May Day,
Ikiwa unataka mimi nifanye mjadala kwa namna utakavyo wewe utanipa shida.
Moja ya namna yangu ya mjadala ni kukwepa ubishi kwani ubishi hauongezi elimu wala kusomesha.
Nimefurahi sana umeniwekea historia ya Wachagga.
Hivi sasa naandika kitabu cha Rajab Ibrahim Kirama (1843 -1962) naamini hili jina hujapata kulisikia katika historia ya Wachagga.
Huyu ndiye aliyeingiaza Uislam Uchaggani na historia ya ukoo huu wake wa Njau kama Majemadari wa Vita inarudi nyuma miaka 300 na imehifadhiwa kwa kumbukumbu za kichwa na kwa ushahidi wa nyaraka zinazokwenda nyuma kiasi cha miaka 100.
Sasa kwa kuwa unasema sina jipya naona nikupe kitu kipya na ni katika haya haya tunayojadili hapa.
Nakuunga mkono katika historia ya Mangi Meli na nakuonyesha kitu kutoka kitabu ninachoandika.
Nimempa Mangi Meli jina kwa utanashati wake na jinsi alivyojaliwa sura jamili.
Nimempa jina ''Handsome Boy.''
Hivi nahangaika kutafuta jina kama hili kwa Kichagga.
Karibu:
''Mwaka wa 1890 Herman von Wissman baada ya kumaliza vita na Abushiri na kumnyonga alielekeza jeshi lake kaskazini na akamshambulia Mangi Sina katika vita vikali ambavyo jeshi la Sina lilionyesha uhodari mkubwa wa mapambano.
Vita hivi vilinyanyua haiba ya Sina na Wajerumani wakanyoosha mkono wa urafiki na huo ndiyo ukawa mwisho wa uhasama baina ya Mangi Sina na Wajerumani.
Juu ya haya Rindi aliungana na Hermann von Wissman dhidi ya Sina na na hii ikapelekea kwa Sina kushindwa vita mwaka wa 1891.
Fitna na usaliti ukawa sasa ni moja ya silaha zilizowapa Wajerumani ushindi.
Sina alifariki mwaka wa 1899 akiwa kaacha sifa ya ushujaa wa vita mbele ya Wajerumani kwani peke yao hawakuweza kumshinda hadi ulipopitika usaliti dhidi yake.
Kunyongwa kwa Mangi Meli Old Moshi mwaka wa 1900 pengine yeye Muro Mboyo akiwa shahidi wa mauaji yale ulikuwa ujumbe tosha kuwa nyakati zimebadika.
Meli kama ilivyokuwa kwa Abushiri na yeye alisalitiwa pia na wale aliokuwa akiwapigania.
Kadhalika kama ilivyokuwa kwa Abushiri kuwa adui wa kweli hakuwa Mjerumani peke yake bali pia nduguze katika ukanda wote wa pwani ambao walikuwa tayari kujiuza kwa Wajerumani.
Haikuwa tabu sana pia kwa baadhi ya watawala wa Uchagani kutambua kuwa adui wa kweli pia hakuwa mtawala jirani yake aliye Kibosho au Machame chini ya Mlima Kilimanjaro bali Mjerumani kutoka mbali.
Hali hii ilikuwa na manufaa makubwa kwa Wajerumani.
Lakini usaliti huu haukuwa uko katika siasa za Wachagga peke yao kwa watawala kufitiana na kusalitiana.
Wajerunani na wao waliucheza mchezo huu kwa mafanikio makubwa kwa kuwaghilibu askari wa Kinubi kutoka Sudan na Wazulu waliowachukua kutoka kijiji kinachojulikana kama Kwa Likunyi, Imhambane Mozambique.
Wissmann alipofika katika kijiji hiki alifanya mazungunguzo na Chifu Shangaan kiongozi wa Wazulu waliokimbia vita vya Chaka na kuingia Mozambique kutafuta hifadhi.
Mkataba alioweka Wissmann na Chifu Shangaan ambae baada ya kufika Tanganyika akajulikana kwa jina la Affande Plantan ilikuwa baada ya kushinda vita Wajerumani na Wazulu wataitawala Tanganyika kwa pamoja.
Jeshi hili la mamluki chini ya Wissmann walipigana dhidi ya Waafrika wenzao kwa tamaa kuwa na wao watakuja kuwa watawala kama Wajerumani baada ya ushindi.
Lakini baada ya Ujermani kushinda vita vyake na kuanza kutawala kwa utulivu hawakutimiza ahadi waliyoweka ingawa walirejesha hisani kwa kuunda jeshi waliloliita Germany Constabulary na mkuu wa jeshi hili alikuwa Affande Plantan.
Hili jeshi liliwekwa ndani ya kambi Dar es Salaam hadi mwaka wa 1918 baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Vya Kwanza Vya Dunia huu ndiyo ukawa mwisho wa jeshi hili Tanganyika.
Wakati wa utawala wao Wajerumani walijenga shule na wakawasomesha watoto wa hawa askari kwa kiwango ambacho watoto wa raia wa kawaida hawakukipata na baada ya kumaliza shule darasa la sita walitoka shule wakiwa wanakisema Kijerumani vizuri na wakiwa na ujuzi mbalimbali na wengi wao waliingizwa jeshini kama askari katika Germany Constabulary.''
(Shule hizi za Wajerumani iliyojengwa Dar es Salaam na shule nyingine zilizojengwa kwengineko huko bara na wamishionari ndizo zilizokuja kuwatoa Waafrika ambao waliacha alama katika historia ya Tanganyika watu kama Joseph Merinyo, Paul Njau kutoka Kilimanjaro, Kleist Sykes, Schneider Plantan, Mashado Plantan kutoka Dar es Salaam, Martin Kayamba kutoka Tanga na wengine wengi ambao walikuja kuutumikia utawala wa Mfalme George wakati wa utawala wa Waingereza na ghilba waliyofanyiwa baba zao na Wissmann ni sehemu ya historia ya wazazi wao.
Hii leo haya ni sehemu ya simuliza katika historia ya Tanganyika vipi wazee wao walifika Tanganyika zaidi ya miaka 100 iliyopita na kuwa sehemu ya utawala wa kikoloni na pia baadae kuwa sehemu ya msingi ya kudai uhuru wa Tanganyika).
Tanbihi: Muro Mboyo ndiye baba yake Rajab Ibrahim Kirama.
View attachment 1526065