...
Kisa cha adam. 2.1
Je, malaika walimuuliza Mwenyezi Mungu?
Katika sehemu hii tunaanza na swali hilo, la kwenye kichwa cha Habari, ambalo In shaa Allah tutalizungumzia kwa kina.
Je, Malaika waliuliza kweli?
Wakati tunaendelea, kwanza tukumbushane kitu ambacho tulikiongelea huko nyuma nyuma kiasi, kijuujuu, nacho ni kua asilimia kubwa sana ya Qur’an, nadiriki kusema zaidi ya asilimia 60 ni visa na hadithi mbali mbali zilizomo ndani ya Qur’an. Kwa kusisitiza; ikiwa hakuna visa na hadithi ndani ya Qur’an basi hakuna Qur’an.
Tunapata na istilahi nyingine “dhikr”, ambayo kama tutavyojionea, mara nyingi inapotajwa “dhikr” katika haya maandiko yetu, inamaanisha kisa, fumbo au hadith ya Qur’an. Hili tutaliongelea kwa kina na kuonesha Ushahidi uliopo ndani ya Qur’an na tutajionea tunavyoweza kujifunza kutokana na dhikr, ambayo ni hadith za Qur’an.
Tutaona pia ndimi “lisan” ya Ibrahim (Abrahamic locution) inavyotolewa kwenye dhikr wakati tunaongelea suala hili la Malaika ambao, eti wamemuuliza maswali Muumba wetu, kama tulivyoaminishwa na watafsiri wengi katika
aya Q 2:30.
Raha ilioje kila tunapogundua njia mpya na za kipekee ambapo Qur’an yenyewe inatufundisha na kuturekebisha mithili ya “advanced software” ya kompyuta kila tunapoendelea kugundua kuisoma kwa kufata mifumo yake ya kutuelimisha.
Kwa hakika ni muujiza kuelewa hayo kutoka kwenye Qur’an yenyewe, ni ya kushangaza na kustajaabisha. In shaa Allah Tutajionea wenyewe kila tunavyoendelea.
Hivi tunaviita moja ya vibainisho “bayyinah” au viashiria vipya tunavyojifundisha kwa pamoja.
In shaa Allah uwe ni ujuzi na elimu yenye manufaa kwetu na kwa wengine wote pia iwe ni sadaka njema kwetu na kwa Waislam wote, waliopo na waliotutangulia.
Tueleweshena na tuelewe kua, hii ni elimu na sio starehe, raha yake isio na mfano ni pale tunapojitambua kua tunaupata ujuzi wa kina wa kuulewa mwongozo wetu wa Qur’an kwa mbinu za Qur’an yenyewe.
Qur’an ni muujiza ambao huwezi kuufananisha kitabu cha mtu yoyote au chochote au mshairi yoyote duniani. Hakuna mbinu za kujifundishia za mtu yeyote zinayoweza kufanana au hata kuzikaribia mbinu za Qur’an.
Kwa kujikumbusha haraka haraka, tulipoipitia aya ya 26 na 27 ya Suratul Baqara tuliona kuhusu (baudhatun) بَعُوضَةًۭ au mbu kwa Kiswahili. Tukajikinaisha kua kilichokusudiwa sio mbu wala mfano wa mbu bali ni moja ya kikundi cha watu katika vikundi vya bani israel ambavyo vimegawanyika lakini daima wako kazini kuwagawanya wengine kwa kuwadunga sumu kama mbu, yaani mradi wawapotoshe tu.
Kutajwa kwa mbu wala kusitustue kwani kwenye Kiswahili pia kwa ulimi (lisan) au “locution” ya Tanzania tuna mifano kama hio mingi tu. Mmojawapo maarufu sana ni pale tunaposema ‘wanyonyaji wenye mirija”, naamini hakuna Mtanzania asiejua maana yake, lakini, anaweza kutokea mtu anaejifundisha Kiswahili au wa kutoka nchi nyengine kabisa yenye Kiswahili lakini haina msamiati huo, asielewe maana ya mirija na wanyonyaji.
Kwaa ufupi, natumai maana ya “locution” au ulimi au “lisan” kwa Kiarabu imeeleweka. Ni msamiati au aina ya neno au maneno yanayotumika sehemu fulani au na watu fulani. Wengine hata kwenye familia tu kuna maneno fulani wakiyaongea, ingawa ni ya Kiswahili lakini kama si mwanafamilia unaweza usielewe kinachoongelewa.
Hii imenikumbusha mfano wa kwetu Tanga, ukiwa baraza za bao, chakula kikiwa tayari nyumbani anaweza kutumwa mtoto akaambiwa “kamwambie babako, kabati limeanguka aje haraka kusaidia kulibeba”. Baba na wanaolewa “lisan” hio wanakua wameshaelewa, chakula tayari.
Au ule utani maarufu wa Ilala; Mume alishikwa na hamu na mkewe alikuwa Jirani na mashoga zake wana sherehe yao. Baba akamtuma mwanae “kamwambie mamako aje haraka kuna nguo za kufuliwa nyumbani”, Mama nae hali ilikua sio nzuri, akamwambia, kamjibu babako “mama anasema washing mashine leo mbovu”. Ni matumaini yangu tumeelewa maana ya “locution”.
