Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
NINAVYOMKUMBUKA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE
MWALIMU MTU WA WATU 6
MWALIMU MTU WA WATU 6
Mwalimu alikuwa anazungumza na Profesa Malima nyumbani kwake na katika mazungumzo Mwalimu akamsikitikia Profesa Malima kuwa kuna watu wanamshutumu yeye yeye kuwa hawapendi Waislam.
Mwalimu akanyanyuka alipokuwa amekaa na kwenda chumbani kwake, akatoka na moja ya picha za wakati wa kudai uhuru, akamwonyesha Malima.
Mwalimu akasema, ''Profesa unaona picha hii, Waislam watupu, Mkristo ni mimi peke yangu, vipi mimi leo niwachukie watu walionifikisha hapa?''
Mwalimu amefariki dunia wakati nchi yetu ipo katika hofu ya kuvunjika amani.
Waislam ambao walikuwa mstari wa mbele katika kumpokea Mwalimu na kumuunga mkono na kudai uhuru wanaichagiza serikali iwafanyie uadilifu kwa kuwa wanadai kuna watu ndani ya serikali wameweka maslahi ya dini zao dhidi ya maslahi ya taifa.
Waislam wanadai kuwa CCM kimekuwa chama cha kanisa kikifanya maamuzi kwa maslahi ya Ukristo.
Waislam wameshapambana na askari mara kadhaa na damu imemwagika.
Hii ni hatari ya wazi na inatishia uhai wa taifa letu.
Waislam walioshiriki katika kuleta uhuru wa nchi hii wanashangaa wanaposoma magazeti na kuambiwa na wanasiasa kuwa wao wanataka kuvuruga amani.
Kinachowashangaza ni kuwa vipi wao wapiganie uhuru wa nchi hii kisha wao waanze kuuvuruga.
Lakini kinachowashangaza Waislam zaidi na hasa marafiki wa zamani wa Mwalimu ni ukimya wake Mwalimu katika tatizo hili zito linalotishia uhai wa taifa hili.
Nafasi za mbele katika mazishi na maombolezo watachukua wale waliokuja kumkumbatia na kujidai kumpenda Mwalimu kwa kuwa kwa kufanya hivyo kuna maslahi makubwa kwao.
Lakini kama Mwalimu angeliweza kufunua macho na kuangalia umma unaoomboleza kifo chake kwa hakika kabisa akili yake ingelirudi nyuma zaidi ya miaka 40 na kuwakumbuka rafiki zake waliompokea Dar es Salaam na katika TANU katika miaka ya 1950.
Katika marafiki zake hawa, wengi wametangulia na kumuacha Mwalimu nyuma.
Kwa bahati mbaya wale walio hai kama Mzee Shaaban Gonga, Mzee Juma Mlevi na Mzee Rashid Sisso, historia imekataa kuwatambua.
Kwa ajili hii basi wataomboleza kifo cha rafiki yao kimya kimya na katika upweke.
Mwalimu hatunae tena na kwa hakika ameacha historia ambayo itazungumzwa kwa muda mrefu baada ya yeye kutoweka.
(Kutoka taazia iliyochapwa na Mtanzania, Jumatatu, Oktoba 18, 1999).