MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi imetoa amri na kumteua dalali wa kukamata nyumba ya mtoto wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Dudley Mbowe na kuipiga mnada kwa kushindwa kulipa Sh milioni 62.7 za waandishi wa habari. Anaripoti Mwandishi Wetu.
Uamuzi huo wa mahakama umetolewa leo tarehe 14 Februari 2024 mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mary Mrio baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume la Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Julai 2023.
Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.
Akiwasilisha hoja mahakamani, Maregesi alidai Mkurugenzi Dudley baada ya wadai kushinda shauri alikubali kulipa lakini baadaye hakutekeleza makubaliano.
"Amekaidi kutulipa tumeona njia sahihi tumekubaliana tukamate nyumba yake namba 9 iliyopo Mtaa wa Feza , Mikocheni B barabara ya Chipaka,"alidai Maregesi.
Akitoa uamuzi huo Naibu Msajili Mrio, alisema mahakama inatoa amri ya kukamata nyumba namba tisa, iliyopo Mtaa wa Feza, Mikocheni B.
"Mahakama inatoa amri ya kukamata nyumba na imemteua Dalali wa Mahakama, Jesca Massawe kutoka Kampuni ya Udalali ya MM Auctioneer &Debt Collectors,"alisema.
Baada ya uamuzi huo, mahakama iliahirisha shauri na kulipanga tarehe 4 Machi mwaka huu kwa ajili ya kupata taarifa ya utekelezaji wa amri hiyo
Walalamikaji hao walipata tuzo tarehe 17 Julai mwaka 2023 mbele ya Mwenyekiti wa CMA, Bonasia Mollel.
Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh milioni 114 baada ya kukaa mezani kwenye majadiliano kwa pamoja kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh milioni 62.7.
Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, tarehe 30 Oktoba, tarehe 30 Desemba mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa tarehe 30 Februari mwaka huu lakini hakulipa.
Chanzo: Mwanahalisi