Nilivyonusurika Kifo baada ya Mzee kunitimua nyumbani - 7.
Sikutaka kabisa marafiki zangu na watu wanaonifahamu pale stendi wahisi kitu,kiukweli japo nilikuwa mikononi mwa wale askari lakini nilijitahidi sana kuonyesha hali ya kawaida na tena tulipofika kwenye hiace ya kuelekea mjini ni mimi ndiye niliyefanya kazi ya kuwaombea lift nikijifanya niwanangu!
Sasa tulipofika pale mjini kukamata mchomoko wa kuelekea Sirari ilibidi askari mmoja atoe hela amlipie yule mwenzie na mimi kudandia bure,wasingeweza kupanda mchomoko bure kwasababu ilikuwa inachukua watu wachache!.
Basi tukaondoka na hatimaye tukafika pale stendi ya mchomoko Sirari,tulipofika pale wanangu walianza kunichangamkia na wengine kuniuliza nilienda wapi,sasa wale askari wakataka kunidhibiti lakini niliwaambia kiaina ya kwamba siwezi kukimbia na wasinidharirishe mbele ya wana,bahati nzuri jamaa walikuwa waelewa na wao wakawa wameniacha najifanya kujizungumzisha mbele ya washikaji kana kwamba sina kosa kumbe moyoni naujua ukweli!.
Baada ya mazungumzo pale stendi na wanangu,nilijikuta kitete chote kimetoweka na kisha nikaandamana na wale mapongo hadi nilipokuwa nimepanga!.Nashukuru Mungu hakuna mtu aliyeshitukia mchezo pale stendi.Basi baada ya kufika hapo nyumbani nilifunua kifuta miguu(zulia)pale mlangoni kisha nikatoa funguo nikafungua mlango!.Sasa ile nyumba sikuwa peke yangu,kulikuwa na wapangaji wengine ambao nao kuna wengine walikuwa kwenye shughuli zao na wengine hasa wanawake walikuwa nyumbani,sasa desturi ikawa ni ileile ya kwamba asifahamu mtu yeyote kwamba wale ni askari,nilipofungua mlango niliwakaribisha kwa sauti ya "Karibuni" ili asitokee mtu yeyote akajua kitu.
Baada ya kufika ndani askari mmoja akaniomba funguo akafunga mlango kisha wakanitaka tuanzie kufanya upekuzi chumbani.Upekuzi haukuchukua muda mrefu kwasababu sikuwa nimejaza mle ndani makorokoro,bali kulikuwa na kitanda pamoja na begi kubwa la nguo na vitu vidogo vya kawaida,sebuleni nako kulikuwa na makochi,TV na redio na picha za ukutani zilizopendezesha sebule.Hakukuwa na vyombo vingi kwasababu nilikuwaga sipiki hapo nyumbani bali nilikuwa nakula kwa mama ntilie,nilikuwa na mabeseni mawili pamoja ndoo mbili tatu nilizotumia kwa ajili ya kuwekea maji ya kuoga na kufulia.
Sasa pesa zangu zote nilikuwaga nazihifadhi kwenye mfuko wa suruali kisha naweka hiyo suruali kwenye begi pamoja na nguo nyingine,wale askari walipekua kila mahali bila kuona kitu chochote.Wakati huo nilikuwa nimebaki na zile fedha haramu kiasi cha shilingi elfu 40,pia nilikuwa nina hela halali kiasi cha shilingi laki moja na elfu themanini.
Askari "Nadhani unajua kilichotuleta hapa ni kitu gani,hebu kuwa mkweli pesa umeweka wapi?,au unataka tutumie nguvu?"
Aliendelea "Mpaka tumefika hapa umekuwa mstaarabu,angalia mambo yasije haribikia hapa"
Baada ya jamaa kuniambia vile na akionekana kumaanisha,nilichukua ile suruali iliyokuwa imetupwa chini kutokana na shaghala baghala ya upekuzi nikatoa zile hela nikamkabidhi jamaa!.
Askari "Haya sasa ndiyo mambo,endelea kutafuta najua bado zipo nyingine!"
