ikawa imezoeleka kwa maaskari pale kituoni maana naweza nikafika kituoni saa 1 asubuhi hadi saa 6 mchana na nikawa sasa yule mzee simpigii simu nafika tu nakaa upande wa pili wa kituo kwenye mgahawa na nikimuona ndio namfuata kumuuliza maana alikuwa mara hapokei au ananiambia ametoka nisije yuko mbali

Nikiwa nimekaa pale mgahawani siku moja kuna afande fulani akaniuliza "we jamaa hivi hadi leo jambo lako ni danadana? Komaa ndugu ujue yule Juma Kasangu anakula na baadhi ya maaskari kwani yupo mtaani na hawataweza kumkamata kama hautakomaa, kaza uzi ndugu yangu" dah kiukweli yale maneno yalinipa ujasiri sana kwani awali mawazo yangu yalikuwa yanaamini askari wote wa pale walikuwa wanalipuuzia shauri langu lakini baada ya yule afande kunambia yale maneno tena akiwa na wenzake wawili yalinipa hope sana na nikajiambia sasa ngoja nikajipange kwa mpango kazi!

Nikatoka pale bila kuonana na yule mzee Juma nikarudi zangu nyumbani na kiukweli niliumiza kichwa sana na kujiuliza sasa nafanyaje? Nakumbuka ile siku ilikuwa ni Jumamosi



Itaendelea....
 
Nimescroll kabla sijasoma kuona kama imefika mwisho,, nilipoona itaendelea nimeignore.. utawaendelezea wengine
 