Qur’an muujiza wake mmojawapo ni huu wa lisan au “locution”, mfano, miaka mingi sana imepita tokea wakati wa Nabii Ibrahim (Alayhi salaam) mpaka wakati ilipokuja Qur’an, lkini imetumika sana ‘lisan” ya Ibrahim (Abrahamic locution ) ndani ya Qur’an.
Pia zimetumika “locution” za Mussa, Firauni na nyenginezo, tutaziona kila tuvyoendelea, kiasi ni muujiza ulio wazi mpaka leo hii, wa kujiuliza, vipi Mtume Muhammad (Sala Allahu Alayhi Wasalaam) alizijua ndimi hizo za zamani sana? Aliwashangaza sana Mayahudi wa Madina wa wakati wake alipokua akitamka mambo mengine kwa ndimi zao. Hadi leo hii Qur’an inaendelea kuwashangaza mabingwa wa tafiti za kugha kwa jinsi ilivyoandikwa.
Kwenye “table” nilipozichambua (tasil) aya mbili za 26 na 27, nimeziwekea herufi za kwenye mabano (a), (B), (C)... na baadhi ya maneno nimeyawekea rangi (highlight) ya njano ili iwe wepesi kuzirejea tunapozielezea.
Kumbuka kua hatuongelei bani Israel wote bali ni baadhi ya vikundi tu na hivyo ndivyo aya ya 28 na 29 za Suratul baqara zinavyowaelezea;
Ili tuipate maana kusudiwa ya aya za 28, 29 na kuendelea, kwanza tujikite kwa kina kwenye tafsil ya aya ya 26 na 27 na tuipate maana kusudiwa ya aya hizo.
Nakumbusha hapa kwa kubandika tafsiri ya kawaida ya Sheikh Ali Mohsin barwani, ya aya hizo, ambayo inatumika sana kwenye mtandao;
Q 2:26. Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walio amini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi, lakini wale walio kufuru husema: Ni nini analo kusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu? Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila wale wapotovu, 26
Q 2:27. Wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kwisha ifunga, na wakayakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio wenye khasara. 27
Baada ya kuiona hio tafsiri, hapa chini tunaweka ufafanuzi (interpretation) ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia kuiona kwa kutumia mbinu za ki Qur’an za "tafsil" kwa kina, ili kupata maana halisi. Mbinu ambayo tutaitumia kwa kina katika episode hii ya adam na nyinginezo zitakazofata.
Tutajionea kua tumeweka maana tu iliokusudiwa na tumeachana na tarjama na tafsiri kama ilivyozoeleka.
Baada ya huu ufafanuzi wetu, tutapiga mbizi, kuzamia kwa kina kwa tafsil ili tujionee jinsi tulivyoweza kuipata maana hii kwa kutumia mbinu (methods) za Qur’an. Tuanze;
Tafsil (syntactic segmentation) ya Qur’an 2:26 na 27
| Mwenyezi Mungu hatafuti kuleta ugumu katika Maisha. | إِنَّ ٱللَّهَ لَا يَسْتَحْىِۦٓ (A) |
| kwa kupiga mfano wowote | أَن يَضْرِبَ مَثَلًۭا مَّا (B) |
| kwa vikundi miongoni mwa Bani Israeli ambao huchochea vikundi kutokubaliana (yaani, watu wanaopanda mgawanyiko kwa kuuma na kuingiza habari za kupotosha). | بَعُوضَة(C) |
| Kwa maana hawakubali kitu chochote juu yao! (Hakika kundi hili liliwakataa kwa kiburi wale wote walioinuliwa na Mwenyezi Mungu juu yao.) | فَمَا فَوْقَهَا ۚ (D) |
| Na wale walio amini wanaelewa kua hio ni haki itokayo kwa Mola wao Mlezi | فَأَمَّا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ فَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ ٱلْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ ۖ |
| Na wale walio kufuru wanasema Mwenyezi Mungu anataka nini kwa methali hii? | وَأَمَّا ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ فَيَقُولُونَ مَاذَآ أَرَادَ ٱللَّهُ بِهَـٰذَا مَثَلًۭا ۘ |
| (Allah) anaitumia kuwapotosha wengi na kuwaongoza wengi. | يُضِلُّ بِهِۦ كَثِيرًۭا وَيَهْدِى بِهِۦ كَثِيرًۭا ۚ |
| Lakini (Allah) hapotoshi kwayo ila wapotoshaji (Alfasiqin). | وَمَا يُضِلُّ بِهِۦٓ إِلَّا ٱلْفَـٰسِقِينَ
(Q 2:26) |
Qur’an 2:27
| |
| Waliokadhibisha ( ni mbu /baudha) ahadi ya Allah baada ya kuthibitika. | ٱلَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ ٱللَّهِ مِنۢ بَعْدِ مِيثَـٰقِهِۦ |
| Na wanayakata (tenganisha) yale aliyo amrisha Allah yasikatwe (yasitenganishwe) | وَيَقْطَعُونَ مَآ أَمَرَ ٱللَّهُ بِهِۦٓ أَن يُوصَلَ |
| Na wanayafisadi maandiko | وَيُفْسِدُونَ فِى ٱلْأَرْضِ ۚ |
| Wao hao ndio wenye hasara | أُو۟لَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلْخَـٰسِرُونَ ٢٧ |
Itaendelea.
...