Mimi "Hapana afande pesa niliyokuwa nayo ndiyo hiyo"
Askari "Kwanini unatupotezea muda?,siutoe pesa mdogo wangu tuondoke!,au unataka tutumie nguvu?"
Mimi "Kweli afande pesa yote niliyokuwa nayo ndiyo hiyo"
Jamaa waliendelea kutafuta kila mahali lakini hawakuona kitu,sasa kwakuwa niliwapa zile hela askari mmoja akawa amesema wanipige pingu kwakuwa tayari kidhibiti nilikuwa nacho.Niliwaangukia miguuni nikawasihi wasinipige pingu na sitowasumbua njiani!,yule askari aliyefunga mlango wakati tunaingia ndani kiukweli akawa akinionea huruma sana kama kijana mwenzie na akamwambia mwenzie asifanye hivyo kwakuwa wakati tunakuja sikuwasumbua,sasa yule mwenzie akawa ameendelea kuweka msisitizo kwamba nipigwe pingu!.
Basi baada ya kuwasihi sana huku machozi yakinitoka,wakawa wamekubali na wakanitaka nisije kujaribu kuwakimbia.Sasa wakati tunatoka nikachukua ufunguo nikampelekea dada mmoja aliyekuwa mke wa mpangaji mwenzangu hapo nyumbani,nilimwambia akae na ule ufunguo kuna mahali naenda na nikirudi nitaukuta kwake!.
Tukaondoka na wale askari mpaka stendi tukapanda mchomoko kuelekea Tarime mjini,kwa namna tulivyokuwa tunatembea na wale askari wakiniuliza maswali kadhaa huku nikiendelea kuwajibu nilihakikisha kabisa hakuna mtu anayefahamu jambo lile,mimi sikutaka kabisa kujifanya mjuaji ili kujiepusha na aibu isiyokuwa ya lazima!.
Tulipofika pale Tarime mjini tukitokea Sirari,kuna askari mmoja niliona anaongea na simu na sikufahamu alichokuwa anaongea,sasa baada ya maongezi yale kwenye simu,alimwambia yule askari mwenzake kwamba ahakikishe nakaa chini,basi nilikaa chini huku yule askari mwingine akiondoka kusikojulikana!,wakati nimekaa chini yule askari alikuwa makini sana na mimi na hakutaka kabisa stori na maongezi!.Baada ya dakika 10 niliona difenda imefika lile eneo na kutakiwa kupanda.
Moyo wangu uliuma sana na nilikuwa nawaza napelekwa wapi wakati ilipaswa nirudishwe hadi buhemba nilikokuwa nimetokea!.Sikufahamu hatima ya Gabriel na mkewe iliendelea vipi nilipowaacha!,mimi nilijua huo msalaba tayari ndiyo nishaubeba!.Kilichokuwa kinaniumiza zaidi ni namna wazazi wangu wakija kufahamu ya kwamba mtoto wao nipo polisi au kufungwa gerezani,nilikuwa navuta picha ya Mzee wangu namna atakavyo ongea akisikia nimekamatwa,tena nilijua ndiyo atajihahakishia kabisa kwamba kunitimua pale nyumbani alikuwa sahihi kabisa!.
Basi niliamua kutulia ndani ya difenda na kumuachia Mungu yeye ndiye akawe muamuzi wa lile jambo,kwa hatua niliyokuwa nimefikia sikuwa na msaada wowote zaidi ya kuamini ni Mungu peke yake ndiye anaweza kuniokoa na mkono wa serikali!.
Kuna muda hata kama humjui Mungu na hujawai kukanyaga kabisa kanisani au msikitini,unapofikwa na jambo gumu kiutatuzi ndipo siku hiyo utatamani mahubiri na mihadhara isikike mahali ulipo ili uweze kuamini kuna Mungu na utajaribu kusali sala zote na utatumia lugha zote kumuomba hata kama unayemuomba uliamini hayupo.
