Nilivyonusurika Kifo baada ya Mzee kunitimua nyumbani - 11.
Nililipa kiasi cha Ksh 50 kwenye Hiace(Shuttle) iliyokuwa ikielekea Kisumu na niliwaambia waniache Migori.Migori ni mji ambao ulikuwa ni mkubwa tu na hapo kabla sikuwahi kufika lakini katika stori za washikaji walikuwa wakidai ni mji ambao ulikuwa jirani sana na Isebania,nilichokua nimepanga ni kwamba nikifika hapo mji wa Migori nitajua cha kufanya,jambo la msingi ni kutoka kwanza hapo Sirari ambapo hali ya hewa ilikuwa imechafuka!.
Nikiwa kwenye gari nilikuwa nimekumbatia kile kibegi ambacho hakikuwa kizito na kiukweli nilikuwa kama nimepagawa na kuduwazwa na ile hali ya hofu niliyokuwa nayo!.Tulitumia takribani nusu saa mpaka dakika arobaini kufika hapo mjini Migori!.
Nilipofika nilishuka na nilitembea kuelekea juu kama narudi tena Sirari,sasa nilipofika kwa mbele nilikutana na jamaa nikamuuliza anielekeze ilipo Guest House ili niende nikapumzike,sasa kwa wale jamaa wao walikuwa wanaita Lodge,ulikuwa ukiuliza neno Guest House kidogo wanakushangaa,basi jamaa akawa amenionyesha Lodge moja ambayo haikuwa mbali na ile stage(stand).
Nilifika pale nikauliza vyumba nikaambiwa ni Ksh 350,nilichomoa hela nikawa nimempa kisha nikaonyeshwa chumba changu!.Kiukweli baada ya kuingia chumbani akili yangu ilitulia sasa!,niliingia bafuni kuoga na nilipomaliza nililala sana na nimekuja kushituka ikiwa mida ya 12 jioni!,basi nikaamua kuamka ili niende kutafuta mahali walipokuwa wanauza msosi ili nitwange nirudi ndani,sasa nilijaribu kumuuliza yule jamaa wa pale mapokezi akawa amenionyesha kimgahawa ambacho hakikuwa mbali na lile eneo,sasa baadae nilikuja kufahamu kumbe mwenye ule mgahawa ndiye aliyekuwa mwenye ile Lodge!.
Nilipofika hapo Migori kiukweli kilichonichanganya ni namna ya kuitumia hela ya Kenya kiusahihi,kuna muda nadhani nilikuwa naibiwa kwasababu sikuwa na muda wa kuanza kuhesabu hesabu vichenji vilivyokuwa vinabaki!.
Sasa wakati natoka Sirari,kwenye lile begi nilikuwa na kiasi cha Tsh milioni 5,na sikufahamu nitazifanyia nini nikiwa hapo Migori!,Sasa asubuhi kulipokucha niliamka mida ya 4 asubuhi nikanawa uso na kupiga mswaki kisha nikaondoka kuelekea pale kwenye kile ki-mgahawa ili kupata chai!.Ule mgahawa ilionekana kwa lile eneo ulikuwa unauza sana kwasababu ile jioni na hata asubuhi nilipoingia nilikuta kuna watu wengi wakipata vyakula mbalimbali,sasa wakati nimeagiza chai na chapati nikiwa nasubiria,ghafla waliingia jamaa wawili wakiwa wamevaa makoti ya kijeshi na suruali za kijani huku wakiwa na bunduki!,nilipata hofu sana lakini nikawa mtulivu,sasa kumbe wale jamaa walikuwa ni askari wa Kikenya na ndivyo walivyokuwa wakivaa,haukupita muda waliongezeka na wengine wawili wakiwa na silaha kama wenzao!.Basi nao walikaa wakawa wameagiza chai wakaendelea kunywa!.
Muda huo nilijikausha kama sina habari na mtu,namshukuru Mungu pia na wao hawakuwa na habari na mtu!,walipomaliza walinyanyuka wakawa wameondoka,sasa nilikuja kugundua kumbe lile eneo nililokuwepo halikuwa mbali na kituo cha polisi hapo Migori na kituo chenyewe kilikuwa barabarani kabisa,niliona lile eneo si sahihi kwangu,hivyo nikapanga ikifika mchana niondoke lile eneo nikatafute Lodge nyingine ambayo itakuwa mafichoni kidogo!. Kiukweli ile hela niliyokuwa nimebadili ilimalizika siku hiyo baada ya kutafuta Lodge nyingine iliyokuwa pembeni ya mji kama unaelekea Kisumu,sasa hofu ilianza kunijaa namna nitakavyoweza kusavaivu kwa kipindi chote nitakachokuwa huko!.
