Kama ukiniuliza leo, ni kitu gani kinakwamisha maendeleo ya nchi yetu (Tanzania) basi nitakwambia ni Katiba ya nchi ambayo kiukweli imepitwa na wakati. Tupo karine ya 21 lakini bado tunatumia Katiba ya karne ya 20, ajabu iliyoje hii! Katiba iliyotungwa enzi za utawala wa chama kimoja tunaitumiaje kwenye zama za mfumo wa vyama vingi?
Tunahitaji Katiba ambayo ina wapa mamlaka wananchi siyo katiba inayompa mtu mmoja (Rais) mamlaka. Tunahitaji katiba ambayo itakuwa imeeleza kinaga ubaga juu ya vipaumbele vya taifa siyo kila mtu anayeshika hatamu ndiyo aje na vipaumbele vyake.
Tunahitaji katiba ambayo Rais akimteua Waziri yoyote yule lazima Waziri huyo athibitishwe na Bunge siyo Waziri anateuliwa leo kesho anakwenda kuapa Ikulu! Bunge likijiridhisha kuwa mtu huyo hafai kuwa Waziri, basi hatoapa kushika wadhifa huo hata kama Rais anamwona mtu huyo anafaa kwa kiasi gani!
Tunahitaji katiba ambayo itapunguza matumizi ya serikali kwa kufuta baadhi ya vyeo kama Ukuu wa Mkoa na Ukuu wa Wilaya. Tunahitaji katiba ambayo Mkurugenzi wa Halimashauri, Wilaya na Jiji wawe awe anaomba kazi kwa Halimashauri/Wilaya ama Jiji husika siyo ateuliwe na Rais. DED ndiyo awe Mtendaji Mkuu wa shughuli zote akishirikiana na Mbunge/Wabunge na maafisa walio katika Idara mbalimbali katika eneo hilo!
Tunahitaji Tume huru ya Uchaguzi (Ili tuwe na uchaguzi huru na wa haki) ambayo, Mwenyekiti na Mkurugenzi wake watakuwa ni watu huru, hawa waombe kazi kupitia Bunge, Bunge ndiyo liwathibitishe kwa niaba ya wananchi siyo wateuliwe na mtu mmoja (Rais) ambaye ana masilahi makubwa na chama chake!
Tunahitaji katiba ambayo tutapinga matokeo ya Urais pale tunapoona yana ukakasi. Tunahitaji Katiba ambayo sifa ya mtu kuwa Mbunge ni lazima awe na elimu kwanzia shahada (Digrii) siyo ajue kusoma na kuandika, hizi siyo zama za kujua kusoma na kuandika. Hatupo zama za mawe za kati, tupo kwenye Ulimwenguni wa kidigitali unakua kwa kasi zaidi ya kusoma na kuandika, tunahitaji Mbunge anayeona kwa jicho la tatu siyo maneno maneno tu!
Tunahitaji katiba ambayo Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na viongozi wengine wakuu wakistaafu ama wakiwa bado madarakani washitakiwe ikiwa watakiuka sheria katika kuongoza ama watajihusisha na ufisadi/rushwa ya aina yoyote ile! Tunahitaji katiba inayomtaka kila Kiongozi wa nchi atekeleze vipaumbele vya taifa siyo ILANI ya chama chake, Ilani ya chama siyo kipaumbele chetu!
Tunahitaji katiba inayolipa Bunge nguvu kumwondoa Rais madarakani bila ya yeye kuvunja Bunge ikiwa anakiuka sheria za nchi. Tunahitaji Katiba ambayo Spika/Naibu Spika Bunge anatakiwa kugombea nafasi hiyo yeye mwenyewe siyo kwa kuletewa jina na Kiongozi wa chama chake ama Kiongozi yoyote wa Serikali, pia Katibu wa Bunge awe ni mtu huru (asiye na chama) na aombe kazi kwa Bunge wala asiteuliwe na mtu yoyote yule.
Tunahitaji Katiba ambayo Jaji Mkuu baada ya kuteuliwa na Rais athibitishwe na Bunge, na kama Bunge litamwona Jaji huyo hafai basi Jaji huyo asiape kushika wadhifa huo. Tunahitaji katiba ambayo vyombo vya Ulinzi na usalama havitalinda masilahi ya mtawala yoyote yule bali masilahi ya nchi na wananchi!
Kwa kifupi, tunahitaji Katiba Mpya. Kama taifa tunalotaka kupiga hatua ni lazima tupate katiba mpya ambayo itatoa msingi/dira ya taifa. Tusiwe kama taifa lililo karne ya 17, taifa linalojiendea tu bila kujilikana linakwenda wapi!
#Mwenda ND,