Nguruvi...
Ukiondoa lugha kali umeleta hoja nzuri ambazo mimi nimeshazieleza kwingi.
Abdul alifikia mahali hakuweza kusogea mbele khasa pale aliposhindwa kumshawishi Chief Kidaha Makwaia kujiunga na TAA waunde TANU.
Hili la katiba huwa kila nikisoma si kwako tu hata katika Wasifu wa Julius Nyerere hujiambia Mwingereza atapitisha katiba gani ya maana kwa chama cha Waafrika.
Wengi hawajui kuwa hata hiyo TANU katiba yake ilinakiliwa kutoka katiba ya Convention People's Party (CPP)ya Kwame Nkrumah...Earle Seaton huyo.
Na hii katiba si kama ilimsubiri Nyerere afike ndiyo itafutwe.
Lakini kinachonifariji ni kuwa kama alivyogusia Dos Santos ni kuwa Abdul Sykes aliyefutwa katika historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika leo karudi anazungumzwa.
Muhimu ni ukweli kuwa Nyerere alipopanda jukwaani hali ya siasa Tanganyika ilibadilika.
Siku zote nasikitika kwa mimi kutopewa shajara za Abdul Sykes kuzisoma.
Naamini ndani ya shajara zile kuna mengi.
Kleist Abdallah Sykes, Muasisi wa Harakati na Mtu wa Fikra: 1894 - 1949
Historia ya ukoo wa akina Sykes inarudi nyuma kiasa cha zaidi ya miaka mia moja hivi.
Katika miaka hiyo yote ukoo huu umeweza kuhifadhi historia yake kupitia kwa Kleist Sykes mwenyewe ambae yeye alijifunza historia ya kabila lao kutoka kwa mlezi wake, Affande Plantan.
Katika kutaka kupata koloni la Kijerumani katika Afrika ya Mashariki huku wakikabiliwa na upinzani kutoka kwa Waarabu katika pwani, pamoja na upinzani kutoka kwa machifu wa huko bara, Chancellor Otto von Bismarck alimchagua Harmine von Wissman akakomeshe upinzani dhidi ya Ujerumani na kuweka amri moja.
Affande Plantan alikuwa chief wa Kizulu katika kijiji cha Kwa Likunyi Inhambane, Mozambique ambae Herman von Wissman aliwekanae mkataba wa kujanae Tanganyika na kikosi cha askari mamluki wa Kizulu kuja kuwasaidia Wajerumani katika vita vyao na Mtwa Mkwawa na Bushiri bin Salim Al Harith.
Katika jeshi hili alikuwamo Sykes Mbuwane baba yake Kleist ambae alifariki dunia mwaka wa 1894 wakati anarudi vitani baada ya kumshinda Chief Mkwawa na huu ndiyo mwaka aliozaliwa Kleist.
Kleist akawa ndiyo mtu wa kwanza katika ukoo huo kuandika historia hii kabla hajafariki akiacha historia hiyo kama mswada na ukieleza yote aliyoyatenda katika uwanja wa siasa kuanzia kuasisi African Association mwaka wa 1929 na Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika mwaka wa 1933.
Mswada huu wa Kleist ukachapwa kama sura ya kitabu kilichohaririwa na John Iliffe mwaka wa 1973 baada ya kuchapwa kama ‘’seminar paper,’’ Chuo Kikuu Cha Afrika ya Mashariki Idara ya Historia iliyoandikwa na mjukuu wake Aisha ‘’Daisy’’ Sykes, mwaka wa 1968.
Wajerumani walihisi kuwa ikiwa Wazulu walikuwa wamewasimamisha Wareno katika vita wakashindwa kupata ushindi kwa urahisi watu wa Tanganyika hawataweza kufua dafu mbele ya mbinu za Wazulu za vita.
Hii ilikuwa mwaka wa 1894.
Baada ya kuwashinda wananchi wa Tanganyika, Wissman alitunzwa na serikali yake na akafanywa Gavana wa German East Africa kati ya mwaka wa 1895 na 1896.
Wazulu nao kwa kuwa walichangia katika ushindi huo na wao hawakutoka mikono mitupu, Wajerumani waliwatunza.
Kleist alipelekwa kusoma shule ya Wajerumani akajifunza Kijerumani, kupiga chapa na hati mkato, ujuzi adimu na wa thamani sana kwa Mwafrika enzi zile.
Katika nyumba ya Affande Plantan, Kleist alilelewa pamoja na watoto wa Affande Plantan mwenyewe, Schneider Abdillah, Ramadhani Mashado Plantan na Thomas Sauti Plantan mtoto wa ndugu yake wa mbali kidogo.
Watoto hawa wote walipata elimu nzuri ambayo iliwawezesha kuwa watu muhimu katika mji wa Dar es Salaam.