Mpaka wakati huo baada ya kujiingiza kwenye upiga debe na vile vistarehe uchwara vya muda mfupi sikuwahi kabisa kukanyaga mlango wa kanisa lakini baada ya kupata hiyo changamoto ya muda mfupi nilikuwa nikimlilia Mungu kimoyo moyo aniokoe na kile kikombe kana kwamba nilikuwa muhudhuriaji mzuri wa ibada!.
Baada ya kupakiwa kwenye ile difenda nilipewa amri ya kukaa chini na kusogea mbele kabisa na miguu kuikalisha chini ikiwa imenyooka,ile difenda iliondoka yale maeneo kuelekea Nyamisangura ambako tulipofika pia huko kuna jamaa kama 6 walipakiwa kwenye ile difenda na kufanya jumla yetu wahalifu kuwa 7.Basi baada ya hapo ikaondoka kwa spidi kali huku askari wengine waliokuwa na bunduki wakidandia na kuondoka!.
Sasa tulipofikishwa pale central,baada ya kushuka tulitakiwa kuelekea ndani kwa kukimbia huku mikono tukiambiwa tuweke kichwani!,baada ya kufika ndani askari mmoja wapo wa wale niliokuwa nao akawa ameniambia nifuatane naye.Ndipo akafungua chumba kimoja ambacho baada ya kuingia ndani nikamkuta Gabriel na mkewe akiwa na yule askari niliyewaacha nae pale nyumbani kwake!.
Askari "Ooh umemleta bwana mdogo"
Aliendelea "Unapofika hapa kwetu bwana mdogo hakuna makaochi hivyo unatakiwa ukae chini!".
Basi baada ya hapo nikaona yule askari anatoa ile hela elfu 40 ambayo haikuwa halali anamkabidhi yule askari ambaye ilionekana alikuwa mkuu wa upepelezi!.Kilichonishangaza ni kutokuona ile laki moja na elfu themanini ambayo ilikuwa halali sikuona anakabidhiwa yule afande na ndipo nikagundua wale askari watakuwa waligawana ile hela!.
Basi baada ya mazungumzo ya muda mrefu hapo ndani huku tukiwa tunahojiwa na yule askari kuandika maelezo yetu,alipomaliza akawa amemwambia yule askari tunapaswa kuwekwa rumande!.Kiukweli nilijuta sana moyoni na sitakaa nisahau ile siku.Kabla ya kuingizwa rumande nilimuomba yule afande simu yangu ili niwasiliane na ndugu zangu wawe na taarifa,hakuwa na shida kabisa na alinipatia ile simu na akanitaka niongee nikiwa mle mle ndani ya kile chumba.
Basi baada ya kupewa ile simu,nilimpigia mwanangu mmoja tuliyekuwa tumeshibana sana aliyekuwa mpiga debe mwenzangu pale Sirari!.
Mimi "Nyamori mambo vipi?"
Nyamori "Mzee wa kuzugia mbona sikuoni kijiweni wewe!?"
Sasa kwa pale Sirari jina maarufu nilifahamikaga kama mzee wa kuzugia,hii ilikuja baada ya kila sentensi nitakayoongea nilikuwa naweka neno kuzugia au kuzuga na hii kitu nimekuwa nayo hadi leo hii,nadhani ni mazoea tu!.Sasa jamaa baada ya kupokea simu yeye alianza utani wake bila kufahamu kilichokuwa kinaendelea!.
Mimi "Mwanangu nimepata msala!"
Nyamori "Msala gani tena mzee?"
Mimi "Nipo hapa polisi mwanangu,kama vipi mje kunicheki!"
Nyamori "Haina noma mwanangu ngoja niwashitue wana"
Basi baada ya yale mazungumzo nikawa nimekabidhi ile simu tena kwa yule afande.
Kabla ya kuingizwa lupango,tulitakiwa kukabidhi kila tulichokuwa nacho,mimi mpaka muda huo sikuwa na chochote zaidi ya saa ya mkononi na waleti ambayo haikuwa na kitu zaidi ya makaratasi na tiketi za gari!.Basi kwa mara ya kwanza mwanaume nikaingizwa lokapu ambako baada ya kuingia niliona ni heri ukalazwa chooni wiki nzima lakini si mule ndani!.
Muendelezo >
Sehemu ya 8