Ilipofika mida ya jioni nilitoka nikaelekea pale stendi kwa mguu na nilipofika jamaa walidhani ni abiria wakaanza kunichangamkia na niliwaeleza mimi si abiria,nilikaa pembeni kujaribu kuangalia namna wanavyofanyakazi lakini kila nikijaribu kuangalia mdau angalau nilete mazoea lakini hola!,kiukweli sikufahamu nitaishije yale mazingira ambayo sikuyazoea!.Utofauti niliuona pale stendi ni kwamba jamaa walionekana kujitahidi kuchangamka lakini bado washikaji na wahuni niliokuwa nikifanya nao kazi pale Sirari walikuwa wamewazidi wale wajaluo kwa uchangamfu!.Basi siku hiyo niliamua kurudi zangu pale Lodge ambako nililala mpaka asubuhi,ilipofika mida ya saa 3 asubuhi nilitoka zangu nikarudi pale stendi kushangaa,sasa nikasogea zilipokuwa zinapaki gari za kuelekea Isebania,pale niliwakuta jamaa wanaongea kikurya hivyo nikajiona kabisa kama nipo Sirari,sasa kuna dogo alikuwa konda akiita abiria kwenye zile shuttle na alikuwa amevaa tisheti iliyokuwa na picha ya Chege na Temba huku ikiwa imeandikwa TMK WANAUME,sasa baada ya kumcheki kwa muda mrefu yule dogo ni kama alinivutia kwa namna alivyokuwa mchangamfu!,sasa baada ya kuitia ile shuttle na kujaza,nilimsogelea kutaka angalau mazoea nae ili ikiwezekana yeye ndiye aifanye ile kazi ya kubadili zile hela wakati nikiwa kule!.
Mimi "Mwanangu mambo niaje?"
Dogo "Ni bomba bro!"
Mimi "Una muda mrefu sana hapa eeh!"
Dogo "Yes bro tuko hapa kitambo!"
Sasa wakati naongea nae hakusita kuniuliza kama mimi ni Mtanzania maana ongea yangu na yake ilikuwa tofauti kabisa!.
Mimi "Unaitwa nani mwanangu?"
Dogo "Mimi naitwa Joe lakini wengi huniita Mkamilifu!"
Dogo "Na wewe bro majina yako nani?"
Mimi " Mimi naitwa Umughaka"
Dogo "Its your first time hapa Migori?"
Mimi "Hapana,huwa nakuja mara kibao tu!"
Dogo "Mi pia huwa nakwenda Sirare kwa jamaa zangu"
Sasa wao kwa kule badala ya kuita Sirari,wao walikuwa wakiita Sirare na hata shuttle zao zote za kuelekea Sirari zilikuwa zimeandikwa Sirare,nadhani ilikuwa ni lafudhi tu lakini walikuwa wakimaanisha Sirari!.Sasa dogo alionekana kupafahamu vizuri Sirari na hata maeneo baadhi niliyomtajia alionekana kuyafahamu!.Pia nilimdanganya kwamba hapo Migori mimi sikuwa mgeni ili isije akawa mkora akatafuta genge la kihalifu wakanifanya kitu mbaya!.
Sikutaka stori nyingi kwasababu sikuwa na hela ya kunivusha siku itakayofuata,nilitaka yeye ndiye akawe chambo wa kubadili zile hela na nilipanga endapo kikinuka basi ningechafua hapo Migori kuendelea kusonga mbele!.
Mimi "Hivi hapa ni maeneo gani wanabadili hela"
Dogo "Ooh kwani una haraka sana bro,huwezi subiri nimalize hii job then nikuonyeshe!"
Mimi "Sawa haina noma"
Basi dogo akaendelea kupambana na ile kazi ya kuita abiria mpaka akawa amejaza tena gari ya pili,hiyo ilikuwa mida ya saa 7 mchana!.
Dogo "Naweza kukuelekeza sasa"
Basi dogo akawa amenichukua mpaka kwenye jengo moja ambalo tukaingia ndani tukakuta maduka kibao,sasa mimi baada ya kuingia mle ndani kiukweli niliona siwezi kubadili zile hela kwenye mazingira yale kwasababu ningedakwa tu!.Sasa nilimchukua dogo nikatoka nae nje nikamwambia twende mpaka kwenye ile Lodge niliyofikia kisha nikamwambia nitamlipa hela ili kufidia muda wake!.Tulipofika kwenye ile Lodge nilimuacha dogo pale mapokezi nikamwambia anisubiri,nilifungua lile begi nikatoa laki moja kisha nikaitia mfukoni nikawa nimefunga kile chumba na kutoka nje!.
Mimi "Nakupa hizi hela naomba ukabadili sehemu nyingine tofauti na pale pa mwanzo kwasababu wale jamaa wanakata hela kubwa"
Dogo "Ok bro kuna jamaa mmoja yupo hapo ng'ambo nampelekea huwa ana-exchange pesa ya Tz,nikukute basi hapa"
Mimi "Nitakulipa vizuri ukifanya vizuri!"
Dogo "Sawa bro nikukute hapa,sa hii tu nakuja!"
Mimi "Uwe muaminifu"
Dogo "Ahahaha bro ndiyo maana nikaitwa Mkamilifu,we uliza watu wote kwa pale stage hakuna ambae hanijui!"
Mimi "Sawa nakusubiri".
Basi dogo alitoka akikimbia akielekea kwa huyo jamaa kubadili ile hela niliyompatia,ile hela kama nilivyosema hapo awali ya kwamba,ulikuwa ukiiangalia kiukweli hakukuwa na shaka yeyote kwamba ilikuwa ni pesa halali kwa matumizi,uenda kama ungeiweka kwenye mashine au ungekuwa na utambuzi wa hela feki ndipo ungeifahamu!.Nilipompa dogo ile hela nilikuwa nina mambo niliyokuwa nayafikiria kichwani,kama angekimbia basi kwangu isingeniuma kwasababu nilikuwa nazo za kutosha,na kama angefanikiwa kubadili basi ndiye angekuwa rafiki yangu kwa kipindi ambacho ningekuwa hapo,lakini pia kama wangemdaka nilipanga kutoweka kama kipanga!.
Basi baada ya kama nusu saa nikiwa pale nje,nilimuona dogo kwa mbali akiwa anakuja!.