Baada ya kumaliza shule Kleist na Schneider waliingizwa katika jeshi la Wajerumani na wakapigana Vita Kuu ya Kwanza wakiwa askari chini ya Von Lettow Vorbeck.
Katika mswada wa maisha yake Kleist ameandika kitu mfano wa Shajara ya Vita (War Diary).
Shajara hii itamsaidia mtafiti yeyote kujua vita vilikwendaje baina ya Wajerumani na Waingereza pale vita vilipoanza kwa Waingereza kuvuka mpaka kuingia Tanganyika wakitokea Kenya na kukutana na batalioni aliyokuwamo Kleist na Schneider ikitokea Dar es Salaam.
Vikosi hivi viwili vilikutana Mwakinyumbi Tanga ambako Waarabu walingia pia vitani upande wa Waingereza kulipa kisasi cha kuuawa Abushiri.
Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ndipo Kleist akaanza kujihusisha na harakati za Waafrika akiwa muasisi wa African Assocaition mwaka wa 1929 kama katibu kisha akaasisi Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika akiwa katibu muasisi vile vile.
Akiwa Katibu wa African Association akaweza kujenga ofisi ya chama Mtaa wa New Street na Kariakoo kati ya mwaka wa 1929 na mwaka wa 1933.
Mwaka wa 1933 akiwa Katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika akaweza kujenga shule kwa ajili ya watoto wa Kiislam, shule ambayo ilikuwa ikisomesha masomo ya Kisekula pamoja na masomo ya kuujua Uislam.
Kleist akawa mfanyabiashara mkubwa katika jamii ya Waafrika wa Tanganyika na kama mjumbe wa Kamati ya Maulidi na kiongozi wa Waafrika waliokuwa waajiriwa wa Tanganyika Railwways nafasi hizi zilimpa sauti kubwa katika siasa za Dar es Salaam.
Nafasi hizi alizokuwa ameshika na muunganiko viongozi wa African Association na Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ndiyo uliojenga nguvu kubwa ya Waislam ndani ya TANU kiasi cha kuifanya TANU kuchukua sura ya chama cha Waislam.
Mashado Plantan aliajiriwa kama askari akiwa na cheo kilichomtabulisha kama askari anaezungumza Kiingereza na baadae alikuja kuwa mhariri wa magazeti aliyoyamiliki mwenyewe.
Gazeti lake la kwanza likiitwa, ‘’Dunia,’’ na wakati wa Vita Vya Pili Vya Dunia akaanzisha gazeti lililoitwa ‘’Zuhra.’’
Gazeti la Zuhra lilichapa habari muhimu katika jamii ya Waafrika.
Thomas Saudtz alikuja kuwa mwalimu wa shule Mpwapwa na Dar es Salaam na Schneider Abdillah Plantan alikuwa mwanachama shupavu wa TAA na aliungana na Sheikh Hassan bin Amir kama katibu wa Daawat Islamiyya fi Tanganyika (Mwito kwa Waislam) Mwenyekiti akiwa Sheikh Hassan bin Ameir mwenyewe.
Kleist aliwashinda ndugu zake wote.
Alikuwa mtu wa fikra na akaweza kuasisi taasisi nyingi na akaacha nyaraka za picha ambazo ndizo zilizokuja baada ya miaka mingi kupita kusaidia watafiti wa historia ya Tangayika kuijua historia ya African Association kwa ukamilifu wake.
Jina la Kleist likahusishwa na harakati za watu wa Tanganyika katika kupinga dhulma ya ukoloni,
Ikumbukwe kuwa Kleist alikuwa kutoka katika kizazi cha pili katika Tanganyika kutumika katika majeshi kama askari kwanza wazee wake waliomtangulia wakiwa katika jeshi la Wajerumani lililovamia Tanganyika chini ya Herman von Wissman kisha yeye akiwa sehemu ya jeshi la Wajerumani akalitumikia jeshi hilo kupigana na Waingereza chini ya Paul Von Lettow Vorbeck.
Tutaangalia kwanza vipi msingi huu alioacha Kleist Sykes ulivyowafanya Waislam na Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika kuwa sehemu ya chama cha TAA na kwa ajili hii kuwa sehemu ya nguvu ya kupambana na ukoloni wa Waingereza chini ya chama cha TANU kikiongozwa na Julius Nyerere.
Pili tutaangalia vipi wanae Kleist, Abdulwahid na Ally kwa kushughulika katika harakati za kupinga ukoloni na wao pia wakawa na kumbukumbu, nyaraka na picha nyingi ambazo zimesaidia sana katika kuhifadhi historia ya uhuru wa Tanganyika kati ya mwaka 1945 hadi 1961 uhuru ulipopatikana.
Bwana Nguruvi,
Unae mtu yeyote hata Nyerere mwenyewe ambae ana historia kama hii?
Hapa sizungumzii kuhusu vielelezo vya nyaraka na mapicha.