NILIVYOMKOMESHA TAPELI WA VIWANJA KIVULE

Sehemu ya 3


KAMA NOMA NA IWE NOMA

Siku ya jumatatu asubuhi na mapema nikiwa na akili zangu za usiku nikatoka zangu Magomeni kuelekea pale Staki shari mapema tu moja kasoro kadhaa niko pale nikawakuta maaskari wanajipanga kwa ajili ya lokoo ya kuanza siku mpya na kulikuwa na kiongozi wao yeye akiwa amevaa combat kama za wale field force mtu mzima hivi mfupi na mweupe kiasi nikamngojea awakague wale maaskari na nikamwendea nikidhani ndio mkuu wa kituo nikamsalimu na kumuelezea changamoto zangu na akanambia yeye sio mkuu ila nipite pale kolidoni na nikate kulia nisome vibao juu ya milango na nikae nje ya mlango ulioandikwa MKUU WA KITUO,nikamshukuru na nikaingia ndani kufata maelezo niliyopewa,nilipofika kaunta askari aliyekuwepo akaniuliza ninapoenda na nikamuelezea ninapoenda,nikasoma vibao na nikafika eneo husika uzuri wake kulikuwa na kibenchi nikakaa pale kimya,sasa wakati nimekaa pale kumbuka maaskari wengi si wananifahamu wakawa wananiuliza kulikoni nikawa namngojea mkuu na nadhani katika wale maaskari walionikuta pale wakaenda kumtonya yule mpelelezi mzee Juma akaja pale anajifanya kama anaongea peke yake kuwa najisumbua tu uko ninapotaka kwenda nami wala sikumjibu kwani ilibidi nijiusie mwenyewe moyoni kwani nilikuwa na donge limenibana sana nikifikiria nadai changu naonekana msumbufu? Tena mtuhumiwa nimemkamata amempa dhamana alafu ananambia nikakae nyumbani hadi atakapopatikana eti ndio atanipigia,leo ananiona mimi ndio tatizo,nikajiambia nisifungue mdomo acha alopoke tu.
Mara akafika askari aliyekuwa amevaa kiraia na akatoa ufunguo na kufungua kile chumba na nyuma yake akiwa ameongozana na kundi la watu kama watano hivi na yule kiongozi akanisalimu huku akiwa ameshafungua mlango nami nikajibu salamu yake na akaniuliza tatizo langu maana yeye hakuwa na muda kwani alitakiwa kwenda uwanja wa ndege kusimamia msafara kuna ugeni unakuja kwahiyo lazima awepo eneo la tukio ila kwakuwa ni jumatatu anataka kufanya kikao kidogo na watendaji wake kupata details za yaliyojiri kwa wiki nzima iliyopita,wakati huo ananipa maelezo hayo tukawa yeye na mimi na wale wenzake tumeshaingia ndani ya kile chumba na akanitaka kama sitojali nimngojee hadi atakapotoka uwanja wa ndege ila nikamuomba sana anipe japo dakika 5 tu kwangu zingenitosha kujua hatima ya shauri langu naye akanipa!
Nikajitambulisha na kumueleza suala langu na aliyekuwa na faili na matukio yote toka kumkamata na hadi kuachiwa na kutakiwa nijae nyumbani hadi atakapopatikana mtuhumiwa na nikahitimisha kwa kumuomba kuwa "yeye ndio mtu wa mwisho katika kituo ambacho faili la kesi yangu lipo naomba kauli yako kuwa kituo kimeshindwa kutatua tatizo langu na unanipa ruksa ya kwenda mbele kusaka haki yangu" tena yule mzee Juma aliwa ameitwa na miongoni mwa waliokuwa pale kumbe kulikuwa na mkuu wa upelelezi wa kituo na maofisa wengine,yule mzee Juma anaulizwa hana analosema lenye mashiko na mkuu akawauliza "toka mmeanza kufanya kazi kwenu mmeshakutana na mwananchi mwenye uthubutu wa kudai haki yake katika mfumo huu? Huu ni mtego kwani kama ameweza kuja hadi kwangu je anashindwa kwenda wapi? Mtuhumiwa kamleta mmemtoa,mwendelezo hamtoi je afanyaje?" Yule mzee Juma akajitdmtea kuwa nitoe pesa ya mafuta ya gari ili waende kumsaka na yule mkuu akaniuliza je nipo tayari kutoa pesa ya mafuta? nikamjibu pale pale nishapoteza pesa na mtuhumiwa nishamleta sina hiyo pesa na huyu mpelelezi yeye kama kutoa ndio atoe kwani alijiridhisha akampa dhamana,sina hiyo pesa,yule mkuu akaona huu mziki sasa akanambia sara naomba japo siku 3 nitakupatia jibu nikamwambia poa ntakuja ijumaa na nikatoka zangu huyooo!
Ile ijumaa mimi sikuenda nikakaa kama wiki kadhaa ndipo huo msemo wa MUNGU SI ATHUMAN ukachukua nafasi tena kwani yule bwana Juma Kasangu akawa anaendelea na utapeli wake sijui walimtapeli mama gani uko waliuza nyumba yao ya familia uko Buguruni na yule mama akaenda kununua kiwanja na kwakuwa alikuwa na pesa tayari ujenzi ukaanza mara moja na mama ujenzi umefika kwenye rinta akaja kuelezwa kuwa eneo analojenga sio lake na kule jirani na eneo ambalo mimi nimeuziwa kulikuwa na eneo kubwa sana lilikuwa linamilikiwa na taasisi flani inaitwa UVIKIUTA sijajua wanajihusisha na nini na hawa kina Kasangu wakawa wanaenda kuwauzia watu viwanja kule na wale jamaa uwa wakifanya operesheni inakuwa kama vita wanakwenda kamili na field force na mabomu ya machozi kutokana na historia ya eneo lenyewe na asilimia kubwa ya wakaazi wa maeneo yale walikuwa Wakulya na kama unavyojua hawa ndugu zetu,tatizo kule mpaka wa wale Uvikiuta hakukuwa na mipaka yenye kuonekana wazi sasa unaweza kuwa hapa ukaambiwa upo nje pale ukaambiwa upo ndani yaani wanaweza kuja awamu hii ukaachwa na wakaja awamu nyingine ukatolewa mkukumkuku sasa wale kina Kasangu ndio wakawa wanatumia huo kutokuwepo na mipaka ya wazi kama njia ya kuwapiga wananchi.
Sasa kumbe yule bwana Juma Kasangu akiwa na vijana wake waliuza sijajua eneo gani na nasikia walipata kama milioni 8 hivi yule bwana akawa amewadhulumu wenzake na kati ya aliowashirikiana nao kuna jamaa anaitwa Chacha😂,huyu bwana nadhani alipewa namba yangu na yule Marwa kwani alinipigia siku hiyo sina hili wala lile akataka kuonana nami nikamuelekeza na akaja mara moja Ilala tulikutania pale Ilala mtaa wa Kigoma na Moshi kulikuwa na duka la Mangi,akanieleza mikasa mingi na kueleza waziwazi kuwa amesikia kuhusu ishu yangu na yule wamefanya tukio pamoja na amewazika yeye na wenzake sasa hasira zake anataka kuzihamishia kwa kumkomoa kupitia mimi,ule msemo wa "adui wa adui yako ni rafiki yako" ukachukua nafasi na akanambia jinsi tunatakiwa tufanye na yeye atafanya yake kadri ya uwezo wake na kazi alitaka ifanyike mapema iwezekanavyo nami nikimshirikisha mshkaji wangu mmoja anaitwa Kindamba na Kindamba akampigia Kasangu na kumwambia anataka eneo kwani amepewa namba kupitia rafiki yake,Kasangu akamuuliza kuwa anakaa wapi naye akamjibu kuwa anakaa Mwananyamala A na akamwambia atakuja jioni akitoka kazini ili aje aone maeneo (tulipanga iwe jioni kwa sababu mbalimbali nazo ni kuweza kufika eneo wakati ofisi za serikali ya mtaa kumefungwa,mimi kutoonekana kwakuwa giza litakuwa lishashuka na kuepusha wambea kuwa wengi na kupata kujipanga vyema)


Itaendelea...
 
ni bodaboda tena hazikuwa kihivyo kuna mchanga sana ila nasikia siku hizi daladala zinafika

KUNA SEHEMU ZINA MICHANGA BALAA ALAF BODA BODA ANAENDESHA KAMA VILE HAKUNA MCHANGA....
BODA WA TOWN HAWEZ KUENDESHA KULE KAMA NDIO FIRST TIME...

pia boda boda wa Kule wengine huogopa KUENDESHA barabara zenye misongamano ya magari mengi.......
 
Ndugu zangu kikubwa tuvumiliane upande wa mwandiko kwani kila ninapojaribu kuweka aya na nikipost nakuta marekebisho niliyoyafanya hayajaleta tija,mnisamehe tu bure mpya katika sekta ya uandishi!
Stori inaeleweka hata usijali kuhusu mwandiko kwani hata madaktari hujawafikia kwa ubovu wa mwandiko. Ukishusha unitag
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…